Mbunge
huyo amehojiwa kwa saa tatu kuhusiana na maneno mengine ambayo
anadaiwa kuyaandika kupitia mitandao ya kijamii kuwa ni ya uchochezi.
Jumatano, 29 Juni 2016
Tundu Lissu Awekwa Rumande Kwa Kukosa Dhamana.
MBUNGE
wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewekwa rumande
kwa kukosa dhamana, mara baada ya mahojiano na Jeshi la Polisi Kanda
Maalum ya Dar es salaam kufuatia kauli yake aliyoitoa jana inayoelezwa
kuwa si ya kiungwana.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika Kituo cha Polisi cha Kati jijini Dar es
Salaam leo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekiri kuwa Lissu amewekwa rumande kwa kukosa dhamana na hataachiwa leo, hivyo atalala huko mpaka kesho.
Alichokiandika Rais Magufuli kuhusu ugunduzi wa gesi ya Helium nchini Tanzania
Jana
ziliripotiwa taarifa kuwa watafiti kutoka chuo kikuu cha Oxford na kile
cha Durham kwa ushirikiano na wataalamu wa madini kutoka Norway
wamegundua uwepo wa takriban futi bilioni 54 za hifadhi kubwa zaidi
duniani ya gesi adimu zaidi ya Helium nchini Tanzania.
Leo
June 29 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe
Magufuli kupitia account yake ya twitter amepost akizungumzia ugunduzi
huo huku akitoa wito kujipanga katika eneo la mikataba.
"Tunamshukuru
Mungu Tanzania tumegundua gesi aina ya Helium(He),wito wangu kwa
wachumi,wanasheria na watanzania wote kwa ujumla tujipange
"Ugunduzi huu utuelekeze kujipanga hasa ktk eneo la mikataba yetu ili rasilimali hii adimu isaidie kuujenga uchumi wetu"
Mfuko wa jimbo la Bunda mjini waweka hadharani
Mfuko wa jimbo la Bunda Mjini halmashauri
ya mji Bunda mkoani Mara umetumia zaidi ya sh.milioni 25 katika kutekeleza
shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni humo katika kipindi cha kuanzia
Januari hadi Juni mwaka huu.
Katibu wa mbunge wa jimbo
hilo,Kaunya Yohana alisema kuwa miradi iliyopewa kipaumbele katika kipindi
hicho ni ya elimu,afya,maji na utawala ili kuwawezesha wananchi kupata huduma
hizo kwa ukaribu.
Alifafanua kuwa shughuli
zilizofanyika ni kuezeka vyumba vya madarasa na kuchimba choo katika shule za msingi
za Kunzugu,Kitaramaka,Nyerere,Bigutu na Bushigwamara pamoja na kununua madawati
katika shule hizo.
Aidha Kaunya alisema pia kwamba
fedha hizo zimechimba kisima na kukarabati tenki la maji katika vijiji vya
Misisi na Mihale pamoja na kujenga ofisi ya serikali ya kijiji cha Rwabu na
kutoa wito kwa wakazi wa wilaya hiyo kushirikiana na mbunge wa jimbo hilo,Esta
Bulaya ili wafikie maendeleo yaliyokusudiwa.
Mahakama Kuu Arusha Yatengua ushindi wa Mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (CHADEMA), yaamuru kurudiwa uchaguzi katika jimbo hilo.
Kesi iliyokuwa inaunguruma kuanzia tarehe 29.02.2016 katika mahakam kuu jijini Arusha imetolewa hukumu leo hii
Katika
shauri hilo aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM jimbo la Longido Dr KIRUSWA
alifikisha mahakamni shauri hilo la kupinga matokeo ya ushindi dhidi ya
mbunge wa Longido mh ONESMO NANGOLE
Akisoma
hukumu hiyo,Jaji MWAGESI alisema kwamba mlalamikaji ndugu Kiruswa
aliwakilishwa na Wakili Dr.Masumbuko Lamwai na Wakili Haraka.
Katika shauri hilo,dai la msingi la mlalamikaji bwana Kiruswa lilikua ni
1.Kutumika kwa lugha ya matusi na kashfa wakati wa kampeni kutoka kwa mh Onesmo Nangole
2.Kuwepo kwa wapiga kura kutoka nchi jirani ya Kenya walioletwa na Mh Nangole
3.kutumika kwa magari ya Chadema kwenye kusindikiza na kubebea masanduku ya kupigia kura
4.Mkurugenzi wa Uchaguzi kutangaza matokeo baada ya mgombea wa CCM kutolewa nje.
5.kutokea kwa vurugu ndani ya chumba cha kuhesabu matokeo
Kutokana
na madai hayo na kwa kuzingatia kanuni,sheria na ushahidi uliotolewa
pamoja na vielelezo na mashahidi wa pande zote mbili,Jaji kutoka
mahakama kuu Bukoba Mh.Jaji Mwagesi alisema;
“Kutokana na kuzingatia viini vyote vya shauri hili kama vilivyosikilizwa na kwa mujibu wa sheria,Natamka kwamba;
Mahakama hii imetengua shauri hili na kwa kujirisha kwamba mchakato mzima haukuwa wa haki."
Jumanne, 28 Juni 2016
Serikali Yakanusha Kupima UKIMWI Nyumba Kwa Nyumba
Kumekuwepo na taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazotokana na habari iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo la tarehe 24 Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari "Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba".
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI
HAUTAPIMWA NYUMBA KWA NYUMBA bali itafanya utafiti wa Viashiria na
Matokeo ya UKIMWI Tanzania kuanzia mwezi Septemba 2016 ambapo UKIMWI
utapimwa kwenye kaya chache ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili
ziweze kuwakilisha kaya nyingine nyingi ambazo hazitahusika moja kwa
moja katika utafiti huu.
Utafiti
huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli iliyochaguliwa
kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na utahusisha
watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.
Aidha,
katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa
chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu na
kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia
dawa hizo.
Ifahamike
kwamba, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016
unafanyika nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika
mwaka 2003, wa pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka
2011.
Hivyo,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa
utafiti huu sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa
wakipitiwa na utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya
asilimia 90.
Utafiti
huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utaendeshwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa
Tanzania Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS),
Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar
(ZAC).
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),
Dar es Salaam,
28 Juni, 2016.
Watano wafariki, 13 wajeruhiwa Jijini Mwanza
WATU
watano wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali ya basi
lenye namba za usajili T. 449 BCB mali ya kampuni ya Super Sami
lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza.
Ajali
hiyo imetokea usiku wa kuamikia leo katika eneo la Bashini Kata ya
Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, baada ya gari hilo kugonga jiwe
lililokuwa barabarani na kusababisha William Elias, Dereva wa gari hilo
kushindwa kulimdu.
Watu
waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Valieth Odede, William Elias
(Dereva) huku mwanaume mmoja na wanawake wawili wenye umri wa miaka 25-
30 majina yao bado yakiwa bado hayajafahamika mpaka hivi sasa.
Majeruhi
katika ajali hiyo ni 13, ambao ni Sophia Miraji, Kibilo Mwacha,
Boniphace Charles na Frank Kunyumi ambao wamelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya awali kutokana na
kujeruhiwa vibaya.
Wengine
ni Stanley Zacharia, Sia Dauson, Hellen Leheke, Michael Leonard, Kudra
Ibrahim (mtoto wa miaka miwili), Zamda Issa, Marieth Christopher,
Elizabeth Simon na Dickson Msamba ambao wamelazwa katika hospitali ya
Rufaa ya Bugando (BMC) jijini hapa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, akizungumzia tukio hilo,
alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hilo kuwa katika mwendo
kasi na kusababisha ashindwe kulimdu basi hilo na kusababisha kupinduka.
Msangi,
alisema kuwa kutokana na ajali hiyo jeshi la Polisi mkoani hapa
linaendelea kuchunguza gari hilo pamoja na kufanya uchunguzi juu ya
ajali hiyo iliosababisha vifo vya watu watano kupoteza maisha na wengine
13 kujeruhiwa.
FFU Jela Miaka 30 kwa Kubaka Mwanafunzi........ Pia Atalipa Faini ya Milioni 15 na Viboko 12
ASKARI
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Raphael Makongojo (25) aliyembaka
aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Korogwe
amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Pia
Makongojo amepewa adhabu kali, ikiwemo viboko 12 pamoja na kuamriwa
kutoa faini ya Sh milioni 15 mara atakapomaliza kifungo chake.
Hukumu
hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Arusha ndani ya chumba cha
faragha (chemba) ambako waandishi hawakuruhusiwa kusikiliza hukumu,
lakini baadaye waliambiwa kwa sharti la hakimu wala waendesha mashtaka
kutajwa majina yao kwa sababu kesi hiyo iliendeshwa faragha.
Awali
kesi hiyo ilianza kwa mshitakiwa kusomewa maelezo yake ya awali
akituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari
ya Wasichana ya Korogwe ambaye hivi sasa amemaliza masomo.
Awali
askari huyo alishushwa pamoja na mahabusu wenzake mahakamani hapo,
lakini kwa kuwa kesi inayomkabili ni ya ubakaji hivyo inasikilizwa ndani
ya chumba cha faragha (chemba) ambako hakuna ruhusa kwa wanahabari
kuandika habari hiyo hadi hapo hukumu itakapotolewa.
Kwa
mujibu wa Kifungu cha Sheria Namba 186 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya Mwenendo wa Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka
(1998) inayosema kuwa bila kujali masharti ya sheria nyingine yoyote
inayohusisha makosa ya kujamiiana, ushahidi au mashahidi watakaohusika
hawaruhusiwi kutolewa kwenye chombo chochote cha habari.
Awali,
mshitakiwa huyo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo na
kusomewa shtaka lake kwa hakimu (jina linahifadhiwa) ambako Wakili wa
Serikali (jina linahifadhiwa) alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa huyo
alitenda kosa hilo Januari 16, mwaka huu katika eneo la Kwa Mrombo, FFU
jijini Arusha.
Alidai
kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 130(1 na
2 a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 16.
Baada
ya hukumu hiyo kutolewa, mama mzazi wa mtoto huyo ambaye hakupenda
kutaja jina lake, aliiomba serikali kuingilia kwa makini sheria
inayohusu makosa ya ubakaji ili adhabu itakayotolewa kwa mbakaji iwe
kifungo cha maisha badala ya hakimu au mahakama kutoa kifungo cha miaka
30.
Atakayempachika Mimba Mwanafunzi Kifungo cha Miaka 30 Jela
BUNGE
limepitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu
kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa
watafungwa jela miaka 30.
Sheria
hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada
kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.
Muswada
huo ulilenga kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa
mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na
umepitishwa kuwa sheria.
Sheria
zilizopendekezwa kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti
Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu;
Kanuni za Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano
Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.
Muswada
huo uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho
ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.
Awali
adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika
kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili
anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Akiizungumzia
sheria hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju
alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio
shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa
sheria ya mtoto.
Kifungu
cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira
yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya
sekondari au ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.
Katika
Sheria ya Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria
ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza
faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.
Wakichangia
muswada huo, wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu
inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo,
baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya
kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.
Mbunge
wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo
na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi
mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kutokana na wahalifu hao kuwa na
mazoea ya kuzoea gereza.
Naye
Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali
kuja na marekebisho hayo pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro
shuleni ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM) alitaka
sheria imtake anayekutwa na kosa hilo kuacha fedha za fidia ambazo mama
atazitumia wakati mwanaume akiwa jela.
Akijibu
hoja ya kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa
utaratibu wa vipimo hivyo utatumika mahakamani na waendesha mashitaka
kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa
na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.
Kuhusu
Sheria ya Taasisi za Kazi, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM),
alitaka adhabu hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija na kutaka kazi ya
kutoza faini hiyo isifanywe na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika
sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii
(SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.
Akijibu
hoja hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Mhagama alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana
waajiri wanaochelewesha michango ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza
sheria waziri ataweka makundi na kuwa kampuni zenye kipato kikubwa
adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.
Jumatatu, 27 Juni 2016
Serikali: “Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume na sheria ya Tanzania”
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju alisema
kuwa mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki na Serikali ilishaweka msimamo
wake katika hilo.
Akizungumza
mapema leo katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika
katika hoteli ya Blue Pearl wa kujadili mapendekezo ya tathmini ya
utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu (Universal Periodic Review), Mhe. Mpanju ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika
mkutano huo alisema mapendekezo yaliyowasilishwa Mwezi Mei mwaka huu
katika mkutano wa Baraza la haki za binadamu uliofanyika Geneva,
serikali ilikubali mapendekezo Mia thelathini (130) na mengine 72
iliyakataa.
“Sehemu
ya mapendekezo hayo serikali iliyakataa kwa sababu kuna mengine yapo
kinyume na katiba, sheria, mila na desturi zetu, kwani katika
mapendekezo hayo yapo yanayotaka mapenzi ya jinsia moja jambo ambalo
haliwezi kukubalika”, Mhe. Mpanju alisema
“Hivyo
wakati mkijadili namna ya kupanga mikakati ya utekelezaji ili serikali
ione umuhimu wa kukubali sehemu ya mapendekezo hayo naomba msijielekeze
kwenye yale yaliyo kinyume na imani”, Mhe. Mpanju alisisitiza
Aidha,
Mhe. Naibu Katibu huyo alisema serikali imefungua milango kwa
kushirikiano na tume, wadau wa haki za binadamu wapeleke serikalini
sababu zenye mantiki ili kuona ni mambo gani ambayo serikali inaweza
kuyashugulikia na kuyatekeleza.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Bwana Onesmo Olengurumwa kutoka taasisi ya watetezi
wa haki za binadamu (THRDC) alisema kuwa wadau wamekutana katika
mkutano huo kujadili ni kwa namna gani wataishawishi serikali ili
iweze kuyakubali mapendekezo yaliyobakia na kuyaweka katika utekelezaji.
Akifungua
mkutano huo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Iddi Mapuri alisema kuwa
mkutano huo umelenga katika kuweka mikakati ya ufuatiliaji wa
utekelezaji wa mapendekezo hayo na alipongeza mchango mkubwa unaotolewa
na wadau wa haki za binadamu katika kuhakikisha masuala ya haki za
binadamu yanapata msukumo mkubwa hapa nchini.
Watu 35 wajeruhiwa kwa ajali ya gari wilayani Bunda
Mwandishi wetu Christopher Mareges
Zaidi ya watu 35 wamejeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka
mjini Bunda katika kijiji cha Sarawe kupinduka katika eneo la Kisangwa katika
barabara kuu ya Bunda-Nyamuswa.
Ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Mezida yenye namba za usajili
T 176 BER ilitokea majira ya saa 4.15 asubuhi baada ya gari hilo kupasuka tairi
moja ya mbele hali iliyopelekea liache njia na kuanguka pembeni mwa barabara.
Baadhi ya majeruhi wa ajali
hiyo walisema mara baada ya kuanguka kwa
gari hilo lililokuwa wazi nyuma,abiria walianza kuruka ili kujiokoa hali
iliyosababisha wengi wao wavunjike mikono huku wengine wakijeruhika vibaya
sehemu mbalimbali za miili yao.
Jeshi la polisi wilayani humo limethibitisha kutokea kwa ajali
hiyo na kwamba linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na ajali hiyo huku
likiwa halijashikilia mtu yeyote kwa mahojiano.
Jumamosi, 25 Juni 2016
Wajawazito watakiwa kuwahi kliniki mapema
Na mwandishi wetu Gharos Riwa
Wazazi katika jamii wametakiwa kuzingatia suala la kuwahi
kliniki mapema ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea kwa mama mjamzito na mtoto aliyeko tumboni .
Rai hiyo ilitolewa na Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto
kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Bunda Mkoani Mara Bi Elizabeth Boniphace katika mahojiano
maalum na blog hii.
Akielezea umuhimu wa
kuwahi mapema kliniki bi Elizabeth alisema kuwa mama mjamzito atakuwa salama
zaidi na kuepukana na dalili za hatari zinazoweza kumpelekea kupata madhara
dhidi yake na kwa mtoto aliyeko tumboni
na kuwasisitiza wana ndao kuona umuhimu wa kutambua dalili hizo mapema.
Pia alishauri jamii hasa wana ndoa kufanya mpango binafsi
mpema ya mama mjamzito kujifungua ili kufanya wanafamilia kumpokea mtoto
atakayezaliwa huku akisistiza kuwa ni muhimimu kufahamu tarehe ya makisio ya
kujifungua kwa mama mjamzito.
Naye kwa upande wake Afisa mradi, katika mradi wa afya ya
uzazi ,mama mjamzito, watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka
mitano Kutoka katika shirika la Msalaba
Mwekundu wilayani Bunda Kizaro Mwakoba alisema kuwa wanaume wengi kwa wanandoa wamekuwa waoga kuongozana na waenza
wao kwenda kliniki kwa kuogopa kupima virusi vya ukimwi.
Alisema kutoka na changamoto hiyo inawapa ugumu kwama
wahamasishaji kutambua idadi ya wanandoa wanaoudhuria kliniki na waenza wao.
Aidha pamoja na changamoto hizo aliwasihi wana jamii kuona
umuhimu wa kuongozana kwenda kliniki kwa kuwa lengo ni kuokoa maisha ya mtoto
aliyeko tumboni kwani haita kuwa furaha kwa wanafamilia na jamii kwa
ujumla kama katika familia hiyo baba,mama,
na mtoto aliyezaliwa wote ni waathirika.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)