Jumatano, 5 Oktoba 2016

CUFwazidi Kunogasha.......Bodi ya Wadhamini Nayo Yagawanyika Viipandevipande

Bodi ya wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imegawanyika vipande viwili  kutokana na mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama hicho.

Kugawanyika kwa bodi hiyo kumekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wake, Abdallah Katau kutangaza kutomtambua Profesa Lipumba, huku baadhi ya wajumbe wakipinga tamko hilo wakiliita ni batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wajumbe wenzake, mjumbe wa bodi ya chama hicho, Peter Malebo, alisema hawatambui tamko lililotolewa na mwenyekiti wao kwani bodi hiyo inajiandaa kuwakutanisha mwenyeki wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad ili kuweza kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Alisema kutokana na hali hiyo, watakaa na wajumbe wenzao na kujadili suala hilo kabla ya kuwaita viongozi hao ikiwa ni pamoja na kujadili ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

“Tutakaa na wajumbe wenzetu ili tuweze kujadiliana mgogoro wa viongozi wetu pamoja na kupitia maazimio ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ili tuweze kupata hoja ya kuwahoji kwenye kikao hicho.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa chama chetu kinarudi kwenye hadhi yake kama ilivyokua awali kuliko hivi sasa ambapo kimegubikwa na mgogoro wa uongozi wa kitaifa,” alisema Malebo.

Alisema ikiwa watashindwa kupata mwafaka wataitisha Mkutano Mkuu wa dharura  ili waweze kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo hali ya chama na hatua za kuchukua.

“Kama mwafaka hautapatikana katika kikao hicho, tutalazimika kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu ambao pamoja na mambo mengine, tutawaeleza mgogoro wa viongozi wetu ili wajumbe waweze kutoa uamuzi,” alisema.

Alisema Bodi ya Wadhamini wa CUF inaundwa na wajumbe wanane ambapo kutoka upande wa bara ni watano na Zanzibar watatu.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni pamoja na Abdalah Katau, Peter Malebo, Ally Mbarouk, Amin Mrisha, Zacharia Kwangu, Yohana Mbelwa na Dk. Juma Muchi.

Alisema mpaka sasa bodi hiyo imegawanyika ambapo wajumbe kutoka Zanzibar wanamwunga mkono Maalim Seif huku wale wa bara wakimwunga mkono Profesa Lipumba hali inayozidi kupandisha joto ndani ya chama hicho.

“Kinachotutafuna  ndani ya CUF ni ubaguzi unaoonyeshwa waziwazi kutoka kwa viongozi wa Zanzibar jambo ambalo limechangia kila mtu kuwa upande wake, lakini tutaitana na kujadiliana suala hili ili tuweze kupata mwafaka,” alisema.

Alisema bodi hiyo inafanya kazi ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo iliteuliwa mwaka 2011 na itamaliza muda wake, Desemba mwaka huu.

Atoa onyo Chadema
Katika hatua nyingine, Malebo aliwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoingilia mgogoro huo kwa madai hauwahusu.

Alisema, kitendo cha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Profesa Lipumba inaonyesha wazi kuwa ameshiriki kuongeza mgogoro ndani ya chama hicho.

“Mbowe haumhusu mgogoro wa viongozi wa CUF, huu ni mgogoro wa ndani ya chama, tunamshangaa kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Lipumba, yeye ni nani ndani ya chama?, tunamuonya asirudie,” alisema.

Alisema, chama hicho kimejipanga kupambana na watu wanaoingilia mgogoro wao wakati si wanachama wa chama hicho, jambo ambalo limechangia kuendelea kuchochea vurugu hizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni