Kumekuwepo na taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazotokana na habari iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la tarehe 24 Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari "Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba".
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI
HAUTAPIMWA NYUMBA KWA NYUMBA bali itafanya utafiti wa Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania kuanzia mwezi Septemba 2016 ambapo UKIMWI
utapimwa kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili
ziweze kuwakilisha kaya nyingine nyingi ambazo hazitahusika moja kwa
moja katika utafiti huu.
Utafiti
huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa
kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha
watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.
Aidha,
katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa
chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na
kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia
dawa hizo.
Ifahamike
kwamba, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016
unafanyika nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika
mwaka 2003, wa pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka
2011.
Hivyo,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa
utafiti huu sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa
wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya
asilimia 90.
Utafiti
huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utaendeshwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa
Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS),
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar
(ZAC).
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),
Dar es Salaam,
28 Juni, 2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni