TAMKO
LA BODI YA WADHAMINI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA
WANANCHI) KUFUATIA KIKAO CHAKE KILICHOFANYIKA JANA, TAREHE 2 OKTOBA,
2016
Kwa
kuzingatia hali iliojitokeza katika chama chetu cha THE CIVIC UNITED
FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kufuatia hatua ya makusudi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kutupandikizia vurugu
na fujo kwa kujipa mamlaka asiyokuwa nayo ya kutuamulia nani awe
Mwenyekiti wa Chama, hatua ambayo imesababisha mtu anayeitwa Ibrahim
Haruna Lipumba na genge lake tarehe 24 Septemba, 2016 kuvamia na kuhodhi
jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Bodi ya
Wadhamini ya Chama iliona kuna haja ya kukutana na kuchukua hatua za
kukabiliana na matukio hayo.
Bodi
ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi)
imefanya kikao chake, tarehe 2 Oktoba, 2016 katika Makao Makuu ya Chama,
mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Abdallah Said Khatau.
Tumefanya
hivyo kwa kutambua wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa,
Sura 258 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Political
Parties Act, Cap 258) na Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014).
Ni
vyema ieleweke kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila
chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kinapaswa kuunda Bodi ya
Wadhamini ambayo ndiyo inayokuwa mmiliki na msimamizi wa mali zote za
chama cha siasa husika. Kifungu cha 21 cha Sheria ya Vyama vya Siasa
kinalieleza hilo kama ifuatavyo:
“21.
—(1) Every political party which has obtained a certificate of full
registration shall appoint a board of trustees to manage the properties
and any business or investment of the party.
(2)
Every board of trustees shall be duly incorporated under the Trustees
Incorporation Act and every party shall, not later than sixty days from
the date of full registration, submit to the Registrar—
a) the names and addresses of the members of ther board of trustees; and
b) a copy of the certificate of incorporation.”
CUF
kilitimiza masharti hayo ya kisheria kwa kuunda Bodi ya Wadhamini, na
Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014), Ibara ya 98 ikafafanua zaidi
namna inavyopatikana, pamoja na nguvu na uwezo wake kichama, kama
ifuatavyo:
“98._
(1) Kutakuwa na Bodi ya Wadhamini ya Chama itakayoteuliwa na Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka
mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda wake
kumalizika.
(2)
Bodi itakuwa na wajumbe wasiozidi tisa (9), watano (5) kutoka Bara
angalau wawili (2) wakiwa ni wanawake na wanne (4) kutoka Zanzibar
angalau mmoja (1) akiwa ni mwanamke ambao watateuliwa kwa masharti
yanayohitajika ya Sheria ya Bodi ya Wadhamini na utaratibu uliowekwa na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
(3)
Bodi ya Wadhamini itakuwa ndiyo mdhamini pekee wa fedha na mali za
Chama pamoja na madeni na itafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizowekwa na sheria ya nchi inayohusu Wadhamini.
(4) Bodi inaweza kushitaki au kushitakiwa kwa niaba ya Chama.
(5)
Bodi itawajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama ambalo
linaweza kuweka utaratibu unaofaa wa kuendesha shughuli za Bodi hiyo, na
itafanya vikao vyake angalau mara mbili kwa mwaka.
(6)
Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini watachaguliwa na
Wajumbe wa Bodi kutoka miongoni mwao, kwa sharti kwamba Mwenyekiti
akitoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Naibu Mwenyekiti atatoka
upande mwengine wa Jamhuri ya Muungano.”
MAAMUZI YA BODI YA WADHAMINI:
Kufuatana
na uwezo wake uliotajwa hapo juu na kwa kuzingatia nafasi yake kama
mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama (rejea Ibara ya 98(3)
iliyotajwa hapo juu, Bodi ya Wadhamini imefikia maamuzi yafuatayo:
1.
Imepuuza wito wa mtu anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba alioutangaza jana
kwamba eti amemtaka mtu mwengine anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao
cha Bodi ya Wadhamini. Lipumba kwa sasa si Mwenyekiti tena wa CUF na
pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa.
2.
Itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama kama
inavyotakiwa na Ibara ya 98(5) ambalo ndilo linaloiteua Bodi na
litaheshimu maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa likiwa ndiyo
chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa Chama.
3.
Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya
98(3) na 98(4) kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za Chama
zilizovamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Ibrahim Lipumba na genge lake
ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam.
4.
Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya
98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka alipe gharama na hasara zote
alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama,
tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza na
genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na
hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban
Sh. 600 milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es
Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban
Sh. 50 milioni.
5.
Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya
98(4) kwa kumshtaki Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuingilia maamuzi
halali ya vikao halali vya Chama na kulazimisha kukichagulia Chama chetu
Mwenyekiti kinyume na onyo lililowahi kutolewa na Mahakama Kuu dhidi ya
Ofisi yake kutokuwa na mamlaka ya aina hiyo.
6.
Inawahakikishia wanachama wote wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar
kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na itasimama pamoja nao kulinda
mali zote za Chama.
7. Inaionya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwache kuingilia mambo ya ndani ya uongozi na uendeshaji wa Chama cha CUF.
HAKI SAWA KWA WOTE
Abdallah Said Khatau
MWENYEKITI WA BODI
Joran Lwehabura Bashange
KATIBU WA BODI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni