Alhamisi, 23 Juni 2016

Rais Magufuli Awaonya Wanasiasa Wanaomchelewesha Kufanya Kazi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amewaonya wanasiasa wanaomchelewesha kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.

Rais Magufuli ameyasema hayo muda mfupi uliopita baada ya kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 
Amesema haiwezekani uchaguzi umepita na mshindi amepatikana lakini wanasiasa hao wanaendeleza siasa ilhali wananchi wanataka watumikiwe wapate maendeleo.

Rais amesema hatawavumilia viongozi wa siasa wenye lengo baya na nchi na kuwataka waweke maslahi ya Taifa mbele badala ya vyama vyao. 
Amewataka kufanya siasa baada ya miaka mitano ambapo wananchi watawapima kile walichokifanya kwa muda wote huo.

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema suala la Kura ya Maoni halikusitishwa kama baadhi ya watu wanavyosema bali iliahirishwa kwa kuwa wakati kura hiyo ilipotakiwa kupigwa Aprili Mwaka jana, Tume ilikuwa na jukumu kubwa la kuandaa uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Lubuva alisema Tume haikuwa na uwezo wa kubeba mambo mawili makubwa kwa wakati mmoja. Jaji Lubuva amesema kutokana na zoezi la Uchaguzi Mkuu kumalizika rasmi, Tume iko tayari kuanza mchakato wa kura ya maoni.

Kuhusu suala hilo la Kura ya Maoni, Rais Dk Magufuli amemhakikishia Jaji Lubuva kuwa serikali italiamualia mara baada ya Tume kulifikisha serikalni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni