WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amelaani kitendo cha wanakijiji kuwaua watumishi
wa Serikali waliokuwa wakifanya utafiti wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 3, 2016) wakati akizungumza
na waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya utaratibu
wake wa kukutana na makundi mbalimbali.
Mauaji
ya watafiti hao, Teddy Nguma, Jafari Mafuru na dereva wao Bw. Nicas
Magazine yalitokea Oktoba Mosi, 2016 baada ya kushambuliwa na wakazi wa
kijiji cha Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Amesema
Serikali imesikitishwa na mauaji ya watu watatu wakiwemo watafiti
wawili kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Seliani (SARI) kilichopo
mkoani Arusha ambao walikuwa kazini kuchunguza sampuli za udongo ili
kubaini kama matetemeko yataendelea kutokea.
“Kutokana
na tetemeko lilitokea mkoani Kagera, Serikali iliamua kushirikisha
watalaamu mbalimbali kufanya uchunguzi kuona kama tetemeko hilo ni
endelevu au la katika maeneo mengine. Kitendo cha watu kujichukulia
hatua mkononi na kukatisha uhai wa watumishi ambao walikuwa kazini
hakikubaliki,” amesema
.
Amesema watalaamu hao walifika katika Wilaya ya Chamwino na kufanya
kazi kwa siku tano na siku ya sita ndipo walipoenda eneo la kijiji cha
Iringa Mvumi kuendelea na kazi ambapo waliuawa wakiwa kazini.
“Serikali
kupitia kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa inaendelea na uchunguzi wa
kuwabaini watu waliofanya kitendo hicho’’ amesema. Hata hivyo, Waziri
Mkuu amewatoa wasiwasi watumishi wanaohamia Dodoma kuwa Dodoma ni salama
na kila anayekuja yupo salama. “Dodoma ipo salama na tunatarajia kila
anayehamia hapa atakuwa salama na hata wakazi wa hapa wataendelea kuwa
salama,’’ amesema.
Akizungumzia
kuhusu migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini,
Waziri Mkuu amesema hali hiyo inajitokeza hivi sasa baada ya wananchi
wengi kutambua thamani ya ardhi.
Amesema
miaka ya nyuma watu wachache walitambua thamani ardhi hivyo kuchukua
maeneo makubwa na kuyamiliki. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa
migogoro hiyo inamalizika kwa kuweka kuweka msisitizo kuwe mipango ya
matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kupima ardhi yote na kutoa
hati kwa wananchi.
“Tunataka
ardhi yote ipimwe na kila mtu anayepewa ardhi apewe hati ya kumiliki na
si vinginevyo’’ amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu aliwaasa waandishi
wa habari wawe makini na kazi yao na wajiepushe na upotoshaji kwenye
taarifa wanazozitoa kwa wananchi. Amesema vyombo vya habari ni kiungo
muhimu baina ya Serikali na wananchi, hivyo aliwataka viongozi wote wa
umma washirikiane na vyombo vya habari kwa kutoa habari za utekelezaji
wa kazi za Serikali.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea msaada wa sh. milioni 11.42 kutoka
kwa taasisi na wadau mbalimbali mkoani Dodoma zikiwa ni kwa ajili ya
kusaidia waathirika wa tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10,
2016 na kusababisha vifo vya watu 17.
Michango
aliyopokea leo imetolewa na Mzee Thakar Singh na familia yake sh.
milioni 5; NSSF Dodoma (sh. milioni 1.2); Shirika la Bima ya Taifa tawi
la Dodoma (sh. milioni moja); Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (sh.
milioni moja) na Ofisi Rais TAMISEMI (sh. milioni 2). Wengine ni
TRA-Dodoma (sh. milioni moja); Dodoma FM (sh. 200,000) na Mwalimu
Mstaafu, Mama Amina Mafuru aliyetoa sh. 20,000/-.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA. JUMANNE, OKTOBA 04, 2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni