Jumatano, 5 Oktoba 2016

Uchaguzi Marekani: Pence na Kaine walumbana kuhusu Trump

Mgombea urais mwenza wa chama cha Republican nchini Marekani Mike Pence na mwenzake wa Democratic Tim Kaine wamelumbana kuhusu taarifa za kodi za Donald Trump kwenye mdahalo wa runinga.

Bw Pence, ambaye ni gavana wa Indiana, amesema mgombea urais wa chama cha Republican Bw Trump alitumia "werevu" katika kutumia sheria za kodi kukwepa kulipa kodi.

Lakini Bw Kaine, seneta wa Virginia, alipinga wazo hilo la "werevu" akishangaa iwapo ilikuwa busara kukwepa kulipa pesa za kutumiwa kulipa wanajeshi au kufadhili elimu shuleni.
Bw Trump ameshutumiwa sana kutokana na rekodi yake ya ulipaji kodi.

Amekataa kufichua taarifa zake za ulipaji kodi lakini gazeti la New York Times majuzi lilifichua kwamba huenda amekwepa kulipa kodi kwa miaka 18 iliyopita.

Tundu Lissu apaki kesi yake ashughurikia ya Bulaya

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, jana alishindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kujibu mashitaka ya uchochezi huku mdhamini wake akiieleza mahakama kuwa, yupo jijini Mwanza akisimamia kesi ya Esther Bulaya, Mbunge wa Bunda katika Mahakama Kuu ya Mwanza.

Lissu ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu na mwansheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo anashitakiwa kwa uchochezi pamoja na washitakiwa wengine ambao ni ni Jabir Idrissa, mwandishi mwandamizi wa Gazeti la MAWIO, Simon Mkina, mhariri wa Gazeti hilo na Ismail Mehboob, meneja wa kampuni ya uchapishaji magazeti ya Flint.

Mdhamini wa Lissu, Ibrahim Hemed, alitoa taarifa ya kutofika kwa mdhamana wake mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Ibrahim alidai kwamba Lissu amempatia taarifa kuwa ameshindwa kufika kwa sababu yupo kwenye kesi ya uchaguzi huku Peter Kibatala wakili wa utetezi akiiomba mahakama ipokee taarifa za Lissu na ikubali kuhairisha kesi hiyo.

“Lissu ni wakili  pekee wa mlalamikiwa Esther Bulaya katika kesi ya uchaguzi,” alisema Kibatala.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31 mwaka huu.

Katika kesi hiyo Lissu anaunganishwa kama mshitakiwa kufuatia kunukuliwa akitoa maoni yake katika habari iliyochapishwa na gazeti la MAWIO ikiwa na kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”

CUFwazidi Kunogasha.......Bodi ya Wadhamini Nayo Yagawanyika Viipandevipande

Bodi ya wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imegawanyika vipande viwili  kutokana na mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama hicho.

Kugawanyika kwa bodi hiyo kumekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wake, Abdallah Katau kutangaza kutomtambua Profesa Lipumba, huku baadhi ya wajumbe wakipinga tamko hilo wakiliita ni batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wajumbe wenzake, mjumbe wa bodi ya chama hicho, Peter Malebo, alisema hawatambui tamko lililotolewa na mwenyekiti wao kwani bodi hiyo inajiandaa kuwakutanisha mwenyeki wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad ili kuweza kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Alisema kutokana na hali hiyo, watakaa na wajumbe wenzao na kujadili suala hilo kabla ya kuwaita viongozi hao ikiwa ni pamoja na kujadili ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

“Tutakaa na wajumbe wenzetu ili tuweze kujadiliana mgogoro wa viongozi wetu pamoja na kupitia maazimio ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ili tuweze kupata hoja ya kuwahoji kwenye kikao hicho.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa chama chetu kinarudi kwenye hadhi yake kama ilivyokua awali kuliko hivi sasa ambapo kimegubikwa na mgogoro wa uongozi wa kitaifa,” alisema Malebo.

Alisema ikiwa watashindwa kupata mwafaka wataitisha Mkutano Mkuu wa dharura  ili waweze kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo hali ya chama na hatua za kuchukua.

“Kama mwafaka hautapatikana katika kikao hicho, tutalazimika kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu ambao pamoja na mambo mengine, tutawaeleza mgogoro wa viongozi wetu ili wajumbe waweze kutoa uamuzi,” alisema.

Alisema Bodi ya Wadhamini wa CUF inaundwa na wajumbe wanane ambapo kutoka upande wa bara ni watano na Zanzibar watatu.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni pamoja na Abdalah Katau, Peter Malebo, Ally Mbarouk, Amin Mrisha, Zacharia Kwangu, Yohana Mbelwa na Dk. Juma Muchi.

Alisema mpaka sasa bodi hiyo imegawanyika ambapo wajumbe kutoka Zanzibar wanamwunga mkono Maalim Seif huku wale wa bara wakimwunga mkono Profesa Lipumba hali inayozidi kupandisha joto ndani ya chama hicho.

“Kinachotutafuna  ndani ya CUF ni ubaguzi unaoonyeshwa waziwazi kutoka kwa viongozi wa Zanzibar jambo ambalo limechangia kila mtu kuwa upande wake, lakini tutaitana na kujadiliana suala hili ili tuweze kupata mwafaka,” alisema.

Alisema bodi hiyo inafanya kazi ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo iliteuliwa mwaka 2011 na itamaliza muda wake, Desemba mwaka huu.

Atoa onyo Chadema
Katika hatua nyingine, Malebo aliwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoingilia mgogoro huo kwa madai hauwahusu.

Alisema, kitendo cha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Profesa Lipumba inaonyesha wazi kuwa ameshiriki kuongeza mgogoro ndani ya chama hicho.

“Mbowe haumhusu mgogoro wa viongozi wa CUF, huu ni mgogoro wa ndani ya chama, tunamshangaa kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Lipumba, yeye ni nani ndani ya chama?, tunamuonya asirudie,” alisema.

Alisema, chama hicho kimejipanga kupambana na watu wanaoingilia mgogoro wao wakati si wanachama wa chama hicho, jambo ambalo limechangia kuendelea kuchochea vurugu hizo.

Kubenea kizimbani tena kwa kupotosha

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kuandika makala ya kupotosha na kusababisha hofu kwa jamii.

Kubenea, ambaye ni mbunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Dereck Mukabatunzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Wakili Mukabatunzi alidai kuwa Julai 25, mwaka huu katika Mtaa wa Kasaba, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Kubenea alichapisha habari ya uongo inayoweza kusababisha hofu na taharuki kwa jamii au kuondoa amani.

Inadaiwa Kubenea alichapisha makala hiyo kwenye gazeti la Mwanahalisi la Julai 25 hadi 31, mwaka huu, lenye namba 349 ISSN: 1832-5432 ikiwa na kichwa cha habari “Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar”.

Baada ya kusomewa mashitaka, Kubenea alikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali.

Jumanne, 4 Oktoba 2016

Ufaransa yatishia kuiwekea vikwazo DRC

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ,Joseph Kabila ni sharti aheshimu katiba na kujiuzulu mwishoni mwa muhula wake ,waziri wa maswala ya kigeni nchini Ufaransa Jean-Mark Ayrault amesema katika mahojiano na kituo cha habari cha TV5.

Bwana Ayrault alikuwa akisisitiza wito aliotoa wiki iliopita wakati akiwahutubia wanafunzi mjini Paris.
Wakati huu aliangazia madai kwamba Ufaransa imekuwa ikiingilia maswala ya ndani ya DRC,akisema kuwa taifa lake haliko pekee kumkumbusha Kabila kwamba lazima aheshimu sheria.

Aliambia kituo hicho: ''Rais Kabila lazima aonyeshe mfano mwema. Ni lazima aheshimu katiba. Iwapo vikwazo vitahitajika tutaamua kuvitekeleza. Nataka watu waelewe; Watu waliopo katika mamlaka DRC ni lazima wawajibike. Iwapo wanahitaji amani nchini mwao, iwapo wanajali hali ya watu wao ,ni lazima wafuate katiba''.

Lakini serikali ya DRC imesema Ufaransa inachochea maasi dhidi ya serikali nchini humo.
Waziri wa mawasiliano Lambert Mende ameambia shirika la habari la AFP kwamba Ufaransa 'inacheza mchezo hatari'.

"Baada ya kuwasha moto na kuwahimiza watu wenye misimamo mikali, Ufaransa itawaondoa raia wake na kuwaacha raia wa Congo taabani," ameambia wanahabari.
"Wasiwasi wa Waziri Ayrault kuhusu DRC unazua shaka kwa sababu unafufua kumbukumbu za uingiliaji kati ambao ulizaa vurugu Libya."

Clouds.........Yafungiwa kwa miezi 3 kipindi cha 'Take One' kwa kukiuka kanuni za utangazaji.

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kali kwa kituo cha Televisheni cha Clouds sambamba na kukifungia kwa kipindi kwa miezi mitatu kipindi cha Take One kinachorushwa na Kituo hicho.
 
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Method Mapunda amesema sababu ya kukifungia kipindi hicho ni kutokana na ukiukwaji wa kanuni za utangazaji za mwaka 2005, kwa kumhoji na kurusha kipindi cha mtu kinachohamasisha biashara ya ngono, kuingilia faragha ya mtu na kutolinda maadili ya watoto.

“Clouds tv inapaswa kukitathimini upya kipindi hicho kwa lengo la kupata njia bora ya kukiendesha na kupeleka mapendekezo TCRA kwa ajili ya kujiridhisha kabla ya kipindi hicho kufunguliwa,”alisema mapunda.
 
Mahojiano yaliyopekea kipindi hicho kufungiwa ni kati ya mtangazaji wa kipindi hicho Zamaradi Mketema na Gift Stanford Maarufu kama ‘Gigy Money’ na yalirushwa Agost 09 saa 3.00 usiku na kurudiwa kesho yake saa 7.00

Kauli ya Makamu wa Rais kufuatia mauaji ya watafiti wawili waliouawa kwa kuchomwa moto

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amelaani vikali mauaji ya watafiti wawili wa kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Arusha na dereva mmoja waliokuwa kazini katika kijiji cha Mvumi Makulu, wilayani Chamwino mkoa wa Dodoma.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo 4-Oct-2016 wakati akifungua kongamano ya 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesema kuwa tukio hilo ni baya na amewahakikishia watafiti wanaoshiriki kongamano hilo kuwa Serikali itachukua hatua stahiki kwa watu  waliofanya kitendo hicho cha kinyama ili kukomesha tabia hiyo.

“Haiwezekani hata kidogo watu kufanya mauaji hayo ya kikatili na waachwe bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria alisisitiza Makamu wa Rais”

Akizungumzia masuala ya utafiti, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na watafiti hao hivyo Serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali ili kuhakikisha watafiti hao wanafanya kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.

Makamu wa Rais pia amewahimiza wafadhili waendelee kusaidia watafiti hasa wanaofanya tafiti za afya nchini kwa sababu tafiti hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Amesema kuwa watafiti wanamchango mkubwa katika kuleta maendeleo kupitia matokeo ya tafiti zao nchini hivyo jitihada hizo ni muhimu zikaimarishwa ipasavyo.

Kongamano hilo la 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu -NIMR- linajumuisha watafiti mbalimbali kutoka Ulaya, Afrika na Amerika.

Katika kongamano hilo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika zoezi utoaji wa tuzo kwa wanasayansi waliofanya tafiti mbalimbali za afya nchini.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam.

4-Oct-2016.