Rais
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange ameweka
jiwe la msingi la jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA) ambalo limejengwa kwa lengo la kuwaweka pamoja
wadau wote wanaotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni
juhudi za kuboresha huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji wa bandari
hiyo.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na kati imefanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2016 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Akizungumza
kabla ya kuwekwa jiwe hilo la msingi Rais Magufuli ameishukuru Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa mteja mkubwa wa bandari ya Dar es
Salaam na amesema aliamua jiwe la msingi la jengo hilo liwekwe na Rais
wa Kongo kwa kutambua umuhimu wa nchi yake katika biashara ya bandari ya
Dar es Salaam na pia undugu na urafiki wa kihistoria uliopo kati ya
nchi hizi mbili.
Rais
Magufuli amemhakikishia Rais Kabila kuwa kama ambavyo Serikali yake
imechukua hatua kadhaa za kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika bandari
hiyo, itaendelea kujenga mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa
Kongo kutumia bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya
rushwa, kuongeza muda wa kutunza mizigo inayoshushwa kutoka siku 14 hadi
siku 30, kuanzisha bandari kavu katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na
kuinua ari ya wafanyakazi wa bandari kutoa huduma bora.
"Mhe.
Rais Kabila bandari yetu ilifikia mahali pa kuandika rekodi ya kupotea
kwa meli kwenye taarifa za bandari, kuna wakati hapa zilipotea meli 60,
lakini pia mizigo ya watu ilikuwa inapotea na wafanyabiashara walikuwa
wanaombwa rushwa.
"Kuna
baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliifanya hii bandari kama mali yao,
walikuwa wanaondoka na fedha za rushwa kwenye buti za magari, naomba
nikuhakikishie kuwa haya hayatatokea tena, na yakitokea Mhe. Balozi wa
Kongo upo hapa njoo unieleze mimi au mwambie Makamu wa Rais au Waziri
Mkuu" amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli pia amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania na kwamba anaamini litasaidia kuimarisha
biashara kati ya Tanzania na Kongo na nchi nyingine zinazotumia bandari
ya Dar es Salaam.
Kwa
upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila
Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa heshimu kubwa aliyompa yeye na
nchi ya Kongo ya kuweka jiwe la msingi la jengo hilo na amesema kutokana
na Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za bandari ya
Dar es Salaam mizigo ya Kongo itapitia bandari hiyo.
"Mhe.
Rais Magufuli bandari hii ipo Dar es Salaam lakini bandari hii ni ya
kwetu sote, mashariki ya Kongo inapakana na nchi nne za Tanzania,
Rwanda, Burundi na Uganda lakini asilimia 50 ya mizigo inatoka Tanzania
hususani katika bandari ya Dar es Salaam.
"Nimefurahi
pia kuwa katika juhudi za Tanzania kuboresha bandari pia mnaboresha
barabara na bandari ndogo ndogo za ziwa Tanganyika, hili ni jambo muhimu
kwa sababu sasa mizigo ya Kongo itasafiri kwa urahisi na wafanyabishara
wa Kongo waliokuwa wameacha kutumia bandari ya Dar es Salaam watarudi" amesema Rais Kabila.
Mhe.
Joseph Kabila Kabange amesema katika miaka ya 70 na 80 Kongo ilikuwa
ikizalisha shaba kiasi cha tani laki 1 lakini hivi sasa inazalisha hadi
tani Milioni 1.2 na zote hizi zinategemewa kusafirishwa nje ya nchi
kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Ameipongeza
Serikali ya Tanzania kwa kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na
ameunga mkono mpango wa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya
Tanzania na Kongo huku akibainisha kuwa nchi yake pia itanunua ndege kwa
ajili ya kuimarisha zaidi usafiri wa anga kati ya nchi hizi mbili.
Mapema
kabla ya Marais wote wawili kuzungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deodatus Kakoko alisema
jengo hilo lina ghorofa 35, urefu wa meta 157, ukubwa wa meta za mraba
65,115 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2016 kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 130.
Rais
Kabila ambaye aliingia hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa
ziara ya kiserikali ya siku tatu, jioni ya leo atahudhuria dhifa ya
kitaifa katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa
ajili yake na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni