Ester Bulaya Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumfananisha Waziri Maghembe na TISHU
Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alichafua hali ya
hewa bungeni baada ya kusema kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe ni mzigo na mwepesi kama ‘tishu’ kwa sababu
hana uwezo wa kusimamia mambo mazito yaliyopo katika wizara hiyo, kama
vile migogoro ya wananchi na hifadhi za Taifa.
“Huyu waziri ni
mzigo kama alivyowahi kusema (Abdulrahman) Kinana. Mimi nasema yeye ni
mwepesi kama tishu, hawezi kuisaidia wizara hii nyeti,” alisema mbunge
huyo jana wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata
hivyo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama
alisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti juu ya mbunge huyo kutumia
maneno ya kuudhi ambao uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew
Chenge aliyemtaka Bulaya kufuta neno mwepesi kisha aendelee na hotuba
yake. Hata hivyo, Bulaya alikataa kufuta neno hilo na kusema wabunge
hawaamuliwi maneno ya kutumia.
Chenge aliendelea kumsihi mbunge
huyo kufuta neno hilo na katika mabishano hayo yaliyodumu kwa dakika
tatu, baadaye, Bulaya alikubali kuondoa neno ‘tishu’ na kuliacha neno mwepesi na kuruhusiwa kuendelea kuchangia.
“Mwenyekiti sitafuta neno mwepesi, kama neno ‘tishu’ linawakera basi naliondoa libaki mwepesi,” alisema Bulaya.
Katika
mchango wake, Bulaya alisema wananchi wanaoishi katika hifadhi zilizopo
jimboni mwake wananyanyaswa na askari wanyamapori wakati Serikali
imeshindwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuishi.
Alimtaka
waziri huyo kushughulikia kero zote zinazowakabili wananchi wa Bunda
akisema Serikali haiendeshwi kwa maneno matupu, bali vitendo na dhamira
ya dhati ya kuwahudumia wananchi.
“Tatua matatizo jimboni kwangu
ili niweze kukupima kama wewe ni mzito au mwepesi,” alisema mbunge huyo
akimwambia Profesa Maghembe.
Baada ya Bulaya kumaliza muda
wake, mbunge aliyefuatia alikuwa Abdallah Ulega wa Mkuranga (CCM) ambaye
alisema kuna haja ya wabunge kupimwa kama wamelewa getini ili kujua
akili zao.
“Kijana aliyefunzwa vizuri hawezi kumtukana mzee kama
yule (Maghembe). Kama suala ni uwaziri basi aangalie hata umri wake
kabla ya kuzungumza... Naungana na aliyesema wabunge tupimwe vilevi
kabla hatujaingia humu ndani. Unaweza kujenga hoja yako bila kutukana,
huhitaji kutukana ili waziri atekeleze madai yako,” alisema mbunge huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni