Machi 30,2017 redio Mazingira fm iliyopo Mjini Bunda Mkoani Mara kupitia kipindi pendwa cha Duru za habari (DZH) kinachoendeshwa na #Thomas J Masalu na Andrew Mbwiga kuanzia saa kumi kamili jioni hadi saa kumi na mbili jioni katika kipengele cha kubwa la leo walikusogezea habari kuhusu Shule ya sekondari Imesela kuvamiwa na mapepo na kuwafanya wanafunzi kuanguka na kutamka maneno yasiyoeleweka!!.
Hali hiyo ilimlazimisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kufika shuleni hapo na kujionea hali halisi na kutangaza ufanyike mkutano siku ya Ijumaa Machi 31 kwa ajili kutafutaufumbuzi wa tatizo hilo.
Sasa jana Machi 31,2017,Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Shinyanga wamefanya maombi maalum kuwaombea wanafunzi waliopatwa na mapepo na kusababisha kuanguka na kupiga kelele wakitamka maneno yasiyoeleweka katika shule ya sekondari Imesela iliyopo wilaya ya Shinyanga.
Viongozi hao wa dini walifika shuleni hapo wakiongozana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Josephine Matiro.
Viongozi hao wa dini mara baada ya kufika katika shule hiyo walishuhudia wanafunzi wakianguka,kugaragara huku wakitamka maneno ya ajabu ajabu ambapo chanzo chetu cha habari kimeshuhudia viongozi hao wakiwafanyia maombi wanafunzi hao na kurudi katika hali zao za kawaida.
Viongozi hao wa dini pia walifanya maombi madarasani,vyoo vya wanafunzi na kwenye baadhi ya miti iliyopo katika shule hiyo ambapo baadhi inadaiwa kuwa pale inapoguswa watu hupigwa shoti kama ya umeme.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa maombi hayo mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Shinyanga Elias Madoshi alisema wamefika hapo kuvunja nguvu za shetani ambazo zinawafanya wanafunzi wakose masomo yao na kwamba jambo hilo ni la aibu na fedheha kubwa katika nchi.
“Sisi viongozi watumishi wa mungu tuliopewa mamlaka na mungu kabla hatujaja hapa tumeoneshwa na mungu tumeshamjua mhusika wa mchezo huu wa kijinga,tunamuonya na tunamtaka aache kuanzia sasa,kama hataacha mtamzika hapa kijijini,tunamtaka asirudie mungu hachezewi”,alisema mchungaji Madoshi.
Naye Askofu Josephat Mussa wa kanisa la Tanzania Mision Revival Church (TMRC) alisema viongozi wa dini kamwe hawawezi kukaa kimya na kufurahia vitendo hivyo vya kishirikina na kwamba viongozi wa dini watafanya kambi katika kata ya Imesela ili watu wamjue mungu.
Naye Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu Wahmadyiya mkoa wa Shinyanga sheikh Shaban Luseza alisema asilimia kubwa na wananchi mkoani Shinyanga hawamjui mungu hivyo kuwataka kumwamini mungu.
Sheikh Luseza alishauri wananchi kumwamini mungu kwani kama huna ulinzi wa mwenyezi huna lazima vitendo vya mashetani,mizimu lazima vikupate.
“Lazima mmrudie mungu,asilimia 60 mpaka 70 ya watu Shinyanga hawafuati dini ndiyo maana matatizo haya yanajitokeza,ukiamua kumwelekea mungu naye atakuelekea na kukupa ulinzi”,aliongeza sheikh Luseza.
Kwa upande wake Sheikh Masoud Ramadhan alieleza kukerwa na vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa wanafunzi hao na kuongeza kuwa kviongozi wa dini wamekubaliana kushirikiana ili kumaliza tatizo linalowakumba wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela.
Awali kabla ya kufanya maombi hayo maalumu mkuu wa wilaya alifanya mkutano na wananchi wa kata ya Imesela na kata jirani kujadili namna ya kumaliza tatizo hilo ambapo kwa pamoja walikubaliana viongozi wa dini wafanye maombi badala ya kutumia njia za kienyeji (waganga) kumaliza tatizo hilo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo la wanafunzi kufanyiwa vitendo vya kishirikina linawaathiri wanafunzi na kusababisha kutohudhuria vipindi darasani kwa kukumbwa na mapepo hayo.
Aidha Matiro aliwataka wananchi kumwamini mungu kwa kila jambo badala ya kuamini katika matambiko kwani hakuna nguvu inayoweza kumshinda mwenyezi mungu.
Kufuatia maombi hayo wanafunzi wa shule hiyo walieleza kufarijika na hatua ya uongozi wa wilaya kufika na viongozi wa dini kufanya maombi hali ambayo inawapa matumaini ya kuendelea na masomo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela yenye jumla ya wanafunzi 252 iliyoanzishwa mwaka 2006 wamekumbwa na mapepo yanayowaangusha na kujikuta wakitamka maneno yasiyoeleweka huku wakitaja majina ya wahusika wanaowafanyia ushirikina.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la shule hilo tatizo hilo limeanza mwezi Novemba mwaka 2016 na hali ilianza kuwashtua mwezi Januari mwaka 2017 na hali ilikuwa mbaya zaidi mwezi Machi mwaka huu ambapo wanafunzi 16 walipatwa na ugonjwa huo usiofahamika na hali imeendelea hivyo kila wanapofika tu shuleni saa moja na nusu asubuhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni