WAZIRI
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametishia
kuwafutia usajili baadhi ya madalali wa ardhi na nyumba, kutokana na
utendaji wao unaokiuka sheria wakati wa uuzwaji wa nyumba.
Kwa
mujibu wa Lukuvi, nyumba nyingi zimekuwa zikiuzwa bila kufanyiwa
tathmini ya gharama zake halisi na hata zilizofanyiwa wahusika wamekuwa
hawashirikishwi.
Lukuvi
alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokutana na madalali wa
kampuni mbalimbali, ambapo aliwaeleza malalamiko anayoyapata kutoka kwa
wananchi ambao nyumba zao ziliuzwa kwa utaratibu usioeleweka.
“Madalali
mmekuwa mkiuza nyumba bila kujali thamani ya mali husika na wengine
mnauza kwa bei ya chini, wengine mnauza kwa bei ya deni lile lile, huo
ni uonevu wa hali ya juu huku mkitambua mnaowafanyia ni maskini,”alisema.
Alisema
asilimia kubwa wanaokumbwa na uonevu huo ni wanawake wajane kutokana na
kutojua kama mali walizoachiwa na waume zao kama ziliandikishwa katika
mkopo wa benki.
Waziri
Lukuvi aliongeza kuwa madalali wengi wamekuwa wakikiuka sheria za
uuzaji wa nyumba pamoja na mali za masikini kwa bei ya chini, huku
wengine wakifanya mnada katika siku za mwisho wa wiki.
“Madalali
wengi wamekuwa wakiuza mali za watu kwa kisingizio cha amri ya mahakama
tena kwa bei ya asilimia 25 badala ya 75 kama sheria inavyotaka huku
mkijua kufanya hivyo ni uonevu na wizi.
“Ninazo taarifa zenu na hata majina yenu nayajua, nitawafutia usajili na majina yenu kutangazwa katika gazeti la Serikali,”alisema.
Waziri
Lukuvi alisema madalali wengi wamekuwa wakifanya mnada wa kuuza mali
wakati tayari wakiwa wameshapata wanunuzi na wengine wakiwa wameshatoa
fedha za awali.
Alisema
amepata malalamiko ya watu 84 kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao
wameonewa kwa namna moja au nyingine na madalali wanaoshirikiana na
baadhi ya maofisa wa benki kwa kuwauzia au kuwabomolea nyumba zao
kinyume cha utaratibu.
Katika
hatua nyingine Waziri Lukuvi aliwataka madalali hao kupeleka taarifa
zote za mali husika kabla ya kupigwa mnada kwa msajili wa ardhi na
nyumba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni