Jana
tarehe 27/7/2016 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walitoa
kauli kwa Waandishi wa Habari kupitia Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa
Ndugu Freeman Mbowe (Mb).
Tamko hilo kama ilivyo kawaida ya CHADEMA
lilijaa uongo mwingi na ghiliba nyingi za kibabaishaji na kuthibitisha
ukweli kuwa kwa hakika kutokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Dr. John Pombe Magufuli wapinzani nchi hii wamekosa ajenda na
hivyo njia peke yake wanayoona inafaa ili waendelee kufanya utapeli ni
kutunga uongo, kujiaminisha katika uongo huo na kuusambaza uongo huo ili
kujaribu kupata wafuasi.
Katika
uongo na uzushi huo walioutangaza jana, CHADEMA wanasema wameamua
kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa tarehe waliyoitaja na
maandamano hayo yatafanyika chini ya operesheni waliyoiita UKUTA.
Kimsingi hoja walizozitumia kufikia uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa
upotoshaji na uongo uliokithiri.
Kwa mfano wanadai Serikali imezuia
mikutano yote ya vyama vya siasa, huku wakijua kuwa ni uongo kwani
Serikali haijazuia mikutano kwenye majimbo yao, Wabunge wako huru
kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao, na tumeona Wabunge wakifanya
shughuli zao majimboni bila shida wakiwemo hao wa vyama vya upinzani.
Lakini
vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao sio
jambo lililozuiliwa pia, ndiyo maana tumeshuhudia vyama vikifanya
mikutano yao ya kikatiba bila tabu.
Lakini
mfano mwingine wa hoja za uongo na uzushi, ni hoja eti ya Serikali hii
ya Awamu ya Tano kuwa ya kidikteta. Udikteta hasa unaosemwa na Chadema
ni upi? Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa? Ni huu wa kuwabana
wakwepa kodi? Ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje? Ni huu wa
kubana matumizi ya Serikali? Ni huu wa kufukuza wabadhirifu na wazembe
kazini? Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi mpaka
kuanzisha mahakama yao? CCM inaamini Watanzania walio wengi wanaunga
mkono hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali yake, sasa kama
kwa Chadema hatua hizi ndiyo tafsiri yake ni udikteta basi bila shaka
wao ni sehemu ya mfumo mbovu ndiyo maana wako tayari kuleta vurugu ili
wautetee.
Kwa
kuwa CHADEMA wamezoea kujenga Chama chao kwa harakati zinazohusisha
kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia, ukweli huu wa maelekezo
ya Serikali hawausemi, isipokuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha
wanafanya mambo ambayo mwisho wa siku yatasababisha vurugu, uvunjifu wa
amani na umwagaji damu.
Lakini
pengine ni muhimu Watanzania na wapenda amani nchini na duniani
wakajiuliza ni kweli kuwa lengo la hizi vurugu na maandamano haya ni la
kujenga na si kubomoa? Kwa nini kila operesheni ikifanywa na CHADEMA
huwa inaambatana na umwagikaji wa damu za Watanzania wasiokuwa na hatia?
Wakati wa Maandamano hayo inapotokea madhara ni kwa nini waathirika
huwa sio viongozi waanzilishi wa maandamano hayo wala wake au waume zao
au watoto wao au hata ndugu zao wa karibu bali huwa ni watu wengine nje
ya hao ndugu zao wa karibu? Mpaka lini damu za Watanzania wasio na hatia
zitaendelea kutumika kutafuta umaarufu wa CHADEMA na viongozi wake?
Hii
ni kwa faida ya nani hasa? Kwa nini pamoja na kuelekezwa namna bora ya
kufanya siasa wao huwa hawataki kufuata utaratibu? Hivi ni kweli kuwa
hawajui bila kufuata utaratibu jambo lolote huwa ni vurugu?
Chama
Cha Mapinduzi kinapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa ni vizuri
kutafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki au
kuruhusu watoto wetu kwenda kuwa kafara ya walafi wachache wa madaraka.
Ni vizuri tukayakumbuka matukio kwenye operesheni kama hizi yaliyopoteza
maisha ya vijana wetu na matokeo ya kila operesheni.
Pamoja
na ukweli kuwa hakuna operesheni yeyote kati ya zote zilizowahi
kufanywa na Chadema ambayo imewahi kuwasaidia Watanzania wa kawaida
zaidi ya kujenga umaarufu wa viongozi wachache wa Chadema na kuneemesha
matumbo yao na ya familia zao, operesheni zote zimepoteza maisha ya
Watanzania kadhaa wasiokuwa na hatia wala wasiofaidika kwa lolote na
operesheni hizo.
Kama
nia ni njema kwa nini hawataki kufuata Sheria na taratibu
tulizojiwekea? Demokrasia gani isiyokuwa na mipaka? Demokrasia bila
mipaka ni fujo. Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua
zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo
vyenye lengo la kuwahujumu Watanzania waliowengi walioamua kuchapa kazi
kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi.
Lakini
pia tunawashauri Watanzania, wapenda amani, utulivu na maendeleo
kupuuza wito wa vurugu na uvunjifu wa amani badala yake wajikite kwenye
kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
Maendeleo
hayaji kwa maandamano, maendeleo huja kwa kuchapa kazi kwa bidii.
Maendeleo hayaji kwa vurugu na fujo nchini, bali amani na utulivu ni
vichocheo muhimu vya maendeleo ya kweli.
Imetolewa na:-
Christopher Ole Sendeka (MNEC),
MSEMAJI WA CHAMA
28/07/2016
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni