Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelaani
vikali mauaji ya watafiti wawili wa kituo cha Utafiti wa Kilimo cha
Selian cha Arusha na dereva mmoja waliokuwa kazini katika kijiji cha
Mvumi Makulu, wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.
Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo 4-Oct-2016 wakati
akifungua kongamano ya 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) katika ukumbi
wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Makamu
wa Rais amesema kuwa tukio hilo ni baya na amewahakikishia watafiti
wanaoshiriki kongamano hilo kuwa Serikali itachukua hatua stahiki kwa
watu waliofanya kitendo hicho cha kinyama ili kukomesha tabia hiyo.
“Haiwezekani
hata kidogo watu kufanya mauaji hayo ya kikatili na waachwe bila
kuchukuliwa hatua kali za kisheria alisisitiza Makamu wa Rais”
Akizungumzia
masuala ya utafiti, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali
inatambua kazi nzuri inayofanywa na watafiti hao hivyo Serikali
itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali ili kuhakikisha watafiti
hao wanafanya kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.
Makamu
wa Rais pia amewahimiza wafadhili waendelee kusaidia watafiti hasa
wanaofanya tafiti za afya nchini kwa sababu tafiti hizo zitasaidia kwa
kiasi kikubwa namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Amesema
kuwa watafiti wanamchango mkubwa katika kuleta maendeleo kupitia
matokeo ya tafiti zao nchini hivyo jitihada hizo ni muhimu zikaimarishwa
ipasavyo.
Kongamano
hilo la 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu -NIMR- linajumuisha watafiti
mbalimbali kutoka Ulaya, Afrika na Amerika.
Katika
kongamano hilo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia
Suluhu Hassan ameshiriki katika zoezi utoaji wa tuzo kwa wanasayansi
waliofanya tafiti mbalimbali za afya nchini.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam.
4-Oct-2016.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni