Serikali inakamilisha Muswada wa Sheria utakaoweka wazi sifa za walimu wakiwamo wa vyuo vikuu, msingi na sekondari nchini.
Hayo
yalisemwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi , Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako katika kongamano la kujadili hali
halisi ya elimu nchini lililoandaliwa na walimu wastaafu.
Profesa
Ndalichako alisema serikali pia inaandaa mpango wa kuanzisha chombo
maalum cha kitaaluma kitakachosimamia walimu kwa mujibu wa sheria.
Alisema muswada huo utakapokuwa tayari utawasilishwa bungeni.
Alisema
pamoja na mambo mengine, utataja sifa za mwalimu mkuu na mkuu wa chuo
kuondoa dhana kwamba ualimu ni kazi ya walimu mazoea.
“Ni lazima kuwe na sheria inayoweka wazi sifa ya mwalimu mkuu wa chuo kikuu na sifa za kuweza kujiunga na chuo cha ualimu.
“Siyo kuweka tu sheria zisizojieleza hali ambayo imesababisha taifa kuwa na wasomi wasiokuwa na sifa.
“Ili
tuweze kufikia katika mpango wa kutoa elimu bora ni lazima tuchukue
hatua zinazostahiki kwa manufaa ya taifa ingawa unapochukua hatua
Watanzania wengi wanalalamikia suala hili ila ukweli utabaki kuwa
ukweli.
“Nchi haiwezi kuendeshwa na walimu wasiokuwa na sifa kwa sababu kitakachozalishwa pia kitakuwa ni mtihani na aibu kwa nchi.
“Kama
kuna mwalimu yeyote ambaye anajijua hana sifa na amekalia kiti hicho
kwa zaidi ya miaka 10 atambue kuwa hicho kiti atakiacha.
“Serikali hii ya awamu ya tano hatutaki kuwa na walimu wasiokuwa na sifa, bora kujiengua mwenyewe,”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri
alisema changamoto kubwa inayoikabili wizara yake ni utekelezaji wa
mipango endelevu ya wizara ambayo ni mizuri lakini utekelezaji wake ni
mdogo kutokana na kuingiliana kwa mipango ya maendeleo endelevu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni