Jumatatu, 20 Juni 2016

Polisi wazuia ndoa ya mtoto wa darasa la sita mkoani Shinyanga.

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na shirika la Agape linalopambana na uvunjifu wa haki za watoto wakike limefanikiwa kuzuia ndoa ya mtoto wa darasa la sita aliyekuwa anaolewa na mwanaume wa miaka 26 kwa mahali ya ng’ombe 14.

Wandishi wa habari walifika katika kijiji cha Mwigumbi kata ya Maganzo wilayani Kishapu na kukutana na sakata hilo ambapo punde tu baada ya polisi kuvamia eneo hilo wazazi wa watoto hao walikimbia na kujificha pasipojulikana ndipo polisi walipowakamata vijana hao na kuwafikisha katika kituo cha polisi cha Maganzo ambapo Msaidizi wa Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Shinyanga Greyfton Mushi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
 
Aidha baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walioshuhudia tukio hilo walitoa maoni yao na kuiomba serikali kuwachukulia hatua kali wahusika ili iwe fundisho kwa watu wenye tamaa ya kupata mali kwa kuozesha watoto wadogo.
 
John Miyola ni Mkurugenzi wa shirika la Agape alimesema ndoa na mimba za umri mdogo zinachangiwa na baadhi ya viongozi wa kata na vijiji kushindwa kutambua wajibu wao katika jamii huku mkuu wa wilaya ya Kishapu Bi.hawa Ng’humbi akiagiza watendaji hao pamoja na wazazi wanaohusika kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kusheria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni