Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka watu
wote nchini wanaohodhi mashamba makubwa na kutoyaendeleza wafanye hivyo
ndani ya mwezi mmoja kabla hayawanyang’aya mashamba hayo kwa mujibu wa
sheria na mamlaka aliyonayo.
Akizungumza jana na wananchi mkoani Pwani wakati wa zoezi la kuzindua kiwanda cha kusindika matunda, Rais Dkt. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji wanaotaka kuja nchini kuwekeza wafanye hivyo kwa kuwa ardhi ipo ya kutosha.
“Nataka
watu wote wanaotaka kuja nchini kuwekeza waje, kwa kuwa ardhi ya
kutosha tunayo na nawataka watu wote waliohodhi ardhi hata kama walikuwa
viongozi huko nyuma nataka wayalime ndani ya mwezi mmoja na kama
wasipofanya hivyo nitabatilisha hati zao za umiliki na kuwapa watu
wengine ambao wapo tayari kuendeleza ardhi hiyo" Alisema Rais Dkt. John Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema
baadhi ya wafanyabiashara wa sukari nchini wamekuwa siyo waaminifu kwa
kuagiza sukari kwa ajili ya matumizi ya viwandani kutoka nje ya nchi
sukari ambayo ikifika nchini huiweka kwenye mifuko na kuiuza kwa
matumizi ya kawaida ya nyumbani jambo linaloweza kuathiri afya za
watumiaji.
“Tatizo
la sukari liliingia baada ya kuanza kuifuatilia sukari ili sukari
inayopakiwa kwa matumizi ya binadamu iwe hivyo ndipo wafanyabiashara
wakaanza kuficha sukari, ndiyo maana ninataka wawekezaji waje hapa
kuwekeza katika kilimo cha sukari ili sukari izalishwe hapa nchini” Alisema Rais Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo Rais Magufuli alikemea
tabia ya watu kuficha pesa na wengine kuzigeuza katika mfumo wa dolla
na kuzificha chini ya ardhi na kusisitiza wanaofanya hivyo mwisho wake
watakuta pesa hizo zimeharibika huku akiwataka wazitumie kuwekeza katika
viwanda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni