Aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewataka
Watanzania kujali makundi ya watu wenye mahitaji maalumu hususan katika
kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Kauli hiyo aliitoa jana alipotembelea vituo vya watoto yatima jijini Dar es Salaam vinavyoendeshwa
na Waislamu kwa lengo la kuwajenga watoto kiimani. Lengo la ziara yake
ni kushiriki nao katika utekelezaji wa nguzo ya mfungo wa Ramadhan.
Katika
ziara hiyo, Lowassa aliyekuwa ameongozana na waumini mbalimbali wa dini
hiyo, alitembelea vituo vitatu vya yatima ambavyo ni Chakuwama
kilichopo Sinza, Khairat cha Kigogo na Umra kilichopo Magomeni
Mwembechai.
Katika ziara hiyo, Lowassa alitoa msaada wa unga, mchele, mafuta ya kupikia, tende na sukari.
Lowassa
alitoa rai kwa watu wenye uwezo kujiweka karibu na jamii inayohitaji
msaada, ili kuenzi utamaduni wa Watanzania kusaidiana.
“Jamii lazima tuangalie makundi haya kwa kushiriki nao pamoja kwenye mahitaji yao, kula nao pamoja,”alisema.
Mratibu
wa misaada hiyo, Sheikh Rajab Katimba ambaye ni Msemaji wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania, alisikitishwa na baadhi ya Waislamu
wanaofuturisha makundi ya watu wenye uwezo na kusahau makundi ya
wasiojiweza.
“Tusaidiane
Waislamu na inashangaza sana kuona jamii inayohitaji msaada
inasahaulika na kufuturisha wenye kujiweza kiuchumi, siyo mbaya ila
tukumbuke jamii hii yenye uhitaji,” alisema Sheikh Katimba.
Mbali
na salamu hizo, dua zilisomwa na watoto wawili, Fadhia Liziki (3) na
Nasra Ramadhan (3) wa kituo cha Kigogo kuombea amani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni