Jumatatu, 18 Julai 2016

Waumini waaswa kumtolea mungu

IBADA MAALUM(July 18,2016)
Imeelezwa kwamba kazi  ya Mungu ya kupeleka Injili  Ulimwenguni kote haitokamilika kama itaendelea kubakia mikononi mwa wazee wa makanisa na wachungaji pekee bila waumini wote wa kanisa kuhusika kikamilifu katika sula zima la uongoji roho.

Kauli hiyo imetolewa leo na mwenyekiti wa kanisa la Waadventista wa Sabato,Divisheni ya Afrika Mashariki na Kati,Mchungaji Blasius Ruguri wakati wa Ibada maalum ya kuchangia Ujenzi wa Ofisi ya kanisa katika Konfrensi ya Mara iliyofanyikia kanisa la Balili mjini Bunda.

Akifafanua Kauli Mbiu ya kanisa isemayo Total Member Involvement (TMI) inayomaanisha Ushirikiswaji mkamilifu wa mshiriki wa kanisa hilo,Mchungaji Ruguri amesema kama waumini wote wataamka na kupeleka injili,ulimwengu wote utamjua Mungu na hivyo kumpokea kama Bwana na Mwokozi wao.

Hivyo Mchungaji Ruguri ameyahimiza makanisa yote katika Divisheni hiyo kuwashirikisha kikamilifu washiriki katika makanisa yao wakiwamo vijana,watoto,wanawake na wanaume katika suala zima la Uongoaji roho hali itakayoharakisha kurudi kwa Yesu mara ya Pili.

Na katika hatua nyingine Mchungaji Ruguri amewasisitizia waumini wa kanisa kutoa kila walichonacho kwa ajili ya kutegemeza kazi ya Mungu Ulimwenguni akiwaonya kuwa iko siku hawatopata muda wa kumtolea kwani mali na fedha zao zitakuwa zimefungiwa.

Mchungaji Ruguri amejenga somo lake katika kitabu cha Luka 19:28-30 linaloelezea kisa cha Yesu kuwatuma wanafunzi wake wakafungue Mwanapunda kwani alimhitaji kumtumia yeye binafsi akisema kwa sasa Yesu anahitaji mali walizonazo kwa ajili ya kazi yake hivyo lazima wampatie.

Awali Mchungaji Ruguri aliyewasili kanisani hapo majira ya saa 2.30 asubuhi alivishwa skafu na Watafuta Njia kabla ya kukagua gwaride maalum lililoandaliwa na Path Finder kutoka makanisa ya Kanda ya Bunda kisha akaelekea ukumbini kwa ajili ya kuendesha Ibada hiyo maalum.
  


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni