Jumanne, 4 Oktoba 2016

Rais Kabila Wa Congo-DRC Aweka Jiwe La Msingi Bandarini Jijini Dar Es Salaam .......Kasema Nchi Yake Itaendelea Kutumia Bandari Yetu Kupitisha Mizigo

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange ameweka jiwe la msingi la jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambalo limejengwa kwa lengo la kuwaweka pamoja wadau wote wanaotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni juhudi za kuboresha huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji wa bandari hiyo.

Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na kati imefanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2016 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Akizungumza kabla ya kuwekwa jiwe hilo la msingi Rais Magufuli ameishukuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa mteja mkubwa wa bandari ya Dar es Salaam na amesema aliamua jiwe la msingi la jengo hilo liwekwe na Rais wa Kongo kwa kutambua umuhimu wa nchi yake katika biashara ya bandari ya Dar es Salaam na pia undugu na urafiki wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi mbili.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais Kabila kuwa kama ambavyo Serikali yake imechukua hatua kadhaa za kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika bandari hiyo, itaendelea kujenga mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa Kongo kutumia bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa, kuongeza muda wa kutunza mizigo inayoshushwa kutoka siku 14 hadi siku 30, kuanzisha bandari kavu katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuinua ari ya wafanyakazi wa bandari kutoa huduma bora.

"Mhe. Rais Kabila bandari yetu ilifikia mahali pa kuandika rekodi ya kupotea kwa meli kwenye taarifa za bandari, kuna wakati hapa zilipotea meli 60, lakini pia mizigo ya watu ilikuwa inapotea na wafanyabiashara walikuwa wanaombwa rushwa.

"Kuna baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliifanya hii bandari kama mali yao, walikuwa wanaondoka na fedha za rushwa kwenye buti za magari, naomba nikuhakikishie kuwa haya hayatatokea tena, na yakitokea Mhe. Balozi wa Kongo upo hapa njoo unieleze mimi au mwambie Makamu wa Rais au Waziri Mkuu" amesisitiza Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli pia amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania na kwamba anaamini litasaidia kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Kongo na nchi nyingine zinazotumia bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa heshimu kubwa aliyompa yeye na nchi ya Kongo ya kuweka jiwe la msingi la jengo hilo na amesema kutokana na Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za bandari ya Dar es Salaam mizigo ya Kongo itapitia bandari hiyo.

"Mhe. Rais Magufuli bandari hii ipo Dar es Salaam lakini bandari hii ni ya kwetu sote, mashariki ya Kongo inapakana na nchi nne za Tanzania, Rwanda, Burundi na Uganda lakini asilimia 50 ya mizigo inatoka Tanzania hususani katika bandari ya Dar es Salaam.

"Nimefurahi pia kuwa katika juhudi za Tanzania kuboresha bandari pia mnaboresha barabara na bandari ndogo ndogo za ziwa Tanganyika, hili ni jambo muhimu kwa sababu sasa mizigo ya Kongo itasafiri kwa urahisi na wafanyabishara wa Kongo waliokuwa wameacha kutumia bandari ya Dar es Salaam watarudi" amesema Rais Kabila.

Mhe. Joseph Kabila Kabange amesema katika miaka ya 70 na 80 Kongo ilikuwa ikizalisha shaba kiasi cha tani laki 1 lakini hivi sasa inazalisha hadi tani Milioni 1.2 na zote hizi zinategemewa kusafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kununua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na ameunga mkono mpango wa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Kongo huku akibainisha kuwa nchi yake pia itanunua ndege kwa ajili ya kuimarisha zaidi usafiri wa anga kati ya nchi hizi mbili.

Mapema kabla ya Marais wote wawili kuzungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deodatus Kakoko alisema jengo hilo lina ghorofa 35, urefu wa meta 157, ukubwa wa meta za mraba 65,115 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2016 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 130.

Rais Kabila ambaye aliingia hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa ajili yake na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

04 Oktoba, 2016

Majaliwa Alaani Mauaji Ya Watafiti Chamwino, Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelaani kitendo cha wanakijiji kuwaua watumishi wa Serikali waliokuwa wakifanya utafiti wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 3, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali.

Mauaji ya watafiti hao, Teddy Nguma, Jafari Mafuru na dereva wao Bw. Nicas Magazine yalitokea Oktoba Mosi, 2016 baada ya kushambuliwa na wakazi wa kijiji cha Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Amesema Serikali imesikitishwa na mauaji ya watu watatu wakiwemo watafiti wawili kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Seliani (SARI) kilichopo mkoani Arusha ambao walikuwa kazini kuchunguza sampuli za udongo ili kubaini kama matetemeko yataendelea kutokea.

“Kutokana na tetemeko lilitokea mkoani Kagera, Serikali iliamua kushirikisha watalaamu mbalimbali kufanya uchunguzi kuona kama tetemeko hilo ni endelevu au la katika maeneo mengine. Kitendo cha watu kujichukulia hatua mkononi na kukatisha uhai wa watumishi ambao walikuwa kazini hakikubaliki,” amesema

. Amesema watalaamu hao walifika katika Wilaya ya Chamwino na kufanya kazi kwa siku tano na siku ya sita ndipo walipoenda eneo la kijiji cha Iringa Mvumi kuendelea na kazi ambapo waliuawa wakiwa kazini.

“Serikali kupitia kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa inaendelea na uchunguzi wa kuwabaini watu waliofanya kitendo hicho’’ amesema. Hata hivyo, Waziri Mkuu amewatoa wasiwasi watumishi wanaohamia Dodoma kuwa Dodoma ni salama na kila anayekuja yupo salama. “Dodoma ipo salama na tunatarajia kila anayehamia hapa atakuwa salama na hata wakazi wa hapa wataendelea kuwa salama,’’ amesema.

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Mkuu amesema hali hiyo inajitokeza hivi sasa baada ya wananchi wengi kutambua thamani ya ardhi.

Amesema miaka ya nyuma watu wachache walitambua thamani ardhi hivyo kuchukua maeneo makubwa na kuyamiliki. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inamalizika kwa kuweka kuweka msisitizo kuwe mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kupima ardhi yote na kutoa hati kwa wananchi.

“Tunataka ardhi yote ipimwe na kila mtu anayepewa ardhi apewe hati ya kumiliki na si vinginevyo’’ amesema. 
 
Wakati huohuo, Waziri Mkuu aliwaasa waandishi wa habari wawe makini na kazi yao na wajiepushe na upotoshaji kwenye taarifa wanazozitoa kwa wananchi. Amesema vyombo vya habari ni kiungo muhimu baina ya Serikali na wananchi, hivyo aliwataka viongozi wote wa umma washirikiane na vyombo vya habari kwa kutoa habari za utekelezaji wa kazi za Serikali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea msaada wa sh. milioni 11.42 kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali mkoani Dodoma zikiwa ni kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17.

Michango aliyopokea leo imetolewa na Mzee Thakar Singh na familia yake sh. milioni 5; NSSF Dodoma (sh. milioni 1.2); Shirika la Bima ya Taifa tawi la Dodoma (sh. milioni moja); Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (sh. milioni moja) na Ofisi Rais TAMISEMI (sh. milioni 2). Wengine ni TRA-Dodoma (sh. milioni moja); Dodoma FM (sh. 200,000) na Mwalimu Mstaafu, Mama Amina Mafuru aliyetoa sh. 20,000/-.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA. JUMANNE, OKTOBA 04, 2016

Jumatatu, 3 Oktoba 2016

Benki Ya NMB Yadhamini Timu Ya Mashua Kwenye Mashindano Ya Mashua Afrika

Kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa vijana nchini, benki ya NMB imedhamini vijana watano kutoka nchini kwa ajili ya kwenda kushiriki mashindano ya mashua ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika Luanda, Angola kuanzia Oktoba 6 - 13, mwaka huu.Akizungumzia udhamini huo wa Milioni 10 na jezi kwa vijana hao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa NMB nchini, Ineke Bussemaker amesema NMB kama benki ya kitanzania inawathamini watanzania wote na inajivunia kuwa sehemu ya makampuni ambao yameidhamini timu hiyo ili ikaiwakilishe nchi katika mashindano ya mashua.
“NMB ni benki ambayo inaongoza Tanzania na ipo kwa ajili ya watanzania, moja ya sehemu ambayo tunaihudumia ni vijana, tunadhamini michezo mingi na tunaamini ni sehemu nzuri kwa vijana wadogo maana wanatakiwa kuandaliwa mapema,

“Mchezo wa mashua una wachezaji wengi, NMB inajivunia kuwa sehemu ya wadhamini kwa vijana hawa ambao watawakilishi nchi, na tunaamini watarudi kutoka Angola wakiwa na medali,” alisema Ineke.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Chama Mashua Tanzania (TSA), Philimon Nassari aliishukuru NMB kwa msaada ambao imewapatia na kuelezea changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiukabili mchezo huo kutokana na kutokuwa na wadhamini wanaowasimamia na kuwaomba NMB kuendeleza udhamini huo kwa kipindi kirefu zaidi.
 
 
“Chama chetu ndiyo kina dhamana ya kuongoza mchezo wa mashua nchini, mchezo huu sio mgeni hata watu wanaovua ngalawa wanatumia mashua, mchezo wetu unadumaa kwasababu hatuna udhamini na kama mnavyojua mchezo huu unachezwa sehemu ya wazi kwahiyo hakuna anayelipa pesa, muda wote niwa kujitolea,

“Mchezo huu kwa sasa nchini unakuwa kama unashuka, tulianza kushiriki na watoto 12 lakini kwa sasa tunakwenda na watoto watano, mwanzo mgumu lakini sisi tunaongeza juhudi na tunawashukuru NMB kwa hili wamelolifanya,” alisema Nassari.

Aliyetoa taarifa za maiti kufufuka ikiwa mochwari Singida ashikiliwa na Polisi

Jeshi la polisi mkoa wa Singida, linamshikilia askari mgambo mwajiriwa hospitali ya mkoa, MG 7822 Emmanuel Daghau (42) kwa tuhuma ya kutoa taarifa za uongo juu ya maiti kufufuka ikiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa.

Imedaiwa kuwa uongo huo ulizua mtafaruku mkubwa kwa ndugu na jamaa wa merehemu Rahel Erasto (28), aliyekuwa mkazi wa Minga manispaa ya Singida.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Singida, SSP Mayala Towo, alisema tukio hilo limetokea Septemba, 30 mwaka huu, majira ya alasiri huko katika hospitali ya mkoa mjini hapa.

Akifafanua, kaimu kamanda huyo alisema kuwa Septemba, 29 mwaka huu Rahel (marehemu) alifikishwa katika hospitali hiyo ya mkoa, kwa ajili ya kupata huduma za kujifungua salama.

“Kutokana na sababu za kitabibu Rahel, alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo ililazimika kufanyiwa upasuaji ambapo mtoto wa kiume alitolewa akiwa hai, Lakini mama kwa bahati mbaya alifariki dunia usiku saa saba Septemba, 30. Mimba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa marehemu Rahel,” alisema kaimu kamanda huyo.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa baada ya Rahel kufariki dunia, mwili wake ulipelekwa mochwari ambapo kesho yake, ndugu walijikusanya eneo hilo wakijadiliana namna kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuzika.

Alisema kuwa wakati ndugu wakiendelea kuzungumzia masuala ya mazishi, alijitokeza mlinzi Daghau na kuwaeleza kuwa ndugu yao huyo, alifariki kutokana na uzembe na kwamba usiku akiwa kwenye doria za kawaida, alisikia marehemu akipiga chafya na aliposogelea dirishani, alimwona akiwa amefufuka.

Towo alisema kuwa awali mgambo huyo baada ya kuhojiwa na Polisi, alikiri kumwona marehemu huyo akiwa amefufuka na alisikia akipiga chafya. Alikiri kwa maandishi na kuweka saini yake.

Alisema lakini baada ya Emmanuel kubaini kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu na watoa huduma za afya hospitali ya mkoa kudai kuwa Rahel amefariki dunia kutokana na matatizo ya kawaida ya uzazi na wala hakufa na kufufuka, alipohojiwa mara ya pili, alikana maelezo yake ya awali aliyotoa kwa Polisi.

Wifi wa marehemu Rahel, Mary Mpaki, alikiri kuwa alimsikia mlinzi Emmanuel wakati akiwatangazia waombolezaji kuwa marehemu amefariki dunia kutoka na uzembe wa madaktari, na kwamba alipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti akiwa hai.

“Kama ndugu wa marehemu ambao baada ya kufanyiwa upasuaji kuna ndugu ambao walitaka kulala wodini lakini hawakuruhusiwa.Tuliposikia maneno ya mlinzi huyo, tuliamini kwa asilimia mia moja maneno yake kwamba Rahel alipelekwa mochwari akiwa bado yu hai,” alisema kwa masikitiko.

Mary alisema baada ya taarifa ya mlinzi huyo, walienda moja kwa moja kituo cha Polisi kutoa taarifa hizo za kusikitisha.

Ndugu wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema taarifa iliyotolewa na mlinzi kuwa Rahel alifufuka na kupiga chafya, zitakuwa ni za ukweli kwa sababu Ni mtu mwenye akili, hawezi kudanganya jambo hilo.

“Tunasikia kwamba mlinzi kala matapishi yake kwa kitendo cha kukanusha taarifa alizotoa awali kituo cha Polisi. Kama amefanya hivyo, itakuwa kuna shinikizo amepata hivyo anatafuta njia ya kujiokoa,” alisema.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa, Dk.Ramadhani Kabala, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kudai kwa sasa mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi, ili kutambua kama kweli Rahel alifufuka na kupiga chafya akiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti.

“Ingawa si rahisi binadamu kufufuka baada ya kufariki dunia, lakini hatuwezi kuzipuuza taarifa hizi za mlinzi. Ipo timu inaongozwa na daktari bingwa kutoka wiraza ya mambo ya ndani, Dk.Ahmed Makata inaendelea na uchunguzi wa kina. Kwa hiyo baada ya kumalizika kwa uchunguzi, tutawaita waandishi wa habari kuwaeleza ukweli ili muweze kuitaarifu jamii,” alisema Dk.Kabala.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, alikiri kupokea taarifa hiyo ya aina yake, na kwamba zipo timu mbili zinaendelea na kuchunguzi ili ukweli uweze kubainika.

Rais wa DRC Joseph Kabila awasili nchini Kwa Ziara ya Siku Tatu

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Mhe. Joseph Kabila Kabange, amewasili hapa nchini jana tarehe 03 Oktoba, 2016 kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Pamoja na Rais Magufuli viongozi wengine waliompokea Rais Joseph Kabila Kabange ni Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi mbalimbali wa Serikali, Mabalozi na wananchi.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Joseph Kabila Kabange alipokea heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.

Leo tarehe 04 Oktoba, 2016 Rais Joseph Kabila Kabange atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli, ataweka jiwe la msingi la jengo la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na baadaye kushiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli Amkabidhi Vifaa Vya Ujenzi Mjane Mkoani Kagera.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemchangia vifaa vya ujenzi Mjane Agripina Angelo Mkazi wa Kitoma Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

Akimkabidi vifaa hivyo kwa niaba ya Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali (Mst) Salum Kijuu alisema kuwa Rais Dkt. Magufuli amefanya hivyo baada ya kuona kupitia vyombo vya habari jitihada za Mjane huyo kuanza kuijenga nyumba yake upya kutokana na kuharibika baada ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani humo mapema mwezi septemba.

Aidha Mkuu wa Mkoa Kijuu alitoa wito kwa wananchi ambao hawajaanza juhudi za kurejesha makazi yao waige mfano wa mjane huyo kwa kuanza ujenzi wa nyumba zao.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo Bi. Agripina alisema kuwa anamshukuru Rais kwa mchango huo kwani vifaa hivyo vitamsaidia kukamilisha ujenzi wa nyumba yake na hatimaye kupata mahali pa kuishi yeye na familia yake baada ya nyumba yake ya awali kuharibiwa na tetemeko la ardhi.

Vifaa alivyokabidhiwa mjane huyo ni pamoja na Mbao pisi 30, Mabati 35 ya futi kumi ,Saruji mifuko 25 ,Misumari ya mabati kilo 4, Misumari ya kenchi kg 7 na waya za kufungia makenchi kilo 3.

Profesa Lipumba Apata Pigo........Baraza la Wadhamini CUF Lagoma Kumtambua, Lapanga Kufunga Jengo la Chama

TAMKO LA BODI YA WADHAMINI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KUFUATIA KIKAO CHAKE KILICHOFANYIKA JANA, TAREHE 2 OKTOBA, 2016

Kwa kuzingatia hali iliojitokeza katika chama chetu cha THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kufuatia hatua ya makusudi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kutupandikizia vurugu na fujo kwa kujipa mamlaka asiyokuwa nayo ya kutuamulia nani awe Mwenyekiti wa Chama, hatua ambayo imesababisha mtu anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake tarehe 24 Septemba, 2016 kuvamia na kuhodhi jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliyopo Buguruni, Dar es Salaam, Bodi ya Wadhamini ya Chama iliona kuna haja ya kukutana na kuchukua hatua za kukabiliana na matukio hayo.

Bodi ya Wadhamini ya The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) imefanya kikao chake, tarehe 2 Oktoba, 2016 katika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Abdallah Said Khatau.

Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258 ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Political Parties Act, Cap 258) na Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014).

Ni vyema ieleweke kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kinapaswa kuunda Bodi ya Wadhamini ambayo ndiyo inayokuwa mmiliki na msimamizi wa mali zote za chama cha siasa husika. Kifungu cha 21 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinalieleza hilo kama ifuatavyo:

“21. —(1) Every political party which has obtained a certificate of full registration shall appoint a board of trustees to manage the properties and any business or investment of the party.

(2) Every board of trustees shall be duly incorporated under the Trustees Incorporation Act and every party shall, not later than sixty days from the date of full registration, submit to the Registrar—
a) the names and addresses of the members of ther board of trustees; and
b) a copy of the certificate of incorporation.”

CUF kilitimiza masharti hayo ya kisheria kwa kuunda Bodi ya Wadhamini, na Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014), Ibara ya 98 ikafafanua zaidi namna inavyopatikana, pamoja na nguvu na uwezo wake kichama, kama ifuatavyo:

“98._ (1) Kutakuwa na Bodi ya Wadhamini ya Chama itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda wake kumalizika.

(2) Bodi itakuwa na wajumbe wasiozidi tisa (9), watano (5) kutoka Bara angalau wawili (2) wakiwa ni wanawake na wanne (4) kutoka Zanzibar angalau mmoja (1) akiwa ni mwanamke ambao watateuliwa kwa masharti yanayohitajika ya Sheria ya Bodi ya Wadhamini na utaratibu uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

(3) Bodi ya Wadhamini itakuwa ndiyo mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama pamoja na madeni na itafanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na sheria ya nchi inayohusu Wadhamini.

(4) Bodi inaweza kushitaki au kushitakiwa kwa niaba ya Chama.

(5) Bodi itawajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama ambalo linaweza kuweka utaratibu unaofaa wa kuendesha shughuli za Bodi hiyo, na itafanya vikao vyake angalau mara mbili kwa mwaka.

(6) Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini watachaguliwa na Wajumbe wa Bodi kutoka miongoni mwao, kwa sharti kwamba Mwenyekiti akitoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Naibu Mwenyekiti atatoka upande mwengine wa Jamhuri ya Muungano.”

MAAMUZI YA BODI YA WADHAMINI:
Kufuatana na uwezo wake uliotajwa hapo juu na kwa kuzingatia nafasi yake kama mdhamini pekee wa fedha na mali za Chama (rejea Ibara ya 98(3) iliyotajwa hapo juu, Bodi ya Wadhamini imefikia maamuzi yafuatayo:

1. Imepuuza wito wa mtu anayeitwa Ibrahim Haruna Lipumba alioutangaza jana kwamba eti amemtaka mtu mwengine anayeitwa Thomas Malima kuitisha kikao cha Bodi ya Wadhamini. Lipumba kwa sasa si Mwenyekiti tena wa CUF na pia si mwanachama wa CUF baada ya kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

2. Itaendelea kuwajibika kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama kama inavyotakiwa na Ibara ya 98(5) ambalo ndilo linaloiteua Bodi na litaheshimu maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa likiwa ndiyo chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa Chama.

3. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(3) na 98(4) kurejesha chini ya dhamana yake mali zote za Chama zilizovamiwa, kuporwa na kuhodhiwa na Ibrahim Lipumba na genge lake ikiwemo jengo la Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam.

4. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) dhidi ya Ibrahim Lipumba kumtaka alipe gharama na hasara zote alizozisababisha kwa kuvamia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama, tarehe 21 Agosti, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza na genge lake kufanya vurugu, ghasia na uharibifu wa mali za hoteli na hatimaye kuvuruga Mkutano Mkuu jambo lililosababisha hasara ya takriban Sh. 600 milioni; na kisha kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 ambapo alisababisha hasara ya takriban Sh. 50 milioni.

5. Itachukua hatua za kisheria chini ya uwezo wake iliopewa na Ibara ya 98(4) kwa kumshtaki Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuingilia maamuzi halali ya vikao halali vya Chama na kulazimisha kukichagulia Chama chetu Mwenyekiti kinyume na onyo lililowahi kutolewa na Mahakama Kuu dhidi ya Ofisi yake kutokuwa na mamlaka ya aina hiyo.

6. Inawahakikishia wanachama wote wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar kwamba Bodi yao ya Wadhamini iko makini na itasimama pamoja nao kulinda mali zote za Chama.

7. Inaionya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwache kuingilia mambo ya ndani ya uongozi na uendeshaji wa Chama cha CUF.

HAKI SAWA KWA WOTE

Abdallah Said Khatau
MWENYEKITI WA BODI

Joran Lwehabura Bashange
KATIBU WA BODI