Jumatano, 5 Oktoba 2016

Kubenea kizimbani tena kwa kupotosha

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kuandika makala ya kupotosha na kusababisha hofu kwa jamii.

Kubenea, ambaye ni mbunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Dereck Mukabatunzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Wakili Mukabatunzi alidai kuwa Julai 25, mwaka huu katika Mtaa wa Kasaba, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Kubenea alichapisha habari ya uongo inayoweza kusababisha hofu na taharuki kwa jamii au kuondoa amani.

Inadaiwa Kubenea alichapisha makala hiyo kwenye gazeti la Mwanahalisi la Julai 25 hadi 31, mwaka huu, lenye namba 349 ISSN: 1832-5432 ikiwa na kichwa cha habari “Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar”.

Baada ya kusomewa mashitaka, Kubenea alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni