Zana haramu za uvuvi, yakiwemo
makokoro 365 ya samaki aina ya Sangara na nyavu za timba 2,764 zenye
thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni 106 zilizokamatwa
na idara ya uvuvi katika halmashauri ya wilaya ya ukerewe mkoani Mwanza
zimeteketezwa chini ya usimamizi wa kamati ya ulinzi na usalama ya
wilaya hiyo.
Zoezi la kuteketeza zana hizo haramu za uvuvi, zilizokamatwa
kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana hadi Mei 31 mwaka huu katika mialo
mbalimbali ya ziwa victoria, limefanywa na mkuu wa wilaya hiyo Joseph
Mkirikiti katika kijiji cha Bukongo, ambapo amewataka viongozi wa
serikali za vijiji na kata wanaomiliki makokoro hayo kuyasalimisha kwa
hiyari yao kabla ya hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ukerewe pia ametangaza mkakati wa serikali
katika vita dhidi ya uvuvi haramu, ikiwemo kuwapata waingizaji wa
makokoro pamoja na nyavu za makila na nyavu za timba.
Afisa uvuvi wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Aboubakary
Rutabanzibwa mbali na kueleza baadhi ya changamoto zinazojitokeza wakati
wa uteketelezaji wa zoezi hilo, zikiwemo za wananchi kushindwa kuwataja
wamiliki wa zana haramu za uvuvi na mahali wanapojificha, amewahimiza
wavuvi kuanza kufikiria kufuga samaki kwenye mabwawa badala ya
kujihusisha na uvuvi usioendelevu unaochangia kupungua kwa samaki
wachanga katika ziwa Victoria.
Zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa wilaya ya Ukerewe, inayoundwa na
visiwa 38 wanajishughulisha na shughuli za uvuvi. Sekta hii ya uvuvi
imeajiri zaidi ya watu 80,000 wilayani hapa na pia inatoa ajira na
riziki kwa wananchi wengi wa wilaya hii.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni