Alhamisi, 23 Juni 2016

Kata ya nyamuswa wilaya ya Bunda kufaidika na mradi wa Maji hivi karibuni



Wananchi wa kata ya Nyamuswa wilaya ya Bunda mkoani Mara  hivi karibu wataanza kunufaika na mradi wa maji safi na salama baada ya kuingia ubia na shirika la Bomba ambalo limeletwa na S N V  ili kuwapatia huduma hiyo kutokana wananchi kuwa na vyanzo vya maji bila ya kuwa na fedha za kuwezesha mradi huo.

Akizungumza mara baada ya mafunzo ya kujengea uwezo kamati ya maji ya kata ya Nyamuswa Diwani wa kata hiyo FYEKA SUMELA alisema shirika la Bomba limekubali kuingia ubia na wao ili kuweza kuwasaidia wananchi wa kata hiyo  katika suala hilo muhimu ambalo limedumu kwa muda mrefu.

< shirika la Bomba limekubali kuingia ubia na sisi ili kuweza kutusaidia kata yetu  katika suala hili muhimu>

Lakini pia Diwani huyo alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi wa kata yake kuwa mradi huo utakuwa mradi  wenye ntija usiokuwa wa ubabaishaji na kwamba watazingatia kutoa huduma ya maji safi na salama kwa watu wa hali ya chini ili wapate maji.
<ni wahakikishie tu wananchi wa nyamuswa kuwa mradi ni mzuri kabisa naamini watafaidika>
Naye mwenyekiti wa kamati ya maji ya kata hiyo Tanganyika Zonzo alisema wananchi watafurahi endapo kamati itafanya kazi yake ya kupeleka majumuisho ya mafunzo ya kuwajengea uwezo na kwamba wataendelea kuiamini kamati kuwa imeanza kufanya kazi.
<wananchi siku zote hufurahia pale wanapopewa mrejesho>

 Awali muwezeshaji wa mafunzo hayo Sevelini Alute alisema wapo kwajili ya kuwajengea uwezo kamati ya maji ya kata hiyo ili waweze kuelewa sera na kanuni za maji.

Rais Magufuli Awaonya Wanasiasa Wanaomchelewesha Kufanya Kazi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amewaonya wanasiasa wanaomchelewesha kufanya kazi ya kuwatumikia Watanzania.

Rais Magufuli ameyasema hayo muda mfupi uliopita baada ya kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 
Amesema haiwezekani uchaguzi umepita na mshindi amepatikana lakini wanasiasa hao wanaendeleza siasa ilhali wananchi wanataka watumikiwe wapate maendeleo.

Rais amesema hatawavumilia viongozi wa siasa wenye lengo baya na nchi na kuwataka waweke maslahi ya Taifa mbele badala ya vyama vyao. 
Amewataka kufanya siasa baada ya miaka mitano ambapo wananchi watawapima kile walichokifanya kwa muda wote huo.

Awali Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema suala la Kura ya Maoni halikusitishwa kama baadhi ya watu wanavyosema bali iliahirishwa kwa kuwa wakati kura hiyo ilipotakiwa kupigwa Aprili Mwaka jana, Tume ilikuwa na jukumu kubwa la kuandaa uchaguzi Mkuu.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Lubuva alisema Tume haikuwa na uwezo wa kubeba mambo mawili makubwa kwa wakati mmoja. Jaji Lubuva amesema kutokana na zoezi la Uchaguzi Mkuu kumalizika rasmi, Tume iko tayari kuanza mchakato wa kura ya maoni.

Kuhusu suala hilo la Kura ya Maoni, Rais Dk Magufuli amemhakikishia Jaji Lubuva kuwa serikali italiamualia mara baada ya Tume kulifikisha serikalni.

Zitto Kabwe Amjibu Rais Magufuli


Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini

Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko makubwa kauli ya Rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa isipokuwa wakati wa Kampeni na kupitia bungeni. 
Kimsingi kauli ya Rais ni kauli yenye nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa vyama vingi na kuhimiza vyaMA vya siasa kufanya shughuli za siasa katika msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.

Tunaichukulia kauli ya Rais kama tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini.
 
Chama chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia nchini mwetu.

Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya kulinda demokrasia nchini mwetu.

Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia. Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.
Hatua zozote za kuua demokrasia ni kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi. 
Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.

Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.

Jumatano, 22 Juni 2016

Mtoto Anajisiwa na Kisha Kuuawa Kwa Kunyongwa

 
Eneo la Unga Limited, jijini Arusha
Mtoto wa miaka minne amenajisiwa na kuvunjwa shingo na kutupwa kandokando ya njia ya watembea kwa miguu karibu na mfereji wa maji umbali wa mita 50 kutoka nyumbani kwao jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Yusuf Ilembo, tukio la kunajisiwa kwa mtoto huyo wa kike lilitokea Juni 20, mwaka huu saa 3.30 usiku kwenye makaburi ya baniani Kata ya Unga Limited.

Kaimu Kamanda wa Polisi Ilembo alidai mtoto huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akicheza na wenzake nje kidogo ya nyumbani kwao na ilipofika saa 12 jioni kwa mujibu wa marafiki zake (majina yamehifadhiwa) wanasema alifika mtu mmoja mwanamume mrefu.

Kwa mujibu wa watoto hao, mwanamume huyo alikuwa amevaa suruali na kumwambia mtoto huyo amfuate akamnunulie pipi na hapo ndipo alipomfuata huyo mwanamume huyo na hakurudi tena.

Watumishi wilayani Kahama wanaopokea mishahara kubandikwa majina ili kufichua watumishi hewa.



Mkuu wa wilaya Kahama Vitta Kawawa amewaagiza maofisa watumishi katika halmashauri tatu zinazounda wilaya hiyo kubandika majina ya watumishi watakaolipwa mishahara kila mwisho wa mwezi na watumishi kuhakiki majina yao na watakapobaini majina ya watumishi ambao hawapo kazini watoe taarifa mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Tukifanya hivi tutakuwa tumepiga hatua zaidi yakutusaidia kubaini mapema wafanyakazi hewa” alisema

Mfumo huo mpya unaolenga kuendelea kubaini watumishi hewa ulitangazwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Bw.Vitta Kawawa wakati akipokea miradi ya maendeleo ya elimu kutoka katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya Acacia miradi iliyotekelezwa kwa thamani zaidi ya shilingi milioni 279.

Akikabidhi miradi hiyo ambayo ni madawati,nyumba za walimu,vyoo vya wanafunzi,pikipiki na majengo ya shule ya sekondari Bugarama yaliyokarabatiwa,Kaimu Meneja mkuu wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Bw.Benedict Busunzu,alisema kampuni ya Acacia imejikita katika kusaidia sekta ya elimu ili kuiwezesha serikali kuzalisha wataalamu,watakaoliwezesha taifa kuingia katika soko la ushindani wa ajira duniani.

“ kampuni ya Acacia imejikita katika kusaidia sekta ya elimu ili kuiwezesha serikali kuzalisha wataalamu” alisema

Baadhi ya waalimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo walidai kuwa kumekuwepo na idadi kubwa ya wafanyakazi hewa ambao nao walijitokeza kuhakikiwa ambapo zoezi la kubandika majina ya watumishi litasaidia kuwabaini.

kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa baada ya zoezi la uhakiki wa wafanyakazi katika wilaya ya kahama,inasemekana shilingi  milioni 360 ambazo zingeweza kutatua kero mbalimbali za wananchi zimetumika kulipa wafanyakazi hewa.


Ugomvi wa Wabunge wa CCM na UKAWA Wafikia Pabaya........UKAWA Wakataa Kusalimiwa, Wenye Wapenzi CCM watakiwa Kuwaacha

Sakata la wabunge wa Ukawa kususa vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson limefika pabaya baada ya baadhi ya wawakilishi hao kuanza kutowasalimia baadhi ya wabunge wa CCM.

Hatua hiyo ilikuwa dhahiri jana baada ya Ukawa kutangaza kuwa hawatashirikiana na wabunge wenzao wa chama tawala katika shughuli za kawaida za kijamii, kama vile michezo na kutumia kantini ya Bunge, wakisema wenzao wameanza kuwabagua.

Mbali na kitendo hicho, wabunge hao pia walitoka kimyakimya bungeni baada ya Dk Tulia kuingia, lakini safari hii hawakufanya mbwembwe za kujiziba midomo kama walivyofanya juzi.

Jana asubuhi, mbunge wa CCM  Kangi  Lugola alisema  kuwa alisikitishwa  baada ya kudai kuwa Mbunge wa Chadema (Viti Maalumu), Lucy Magereli hakumjibu salamu yake wakati akiingia bungeni licha ya kumsalimia mara tatu na kuwa katika umbali mfupi wa kusikika.

Kusalimia ni jambo la utamaduni wetu. Nilikuwa namsalimia mbunge wa kike wa Ukawa, lakini hakujibu. Lakini, nikajua ni sababu ya wao kufunga mdomo na plasta, nikamtania au kwa sababu ya plasta hujibu ili isije kudondoka hakuitikia,” alisema Lugola.

Alisema ameshtushwa na hali ilipofikia na hajui sababu za msingi za wabunge wa Ukawa kufanya vitendo hivyo, kinyume na udugu na utamaduni wa Watanzania.

Mbunge huyo machachari, alisema Kubenea alimziba mdomo Msigwa kwa mkono ili asizungumze chochote.

Naye mbunge wa  Sumve (CCM ) Richard Ndassa  alisema jambo wanalolifanya wabunge wa Ukawa siyo jema na halina tija kufanywa na wawakilishi hao wa wananchi.

Sisi ni wabunge, hivi inapofikia kususa kuongea na wabunge wenzako, hatima yake nini?” alisema.

Mimi nilienda kuwasalimia kama kawaida ambavyo huwa tunafanya kwa wabunge awe CUF, CCM au Chadema, sasa unavyosusa una maanisha nini,” alilalamika Ndassa.

Alisema kitendo cha kutosalimia ni cha juu sana na kwamba iwapo Ukawa wanashauriwa na mtu basi inawapasa kuchuja mambo mengine, likiwamo hilo la kuwasusa wabunge wenzao.

Juzi Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia wakati anawaongoza wabunge wa Ukawa kutoka bungeni aliwatuhumu wabunge wenzao wa CCM kuwa wanawabagua
Naye Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea   alisema;   Leo  tumekubaliana hatutashiriki katika michezo na wabunge wa CCM, hilo tumeanza leo asubuhi kwenye mazoezi katika viwanja mbalimbali, hivi sasa tunatafakari hata kutafuta uwanja wetu.

Tukikutana katika uwanja mmoja, sisi tutatumia upande mmoja na wao watatumia upande mwingine, hatuchanganyani, hata salamu leo kuna mmoja kanisalimia nimekwepesha mkono wangu,
 

Lowassa Asaidia Watoto Yatima Dar es Salaam

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewataka Watanzania kujali makundi ya watu wenye mahitaji maalumu hususan katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

 Kauli hiyo aliitoa jana alipotembelea vituo vya watoto yatima jijini Dar es Salaam vinavyoendeshwa na Waislamu kwa lengo la kuwajenga watoto kiimani. Lengo la ziara yake ni kushiriki nao katika utekelezaji wa nguzo ya mfungo wa Ramadhan.

Katika ziara hiyo, Lowassa aliyekuwa ameongozana na waumini mbalimbali wa dini hiyo, alitembelea vituo vitatu vya yatima ambavyo ni Chakuwama kilichopo Sinza, Khairat cha Kigogo na Umra kilichopo Magomeni Mwembechai.

Katika ziara hiyo, Lowassa alitoa msaada wa unga, mchele, mafuta ya kupikia, tende na sukari.

Lowassa alitoa rai kwa watu wenye uwezo kujiweka karibu na jamii inayohitaji msaada, ili kuenzi utamaduni wa Watanzania kusaidiana. 
 
 “Jamii lazima tuangalie makundi haya kwa kushiriki nao pamoja kwenye mahitaji yao, kula nao pamoja,alisema.

Mratibu wa misaada hiyo, Sheikh Rajab Katimba ambaye ni Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, alisikitishwa na baadhi ya Waislamu wanaofuturisha makundi ya watu wenye uwezo na kusahau makundi ya wasiojiweza.

Tusaidiane Waislamu na inashangaza sana kuona jamii inayohitaji msaada inasahaulika na kufuturisha wenye kujiweza kiuchumi, siyo mbaya ila tukumbuke jamii hii yenye uhitaji,” alisema Sheikh Katimba.

Mbali na salamu hizo, dua zilisomwa na watoto wawili, Fadhia Liziki (3) na Nasra Ramadhan (3) wa kituo cha Kigogo kuombea amani.