Alhamisi, 28 Julai 2016

Wanaotengeneza Vyeti bandia vya Serikali Wapewa Mwezi Mmoja kujisalimisha

MPIGACHAPA Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, ametoa   mwezi mmoja kwa watu wanaojihusisha na utengenezaji wa vyeti bandia vya Serikali kujisalimisha kabla hawajachukuliwa hatua za  sheria.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam liliwakamata watu watatu ambao walikutwa na vyeti bandia vya kidato cha nne, vyeti vya uuguzi, stika za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), vyeti vya kuzaliwa na   vyuo vya ufundi.

Akizungumza na waandishi wa habari , Chibogoyo alisema wanakusudia kuendesha msako nchi nzima kuwabaini watu hao na kuwachukulia hatua za  sheria.

“Baada ya muda tuliotoa kuisha tutafuatilia mkoa hadi mkoa kuhakikisha tunadhibiti nyaraka bandia,” alisema Chibogoyo.

Aliwataka Watanzania kuacha kutumia vibaya bendera, nembo na wimbo wa taifa kwa sababu  ni vielelezo vya taifa.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile inayopendekezwa, zote zinaelekeza kuhusu matumizi bora ya vielelezo vya taifa kama vile bendera, nembo na wimbo wa taifa.

“Bendera iheshimiwe, hairuhusiwi kupeperusha bendera iliyotoboka, kupauka au chafu. Katika maeneo mengine unaweza kukuta bendera inapandishwa au kushushwa lakini watu wamekaa chini na wengine wanaendelea na shughuli zao,” alisema Kibogoyo.

Ccm wasema haya baada ya kauli iliyotolewa jana na chadema

Jana tarehe 27/7/2016 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), walitoa kauli kwa Waandishi wa Habari kupitia Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Ndugu Freeman Mbowe (Mb). 
 
Tamko hilo kama ilivyo kawaida ya CHADEMA lilijaa uongo mwingi na ghiliba nyingi za kibabaishaji na kuthibitisha ukweli kuwa kwa hakika kutokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dr. John Pombe Magufuli wapinzani nchi hii wamekosa ajenda na hivyo njia peke yake wanayoona inafaa ili waendelee kufanya utapeli ni kutunga uongo, kujiaminisha katika uongo huo na kuusambaza uongo huo ili kujaribu kupata wafuasi.

Katika uongo na uzushi huo walioutangaza jana, CHADEMA wanasema wameamua kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa tarehe waliyoitaja na maandamano hayo yatafanyika chini ya operesheni waliyoiita UKUTA.
 
Kimsingi hoja walizozitumia kufikia uamuzi wao bila kuzirudia zimejaa upotoshaji na uongo uliokithiri.
 
Kwa mfano wanadai Serikali imezuia mikutano yote ya vyama vya siasa, huku wakijua kuwa ni uongo kwani Serikali haijazuia mikutano kwenye majimbo yao, Wabunge wako huru kufanya shughuli zao kwenye majimbo yao, na tumeona Wabunge wakifanya shughuli zao majimboni bila shida wakiwemo hao wa vyama vya upinzani.

Lakini vyama vya siasa kufanya shughuli kwa mujibu wa katiba ya vyama vyao sio jambo lililozuiliwa pia, ndiyo maana tumeshuhudia vyama vikifanya mikutano yao ya kikatiba bila tabu.

Lakini mfano mwingine wa hoja za uongo na uzushi, ni hoja eti ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kuwa ya kidikteta. Udikteta hasa unaosemwa na Chadema ni upi? Ni huu wa kushughulikia watumishi hewa? Ni huu wa kuwabana wakwepa kodi? Ni huu wa kupunguza na kudhibiti safari za nje? Ni huu wa kubana matumizi ya Serikali? Ni huu wa kufukuza wabadhirifu na wazembe kazini? Hivi udikteta huo ni huu wa kushughulikia mafisadi mpaka kuanzisha mahakama yao? CCM inaamini Watanzania walio wengi wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli na Serikali yake, sasa kama kwa Chadema hatua hizi ndiyo tafsiri yake ni udikteta basi bila shaka wao ni sehemu ya mfumo mbovu ndiyo maana wako tayari kuleta vurugu ili wautetee.

Kwa kuwa CHADEMA wamezoea kujenga Chama chao kwa harakati zinazohusisha kumwaga damu za Watanzania wasiokuwa na hatia, ukweli huu wa maelekezo ya Serikali hawausemi, isipokuwa wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanafanya mambo ambayo mwisho wa siku yatasababisha vurugu, uvunjifu wa amani na umwagaji damu.

Lakini pengine ni muhimu Watanzania na wapenda amani nchini na duniani wakajiuliza ni kweli kuwa lengo la hizi vurugu na maandamano haya ni la kujenga na si kubomoa? Kwa nini kila operesheni ikifanywa na CHADEMA huwa inaambatana na umwagikaji wa damu za Watanzania wasiokuwa na hatia? Wakati wa Maandamano hayo inapotokea madhara ni kwa nini waathirika huwa sio viongozi waanzilishi wa maandamano hayo wala wake au waume zao au watoto wao au hata ndugu zao wa karibu bali huwa ni watu wengine nje ya hao ndugu zao wa karibu? Mpaka lini damu za Watanzania wasio na hatia zitaendelea kutumika kutafuta umaarufu wa CHADEMA na viongozi wake?

Hii ni kwa faida ya nani hasa? Kwa nini pamoja na kuelekezwa namna bora ya kufanya siasa wao huwa hawataki kufuata utaratibu? Hivi ni kweli kuwa hawajui bila kufuata utaratibu jambo lolote huwa ni vurugu?

Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa ni vizuri kutafakari na kujiuliza maswali ya msingi kabla ya kuamua kushiriki au kuruhusu watoto wetu kwenda kuwa kafara ya walafi wachache wa madaraka. Ni vizuri tukayakumbuka matukio kwenye operesheni kama hizi yaliyopoteza maisha ya vijana wetu na matokeo ya kila operesheni. 

Pamoja na ukweli kuwa hakuna operesheni yeyote kati ya zote zilizowahi kufanywa na Chadema ambayo imewahi kuwasaidia Watanzania wa kawaida zaidi ya kujenga umaarufu wa viongozi wachache wa Chadema na kuneemesha matumbo yao na ya familia zao, operesheni zote zimepoteza maisha ya Watanzania kadhaa wasiokuwa na hatia wala wasiofaidika kwa lolote na operesheni hizo.

Kama nia ni njema kwa nini hawataki kufuata Sheria na taratibu tulizojiwekea? Demokrasia gani isiyokuwa na mipaka? Demokrasia bila mipaka ni fujo. Tunaomba vyombo vinavyohusika visisite kuchukua hatua zinazostahili bila kumuonea mtu lakini bila kufumbia macho vitendo vyenye lengo la kuwahujumu Watanzania waliowengi walioamua kuchapa kazi kuitikia wito wa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya kazi.

Lakini pia tunawashauri Watanzania, wapenda amani, utulivu na maendeleo kupuuza wito wa vurugu na uvunjifu wa amani badala yake wajikite kwenye kuchapa kazi na kujitafutia maendeleo yao kwa kufanya kazi kwa bidii.

Maendeleo hayaji kwa maandamano, maendeleo huja kwa kuchapa kazi kwa bidii. Maendeleo hayaji kwa vurugu na fujo nchini, bali amani na utulivu ni vichocheo muhimu vya maendeleo ya kweli.

Imetolewa na:-
Christopher Ole Sendeka (MNEC),
MSEMAJI WA CHAMA
28/07/2016

Jumatano, 27 Julai 2016

Rais Magufuli kuhutubia mkutano wa hadhara Jumapili Wilayani Kahama

Rais John Magufuli anatarajia kufanya ziara wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako atafanya mkutano wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita. 
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu alisema jana kwamba Rais Magufuli atawasili hapa Jumamosi jioni kabla ya kufanya mkutano wa hadhara Jumapili. 
Nkulu aliwataka wananchi wa Kahama na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kumlaki kiongozi huyo katika ziara hiyo ambayo alisema: “Lengo lake ni kuwapongeza wananchi wa Kahama kwa kumpa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka jana.” 
Alisema ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni ya kwanza mkoani Shinyanga akianzia na Kahama. 
“Tujipongeze wananchi kutokana na kupata bahati ya wilaya chache zilizotembelewa na kiongozi huyu, Kahama imekuwa mojawapo,” alisema Nkulu. 
Alisema kwa kuwa Jumamosi ni siku ya usafi kitaifa, kila mmoja wilayani humo ahakikishe anaweka mazingira katika hali ya usafi na kuwaonya wafanyabiashara kuwa atakayeshindwa kufanya hivyo hataruhusiwa kufungua biashara. 
“Nitafanya ukaguzi Jumamosi kuhakikisha kila mtu anashiriki usafi. Hilo ni agizo la kitaifa kwa sasa lazima kila mmoja awajibike, nimewaagiza watendaji wote wa kata kusimamia hilo,” alisema Nkulu. 
Alisema wananchi watatangaziwa ratiba yote ya Rais Magufuli kwenye gari la matangazo ambalo litazunguka mji mzima wa Kahama kuwaeleza muda na eneo ambalo kiongozi huyo atafanyia mkutano.

Mtanzania anayeteswa na Mchina yampeleka Mwigulu hutua huko Geita

 
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewasili mkoa wa Geita kwa ziara ya kikazi, kubwa ikiwa ni kufuatia taarifa za mateso na mauaji yaliyodaiwa kufanywa na raia wa China wanaomiliki sehemu ya mgodi wa Nyamhuna uliopo Katoro, Geita dhidi ya wafanyakazi/vibarua ambao ni Watanzania.

Takribani wiki moja sasa kumekuwa na  hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania anayefanya kazi kwenye mgodi tajwa akiteswa na kufanyiwa vitendo ya kinyama na mwajili wake ambaye ni raia wa china.

Ilimlazimu Waziri mwenye dhamana na usalama wa raia na mali zao kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani  ya Nchi kufika eneo la mgodi kujiridhisha kwa taarifa zilizotapakaa na kubeba simanzi kwa Watanzania.

Mwigulu Nchemba amejiridhisha kuwa kulikuwepo na tukio hilo la Mtanzania kuteswa na mwajiri wake, kipigo kilichosababisha kupoteza fahamu na siyo kifo.

Hatua za awali Waziri Nchemba alizozifanya ni kwenda gereza la Geita mjini alikohifadhiwa kijana huyo kwa madai ya kushitakiwa na mwajiri wake kwa kosa la wizi lililosababishwa apigwe.

Katika mahojiano ya Waziri Mwigulu Nchemba na kijana huyo, Mwigulu alibaini kuwa kijana huyo aliyepo gerezani ndiye mhusika hasa wa tukio lile kwa uthibitisho wa makovu yaliyopo mwili mwake na mavazi aliyovalia wakati anateswa na akiwapo gerezani.

Katika hali hiyo, ilimlazimu, Mhe. Mwigulu kwenda mgodini akiwa ameambatana na kijana huyo kwa ajili ya kutambua waliofanya vitendo hivyo vya kinyama. 
Katika oparesheni hiyo, kijana aliyeteswa na kujeruhiwa aliwabaini Watanzania 5 ambao ni walinzi wa eneo hilo na Mchina mmoja walioshirikiana kumpiga, kumtesa na kumjeruhi.

Kufuatia utambuzi huo na maelezo ya wahusika, Nchemba akaagiza wahusika wakamatwe mara moja na akaondoka nao kwa hatua zaidi za kisheria.

Katika hali nyingine ya kusikitisha, Waziri Nchemba amebaini uwepo wa wahamiaji haramu raia wa China katika mgodi huo ambapo nyaraka za uhamiaji mkoa wa Geita zinaonesha raia 28 wenye vibali ndio waliruhusiwa kukaa kwenye mgodi huo, lakini katika operasheni ya kushitukiza aliyoifanya Mhe. Nchemba amebaini uwepo wa raia wa china zaidi ya 50 wanaoishi katika mgodi huo kinyume na sheria.

Hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa na timu yake ya uhamiaji kuhakikisha wote wasio na vibali wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.


 
 

Muuaji wa Mwangosi jela miaka 15

Leo July 27 2016 Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Iringa imetoa hukumu ya kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwanahabari wa kituo cha Television cha chanel Ten, Daud Mwangosi.

Mahakama hiyo imemuhukumu kwenda jela miaka 15 mshtakiwa wa mauaji hayo, askari wa polisi kikosi cha kutuliza ghasia ‘FFU’ Pacificius Simon.

Hukumu hiyo imekuja baada ya juzi mahakama hiyo kumkuta na hatia askari huyo ya mauaji ya bila kukusudia ya Mwangosi yaliyofanyika September 2 2012 kwenye kijiji cha Nyololo, Mufindi  wakatia CHADEMA ikifanya uzinduzi  wa matawi, huku kukiwa na katazo la mikutano au makusanyiko ya kisiasa kutokana na seriakali kuongeza muda wa sensa ya watu na makazi.

Chadema yajenga UKUTA mpya

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU ILIYOFANYIKA HOTELI YA BAHARI BEACH LEDGER PLAZA, 23-26 JULAI, 2016

1.0 UTANGULIZI
Kamati Kuu ya dharura ya Chama iliketi kuanzia tarehe 23-26 Julai, 2016 Jijini Dar Es Salaam na ilikuwa na ajenda moja mahsusi ambayo ni kujadili hali ya siasa na uchumi wa Taifa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015.

Mwenendo wa serikali hii ya CCM ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, ni dhahiri kuwa umeamua kuiweka demokrasia kizuizini na kuleta utawala wa Kidikteta katika nchi yetu.

  1. MATUKIO MAHSUSI YA UKANDAMIZAJI WA HAKI NA DEMOKRASIA
NCHINI
  1. Kupiga Marufuku Mikutano ya Vyama vya Siasa: Serikali kupitia Waziri Mkuu na hatimaye Rais na jeshi la Polisi walitangaza kwa nyakati tofauti kwamba ni marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuipa Serikali nafasi ya kufanya kazi. Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba. Aidha, katazo la mikutano ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa.
2.2 Kupiga Marufuku Urushwaji wa moja kwa moja (live coverage) wa Mijadala ya Bunge: Katazo hilo ni kinyume na Katiba ibara ya 18 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi.

2.3 Kudhibiti Wabunge wa Upinzani Bungeni: Serikali imejificha nyuma ya kiti cha Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb) ili kuwadhibiti Wabunge wa Upinzani Bungeni kwa lengo la kuwanyamazisha wasiikosoe Serikali.

Ikumbukwe kwamba Dkt. Tulia akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni mtumishi wa umma asiyepaswa kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa; lakini ghafla anaonekana akigombea nafasi ya Naibu Spika kupitia CCM. Hivyo yupo Naibu Spika ambaye ni mteule wa Rais. Swali: Anawajibika kwa nani kati ya Bunge na Rais?
 
Kuingilia Mhimili wa Mahakama: Serikali ya CCM kupitia Rais, kwa nyakati tofauti imeonekana kujaribu kuingilia uhuru wa Mahakama jambo ambalo ni hatari kwa utoaji wa haki nchini. Katika hotuba yake, wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria duniani Rais alinukuliwa akisema kwamba Mahakama iwahukumu harakaharaka watu waliokwepa kodi halafu atatumia asilimia fulani ya fedha ambazo zitakuwa zimepatikana kutokana na faini za wale walioshindwa kesi kuwapa Mahakama.
Muswada wa Sheria ya Haki ya kupata habari –Serikali imepeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Haki ya kupata habari. Sheria hii imeweka adhabu kubwa sana kwa waandishi kama vile kifungo cha miaka 15 na kisichozidi miaka 20 kwa mujibu wa kifungu cha 6(6)

Kupuuza Utawala wa Sheria: Tarehe 24 Juni, 2016 wakati wa uzinduzi wa siku ya usalama wa raia, Rais Magufuli alinukuliwa akiwaruhusu polisi kuwaua majambazi bila kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Aidha aliuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi kuwapandisha vyeo watakaowauwa majambazi. 
Serikali hii inatishia ukuaji wa uchumi
Tangu serikali ilipoingia madarakani hali ya ukuaji wa uchumi na hata uwekezaji wa mitaji imekuwa ikiporomoka kwa kasi kubwa sana nchini mwetu na hata baadhi ya wawekezaji wanaondoa mitaji yao kutokana na serikali hii kukosa mwelekeo unaoeleweka wa Kiuchumi.
 
Serikali za mitaa kunyanganywa mapato na serikali kuu.
Baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 tulifanikiwa kushinda maeneo ya Majiji ya DSM, Mbeya,Arusha na Miji mikubwa ya Iringa, Moshi,Bukoba,Babati,Tunduma na mingineyo ya maeneo ya mijini ambayo kwa kiasi kikubwa wanategemea sana kuendesha Halimashauri hizo kwa kutumia kodi ya Majengo Kodi ya Majengo inachangia kati ya 30% hadi 60% ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Miji.

2.9 Diplomasia na mahusiano ya kimataifa

Hivi karibuni serikali imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na Mabalozi (Note Verbale) kuelekeza kuwa kabla ya Mabalozi au maofisa wa Ubalozi kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha serikali kupitia Wizara ya Mambo Nje.

Utaratibu huu unaminya uhuru wa mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali kufanya kazi zao nchini na ni utaratibu ambao unakiuka utamaduni uliokuwepo awali na pia unakiuka masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu mahusiano ya Kibalozi Duniani.

2.10 Uteuzi wa Wakurugenzi wa Halimashauri

Uteuzi wa Rais wa Wakurugenzi wa Halimashauri na Makatibu Tawala wa Wilaya haukuzingatia sheria za utumishi wa umma na badala yake umezingatia kigezo cha Ukada zaidi badala ya weledi na historia katika utumishi wa umma kama ambavyo sheria zinataka, zaidi ya wakurugenzi 80 na Makatibu tawala zaidi ya 40 waligombea kura za maoni ndani ya CCM 2015.

2.11 ZANZIBAR

Kwa sababu ya hasira ya kukataliwa kwa CCM, vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za raia huko Zanzibar ambapo kwa zaidi ya miezi miwili sasa, wamekuwa wakipita katika vijiji na kuwapiga, kuwatesa, kuwakamata, kuwatishia na hata kuharibu mali za wananchi na mifugo yao

Tunawataka wananchi wa Unguja na Pemba waendelee kuikataa Serikali haramu iliyopo madarakani huko Zanzibar kwa njia za amani .

3.0 MAAZIMIO YA KAMATI KUU

Baada ya majadiliano Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo;
Septemba 1, siku ya mikutano ya hadhara nchi nzima
Kamati kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, Kata, Majimbo, Wilaya, Mikoa, Kanda, Mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba na imeelekeza ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa, hali ya uchumi na maandalizi ya mikutano ya hadhara ya tarehe 01 Septemba, 2016 nchi nzima.
 
Wanasheria wa Chama kuchukua hatua
Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria.
 
OPERESHENI UKUTA
UMOJA WA KUPAMBANA NA UDIKTETA TANZANIA (UKUTA)

UTANGULIZI

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika utangulizi kuna maneno yameandikwa na ambayo yamekaziwa na sheria namba 15 ya mwaka 1984 ibara ya 3 na sheria namba 1 ya mwaka 2005 ibara ya 3. Katika utangulizi huo wa katiba yetu imeandikwa kama ifuatayavyo;

“KWA KUWA Sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani” “NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia, ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi na pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu:”

“KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kwa niaba ya Wananchi kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya Demokrasia ujamaa na isiyokuwa na Dini”

Aidha kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana ibara ya 3 (1) inasema kuwa “Jamhuri ya Muungano ni Nchi ya Kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”

Ni wazi sasa kuwa kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa Demokrasia hapa Nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano kukandamiza Demokrasia na madhara ya kukandamizwa kwa demokrasia yameshaanza kulitafuna taifa letu.

Ni dhahiri kuwa kama raia wema tuna wajibu na haki ya kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi na kuhakikisha kuwa haivunji na yeyote na misingi ya Kidemokrasia ambayo ilijengwa kwa miongo mingi inaendelea kuimarika, kulelewa na kukuzwa mara dufu.

3. 4 KWANINI UKUTA NI MUHIMU !

Wakati wa Ufashisti wa Adolf Hitler huko Ujerumani unaanza kuchipua kabla ya kukomaa alianza kuchukua hatua mbalimbali za kuwanyamazisha Wajerumani kwa njia mbalimbali ili aweze kutawala kwa mkono wa Chuma.

Alikuwepo Mchungaji mmoja anayejulikana kwa jina la Martin Niemoller na ambaye alikuwa akimsemea Hitler kwa kila hatua ambazo alikuwa anachukua dhidi ya makundi mengine katika jamii ya wajerumani bila kujua kuwa lilikuwa ni suala la muda tu kabla hata yeye hajafikiwa na mkono wa Chuma wa Hitler.

Mchungaji huyu ni maarufu sana kwa msemo wake ambao aliutoa alipofikiwa na mkono wa Hitler ambao ulimpelekea kuishia jela kwa miaka 7 na wakati huo hapakuwa na

mtetezi wa kumsemea, alisema hivi;

First they came for the Socialists, and I did not speak out— Because I was not a Socialist. Then they came for the Trade Unionists, and I did not speak out— Because I was not a Trade Unionist. Then they came for the Jews, and I did not
speak out— Because I was not a Jew. Then they came for me—and there was no one left to speak for me.

3.5 HALI TANZANIA IKOJE?

Tangu utawala wa awamu ya Tano ulipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015 umechukua hatua mbalimbali za kubinya Demokrasia na kuua dhana ya utawala bora kwa njia mbalimbali.

Yapo makundi ya kijamii ambayo tayari yameshaumizwa au kubinywa na watanzania walio wengi wanakaa kimya kwa sababu wao sio sehemu ya kundi husika ambalo limenyimwa haki au kwa kuwa hajafikiwa moja kwa moja.
  1. 3.6 KWANINI NI MUHIMU KUJENGA UKUTA.
  • Rais alipiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma- sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mtumishi wa umma
  • Rais aliitaka mahakama kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi na serikali lazima ishinde-sikusema kwa kuwa sikuwa mfanyabiashara na wala sikuwa na kesi ya kodi
  • Serikali iliingilia Bunge na kupanga kamati za kudumu za Bunge-sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mjumbe
  • Serikali ilizuia matangazo ya Bunge live-sikusema kwa kuwa mimi sio Mbunge
  • Wabunge wa Upinzani kunyanyaswa Bungeni na kuonewa –sikusema kwa kuwa mimi sio UKAWA
  • Hotuba za Upinzani kufutwa Bungeni kinyume cha Kanuni za Bunge –sikuwa mpinzani nilikaa kimya Bunge kurejesha fedha zake kwa Rais kinyume cha sheria –sikusema kwa kuwa halinihusu
  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi kurejesha fedha kwa Rais kinyume cha sheria – sikusema kwa kuwa Tume hainihusu
  • Serikali Kuwafukuza na kuwadhalilisha wanafunzi wa UDOM –sikusema kwa kuwa sina ndugu wala mtoto anayesoma UDOM.
  • Mikutano ya kisiasa kupigwa Marufuku –sikusema kwa kuwa mimi sio mwanasiasa
  • Wafanyabiashara kupelekewa bili kubwa za kodi na hata kuzuiliwa kwa Akaunti zao-sikusema kwa kuwa mimi sio mfanyabiashara
  • Uchumi unaporomoka kwenye sekta zote nchini -sikusema kwa kuwa mimi sijawahi kumiliki uchumi
  • Fao la kujitoa limeondolewa kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii, sikusema kwa sababu mimi si mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
  • Mashirika na Makampuni kuanza kupunguza wafanyakazi kutokana na kuporomoka kwa uchumi –sikusema kwa kuwa sijapunguzwa kazini
  • Mabalozi na wanadiplomasia kuzuiliwa kukutana na viongozi wa kisiasa bila kibali cha serikali- sikusema kwa kuwa halinihusu
  • Watumishi wa umma kulazimishwa kwenda kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma wametakiwa kuwa Makada wa CCM –sikusema kwa kuwa mimi sio mtumishi wa umma
  • Ukaguzi wa vyeti vya kidato cha nne na kutumika kama msingi wa kufukuza watu kazi hata kama ni Maprofesa –sikusema kwa kuwa hawajaja kwenye sekta yangu
  • Watumishi wa umma kutumbuliwa majipu bila kufuatwa kwa sheria na kanuni za utumishi wa umma –sikusema kwa kuwa mimi sikutumbuliwa
  • Mawakili kuunganishwa kwenye kesi za wateja wao wanapoenda kuwatetea – sikusema kwa kuwa mimi sio wakili
  • Waalimu kukatwa mishahara iwapo dawati litavunjika kwenye shule yake – sikusema kwa kuwa mimi sio mwalimu
  • Kupotezwa kwa wana CCM ambao watapinga kauli ya Mwenyekiti au kuwa na maoni tofauti-sikusema kwa kuwa mimi sio mjumbe wa vikao vya CCM .
  • Muswada wa sheria ya haki ya kupata habari na adhabu ya kifungo cha miaka 15-20- sikusema kwa kuwa mimi sio mwandishi wa habari
  • Viongozi wa dini kudhalilishwa –sikusema kwa kuwa mimi sio kiongozi wa dini
  • Unyanyasaji na udhalilishaji wa wananchi Zanzibar –sikusema kwa kuwa mimi sio mzanzibari
3.7 TUCHUKUE HATUA!

Kwa kuwa wewe tayari umeshafikiwa hauna budi kujenga UKUTA ili kuzuia wengine wasidhurike na utawala huu.
  1. Kwa kuwa wewe hujafikiwa na ndio maana husemi wenzako wanapofikiwa, njoo tujenge UKUTA ili ukifikiwa awepo wa kusema
  2. Tuungane Tujenge UKUTA ili kuzuia uchumi wetu kuporomoka
  3. Njoo Tujenge UKUTA kuzuia Udikteta huu
  4. Tujenge UKUTA tuilinde Katiba yetu
  5. UKUTA huu ni wa wananchi wote bila kujali dini, kabila, chama cha siasa au rangi
Historia inaonyesha kuwa Duniani pote Hakuna utawala uliwahi kuushinda UKUTA wa wananchi .Na hii ndio Nguvu ya Umma. Kila mmoja achukue hatua popote alipo ya kujenga UKUTA!

Imetolewa na;

…………………….

Freeman A Mbowe

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa

27 Julai, 2016

Jumatatu, 25 Julai 2016

Vikongwe wauawa kwa tuhuma za uchawi

Vikongwe wawili mke na mumewe wa Kitongoji cha Nyag’holongo, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameuawa kwa kutumia silaha za jadi na watu wasiojulikana wakituhumiwa kuwa ni wachawi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Isack Msengi alisema tukio hilo lilitokea Julai 22 saa tatu usiku nyumbani kwao.

Aliwataja wanandoa hao kuwa ni Machene Magina (80) na Mkewe Genke Bundara (75) ambao waliuawa na wananchi wakiwatuhumu kwa uchawi.

Msengi alisema watu watano wanashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea. Diwani wa Kata ya Nanda, Jumamosi Mathias alisema kundi la watu ambalo halijulikani lilivamia nyumbani kwa familia hiyo wakati wakijiandaa kulala na kufanya ukatili huo.

Mathias alisema akiwa nyumbani kwake, alisikia kelele za watu wakisema; “Tumechoshwa na hawa wachawi. Kwa kuwa hawa wazee ni majirani zangu, nilianza kuhangaika ili kuona jinsi ya kudhibiti maafa hayo,” alisema Mathias.

 Hata hivyo, alisema kabla ya kutoa taarifa polisi, watu hao waliivamia nyumba hiyo na kufanya mauaji hayo ya kinyama kwa vikongwe hao.

Alilaani kitendo kilichofanywa na watu hao kuwa ni cha kikatili dhidi ya wazee kwani tangu aishi nao kijijini hapo hakuwahi kusikia tuhuma za uchawi dhidi yao.

Mathias alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuwahisi wazee kuwa ni wachawi na kujichukulia sheria mkononi, badala yake wawathamini na kuwalinda kwani wazee ni hazina ya Taifa.

Vijana wa mji wa Bunda wafunguka juu ya maisha yao



Vijana wa mji wa Bunda mkoani Mra  wameaswa kujituma kwa moyo mmoja  katika kufanya kazi kwa bidii kwa kipindi hiki cha awamu ya tano ili kuendelea kujenga taifa lisilo kuwa na vijana tegemezi katika ujenzi wa taifa.

Hayo yalisemwa na baadhi ya vijana wa mji wa Bunda wakati wakizungumza na wandishi wa habari  juu ya mwenendo wa maisha yasasa kwa vijana  jinsi yanavyokwenda kila kukicha.

Walisema kuwa vijana walio wengi  siku hizi wamejisahau kujituma katika shughuli mbalimbali zinazowaingizia kipato kwa siku na badala yake wamekuwa ni watu wakuwa vijiweni bila sababu za misingi.
“Siku hizi vijana tumejisahau kuwa sisi ndio wenye nguvu na ndio viongozi wa badaye” walisema vijana

Walisema licha ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kusema watu wafanyekazi kwa nguvu zote lakini bado kuna baadhi hawaoni umuhimu wa jambo hilo hali ambayo inasababisha waanze kuwa tegemezi licha ya kuwa na nguvu za kufanya kazi.

Katika hatua nyingine  vijana hao waligusia suala la mavazi yanayovaliwa na vijana kwasasa jambo ambalo limekuwa kero kwa watu licha watu kuongelea kila kukicha.
“Licha ya wazazi wetu kupiga kelele kila kukicha lakini ngoma bado iko palepale maana sie tunaona ndo muda wetu” walisema

Diwani Akwepa Risasi sita akipambana na majambazi Moshi

Diwani wa Kata ya Kiborlon (Chadema) katika Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi waliokuwa na silaha za moto.
 Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo, hazikumpata. 
Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya majambazi hao kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni. 
Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hao walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame Safaris. 
Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri. Akisimulia tukio hilo, diwani huyo alisema siku hiyo akiwa maeneo ya Kiborlon, alipigiwa simu kuwa mfanyabiashara huyo amevamiwa na majambazi ndipo alipoendesha gari lake hadi eneo la tukio. 
“Nilipofika pale wale majambazi watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka. Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika bunduki. Kuona hivyo akafyatua risasi hewani,” alisema Kagoma. 
“Yule mwenye bunduki akaingia uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola naye akawasha risasi nyingine hewani kunitisha,” alisema. 
Baada ya hali hiyo, diwani huyo alilazimika  kujificha kwenye gari na majambazi hao walidandia pikipiki na kuanza kukimbia kuelekea Barabara ya Msaranga, naye akawafuata kuelekea huko. 
“Wakati huo tayari vijana wangu wa bodaboda wakawa nao wamesikia hilo tukio tukaanza kusaidiana kuwafukuza lakini mbele kidogo pale Msaranga wale majambazi wakasimamisha pikipiki yao umbali wa mita 30 kutoka nilipokuwa na mmoja wao mwenye bunduki alifyatua risasi mbili na mwenye bastola risasi mbili kuelekea uelekeo wangu. 

“Nililazimika kujificha kwenye kiti, wale majambazi wakajua wameniua. Wakapanda tena pikipiki ili watoroke. Nikawasha tena gari huku vijana wangu nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema. 
Kagoma alisema majambazi hao walipita maeneo ambayo gari haliwezi kupita wakaelekea eneo la Mabogini Moshi Vijijini hadi lango la TPC na baadaye wakaelekea Rundugai wilayani Hai. 
“Kuna eneo vijana wangu wanasema kulikuwa na vumbi sana, ndipo walipowapoteza na majambazi wakatoroka kupitia njia ya reli ili kukwepa polisi waliokuwa wakiwasubiri mbele,” alisema na kuongeza: “Hatukuwa na silaha, lakini tulijitahidi kupambana nao kwa ujasiri. Tatizo nafikiri tulikosea kidogo. Ilitakiwa wakati tukifukuzana nao tuwape polisi uelekeo wa majambazi.” 
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa Jeshi lake litatoa taarifa rasmi kwa wanahabari leo kuhusiana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo. 
“Kuna mambo tumeyafanya tangu tukio hilo litokee lakini kesho (leo) saa sita mchana tutatoa taarifa rasmi pamoja na mafanikio tuliyofikia hadi sasa. Tunaendelea vizuri na upelelezi,” alisema.
Kamanda Mutafungwa, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ikiwamo kuwafichua wahalifu na mbinu wanazozitua akisema polisi wamejipanga kukabili wimbi jipya la ujambazi.

Alhamisi, 21 Julai 2016

Taarifa Kwa Umma Kutoka Wizara Ya Elimu



Kinana atoa Masharti Endapo Rais Magufuli Atamhitaji Aendelee Kuwa Katibu Mkuu wa CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine alikata tamaa.

Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu, lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.

CCM kuwa mbali na wananchi 
Alisema kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.

“Ninyi ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.

“Changamoto ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.

Azuiwa ziarani
Kinana alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi
 “Changamoto nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua kwenda lazima niende,alisema Kinana.

Katibu huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.

“Walichofanya wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.

Ashitakiwa kwa JK
“Baadaye Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao, ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia nimekuelewa endelea,” alibainisha.

Alisema zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.

“Nikazungumza na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina kwenda, alisema na kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.

Pia nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati, mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na hifadhi za taifa.

“Ndio maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara moja, alifafanua Kinana ambaye kuanzia mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha chama chake na kuibana serikali.

Kurejea kwake CCM
“Yalitokea mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.

Alisema amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa kung’atuka.

“Mwanasiasa mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,” alieleza.

Alisema moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama, kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.

“Uchaguzi umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana, alieleza.

Akiombwa na JPM
Alipoulizwa kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”

Waliokisaliti chama
Akizungumzia walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.

“Kwenye CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,” alisema.

Pia alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.

“Kama mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza.