Jumatano, 4 Januari 2017

Mkuu Wa Jeshi La Polisi Nchini, Igp Ernest Mangu Atuma Timu Ya Maofisa Wa Jeshi La Polisi Kwenda Zanzibar Kuchunguza Vitendo Vya Udhalilishaji



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu ametuma timu ya Maofisa  wa Polisi ikiongozwa na Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa kwenda Zanzibar kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto/wanawake ambavyo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara.

Timu hiyo imepewa jukumu la kuchunguza vitendo hivyo vya udhalilishaji na kiini chake na hatimaye kuja na mpango mkakati wa kuzuia vitendo hivyo ikiwemo kuwakamata  wahusika na kuwafikisha mahakamani.

IGP Mangu amewataka wananchi wa Zanzibar, Taasisi za kiserikali na Taasisi za kiraia zilizopo Zanzibar kutoa ushirikiano kwa timu hiyo ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya Watanzania.

Godbless Lema Arudishwa Tena Gerezani.....Ni Baada ya Serikali Kuwasilisha Notisi Ya Kupinga Dhamana yake Mahakama ya Rufaa



Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, leo imeshindwa kusikiliza rufani ya Jamhuri dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kupinga dhamana yake, baada ya mawakili wa Serikali kuwasilisha notisi ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa wakipinga kusikilizwa kwa rufani hiyo .

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Salma Maghimbi   alitarajiwa kutoa uamuzi juu ya rufaa ya Jamhuri iliyopinga  Lema kupatiwa dhamana Novemba 11 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, ambapo siku hiyo Jamhuri iliwasilisha notisi ya mdomo.

Baada ya Lema kufikishwa mahakamani saa 3.25 asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali, huku pia polisi wakiwa wametanda viwanja vya Mahakama Kuu ndani na nje sanjari na gari moja la maji ya kuwasha, baada ya  mawakili wa pande zote kujitambulisha Jaji Maghimbi alisoma notisi ya Jamhuri kupeleka shauri hilo Mahakama ya Rufaa na kueleza kufungwa kisheria kutoa uamuzi wa rufani hiyo.

Anaswa na polisi akifukua kaburi la albino



Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kufukua kaburi la marehemu ambaye likuwa ni mlemavu wa ngozi (Albino) aliyefariki mwaka 2010 kwa lengo la kuchukua viungo vyake.

Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Kamanda a Polisi Mkoani Mbeya DCP Dhahiri Kidavashari inasema kuwa mnamo tarehe 03.01.2017 majira ya saa 01:00 usiku katika Kijiji cha Mumba kilichopo Kata ya Ilembo, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JONAS JOHN mkazi wa Chapakazi alikamatwa na askari Polisi akiwa na wenzake wawili wakifukua kaburi la marehemu SISTER OSISARA aliyekuwa mlemavu wa ngozi (ALBINO)

Inadaiwa kuwa marehemu alifariki dunia mwaka 2010 kwa ugonjwa wa homa na kuzikwa katika makaburi ya Kijiji cha Mumba.

Mtuhumiwa alikutwa na majembe na makoleo ambayo walikuwa wakiyatumia kufukuria kaburi hilo. Baada ya mahojiano mtuhumwa huyo aliwataja washirika wenzake wawili ambao walikimbia baada ya kuwaona askari.

Jeshi hilo linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa .

Katika tukio lingine Mnamo tarehe 03.01.2017 majira ya saa 3:30 usiku katika kata ya Makongolosi wilayani Chunya, mkoa wa Mbeya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la KELVIN KUBANDA mkazi wa Kahama alikamatwa akiwa na bhangi kete 10 sawa na uzito wa gramu 55.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa katika kijiwe cha kuvutia Bhangi. Upelelezi unaendelea.

Jumanne, 3 Januari 2017

PIL Trade yaanzisha mafunzo kwa wafugaji kuku

Kampuni ya ufugaji na utengenezaji chakula cha kuku ya PIL Trade ya mjini DAR ES SALAAM imeanzisha shamba darasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku kwa wajasiriamali

Kampuni ya ufugaji na utengenezaji chakula cha kuku ya PIL Trade ya mjini DAR ES SALAAM imeanzisha shamba darasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku kwa wajasiriamali

 Akizungumza kwenye uzinduzi wa shamba hilo,mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Ismail Lankii amesema mafunzo hayo yatahusu utunzani wa kuku kuanzia vifaranga, uchangaji bora wa chakula na yatamwezesha mjasiriamali kuanzisha miradi ya kisasa ya ufugaji wa kuku.

Naye afisa masoko wa kampuni hiyo Sharifa Issah amewashauri  vijana kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku kwani ni njia ya uhakika ya kujipatia kipato.

TRA - ZANZIBAR yakusanya bilioni 80.17 kati ya mwezi Julai na Novemba

Mamlaka ya mapatoa nchini, TRA, ofisi ya ZANZIBAR imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 80.17 kwa kipindi cha kati ya mwezi Julai na Novemba 2016 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato visiwani humo.

Mamlaka ya mapatoa nchini ,TRA - ofisi ya ZANZIBAR imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 80.17 kwa kipindi cha kati ya mwezi Julai na Novemba 2016 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato visiwani humo.

Akizungumza mjini UNGUJA, naibu kamishna TRA Zanzibar , MCHA HASSAN MCHA amesema kiasi hicho cha mapato ni mwenendo mzuri wa makusanyo ambapo malengo ni kufikisha shilingi bilioni 188.80 utakapokamilika mwaka wa fedha wa 2016/17.

Shirika la manunuzi KARIAKOO lawatimua maafisa wake wa wili kwa manunuzi kinyume na taratibu

Shirika la masoko ya kariakoo limewasimamisha kazi maafisa wawili wa idara ya manunuzi kwa tuhuma za kufanya manunuzi kinyume cha sheria ya manunuzi.

Shirika la masoko ya Kariakoo limewasimamisha kazi maafisa wawili wa idara ya manunuzi kwa tuhuma za kufanya manunuzi kinyume cha sheria ya manunuzi.

Meneja Mkuu wa Shirika hilo HETSON KIPSI amewataja waliosimamishwa kazi ni mkuu wa kitengo cha manunuzi wa shirika hilo MATHIAS MBAFU  na msaidizi wake HENRIKA KAWILI .

KIPSI amesema maafisa hao wanatuhumiwa kughushi saini ya meneja mkuu ili waweze kununua mafuta ya jenereta na vifaa vingine na uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea.

GAMBO ataka kufuatiliwa fedha za mikopo ya wanawake na vijana


Mkuu wa mkoa wa ARUSHA, MRISHO GAMBO amemwagiza Mkuu wa wilaya ya ARUSHA kuunda timu ya kufuatilia fedha za mikopo zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya Vijana na Wanawake kwa kipindi cha miaka MITATU namna zilivyotumika.
 
Mkuu wa mkoa wa ARUSHA, MRISHO GAMBO amemwagiza Mkuu wa wilaya ya ARUSHA kuunda timu ya kufuatilia fedha za mikopo zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya Vijana na Wanawake kwa kipindi cha miaka MITATU namna zilivyotumika.

GAMBO ametoa agizo hilo jijini ARUSHA wakati akikabidhi mfano wahundi yenye thamani ya shilingi Milioni 425 kwa vikundi vya wanawake 85 na hundi ya shilingi Milioni 199 kwaajili ya vikundi 40 vya vijana wa jiji hilo,GAMBO nakusisitiza kuwa fedha hizo zinatakiwa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ya kufanya shughuli za kiujasiriamali.

 Amesema bado jiji hilo linatoa fedha kidogo ikilinganishwa na mapato yanayokusanywa na kuvinufaisha vikundi vya vijana na wanawake hivyo ni vyema mikopo iliyotolewa ikadhibitiwa ikiwa nipamoja na kufanya uchunguzi wa fedha za mikopo zilizotolewa katika kipindi cha miaka MITATU.

Kwa upande wake Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii katika jiji la ARUSHA, JANETH MMASI, amesema mikopo hiyo itasaidia vikundi 125 vya Vijana na Wanawake katika kujikwamua kiuchumi huku Mkuu wa wilaya ya ARUSHA, GABRIEL DAQQARO akiahidi kusimamia kikamilifu fedha hizo ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

Wakulima Katavi waiomba serikali kuwaruhusu kutumia miundombinu ya umwagiliaji wa kienyeji

Wakazi wa kijiji cha, ITENKA katika Halmashauri ya NSIMBO Wilayani MPANDA Mkoani KATAVI wameiomba serikali kuwaruhusu kutumia miundombinu ya umwagiliaji wa kienyeji wakati wakisubiri kuwekewa miundombinu ya kisasa katika bonde la umwagiliaji la ITENKA.

Wakazi wa kijiji cha,  ITENKA  katika Halmashauri ya NSIMBO Wilayani MPANDA Mkoani KATAVI wameiomba serikali kuwaruhusu kutumia miundombinu ya umwagiliaji wa kienyeji wakati wakisubiri kuwekewa miundombinu ya kisasa katika bonde la umwagiliaji la ITENKA.

Wakazi hao wametoa ombi  hilo wakati wa mkutano wa hadhara uliokua na lengo la kujadili shughuli za maendeleo katika jimbo la NSIMBO, mkutano ulioongozwa na Mbunge wa jimbo hilo RICHARD MBOGO.

Wakazi hao Wamesema wao wanategemea kilimo cha mpunga hivyo kubomolewa kwa miundo mbinu iliyokuwa imejengwa na kuzuia maji kutiririka katika  bonde la mto katuma kumeyafanya Maisha yao kuwa mashakani kwa kuwa hawana tegemeo jingine la uchumi tofauti na kilimo cha mpunga katika bonde hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la NSIMBO Richard Mbogo amesema atawasilisha suala hilo serikalini  ili liweze kufanyiwa kazi na kuwataka Wakazi hao kuheshimu sheria za uhifadhi wa  mazingira kwa kutii maagizo yaliyotolewa na serikali.

Majambazi yapora mamilioni mbele ya askari polisi Dar

Watu  wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea  jana saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara.

Watu hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.

Aidha taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke, Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo wa usalama barabarani.

Wakati tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari doria zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa Barabara ya Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu hao waliokuwa wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na Jeshi la Polisi.

Majambazi hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.

Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.

Kwa mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.

Charles alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.

“Kwa kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili mmoja upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola nifungue mlango niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo cha nyuma kwa kutumia kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na kutokomea” alisema Richard.

Askari wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio hilo wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo linalohatarisha usalama wao na mali zao.

“Kama walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini wasingeomba hata ‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni tatizo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.” alisema askari huyo.

Credit: Habari Leo

Mkulima afunga safari kutoka Urambo mpaka Bukoba kumuona Rais Magufuli

Mkulima wa tumbaku aliyesafiri kutoka Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Moshi Rubibi akitafuta upenyo wa kumfikishia Rais John Magufuli kilio cha wakulima, alifanikiwa kufanya hivyo mjini Bukoba  wa kutumia staili iliyomvuta Rais kumsikiliza. 
Awali, mkulima huyo anayewakilisha wenzake zaidi ya 60 alikwama kufanya hivyo wakati Rais Magufuli alipokuwa kwenye mapumziko wilayani Chato mkoani Geita baada ya kuzuiwa na walinzi lakini bila kukata tamaa alimfuata Rais mjini Bukoba baada ya kusikia anafanya ziara. 
Utaratibu wa Rais Magufuli kutaka kusalimiana na wananchi baada ya mkutano ndiyo uliofanikisha mpango wa mkulima huyo kwani aliamua kupiga kelele mfululizo kwa mbali akilitaja jina la Rais huku akipunga hewani mkono uliokuwa na bahasha ya kaki. 
Pamoja na kudhibitiwa na walinzi, sauti ya mkulima huyo ilizidi kuchomoza kwa nguvu hali iliyomfanya Rais Magufuli aliyekuwa anaondoka kwenye eneo la mkutano kupiga hatua kadhaa nyuma na kuwaambia walinzi wake wamuache amsikilize. 
Huku akitweta na kuhema kwa nguvu baada ya kuruhusiwa kumfikia Rais Magufuli, mkulima huyo alimwambia kuwa yeye ni mwenyeji wa Urambo, Tabora na amemtafuta ili kumfikishia malalamiko ya wakulima wa tumbaku wanaopigwa chenga kulipwa mafao yao. 
Alisema wakulima hao wanadai zaidi ya dola za Marekani 98,000 (zaidi ya Sh200 milioni) za mauzo ya tumbaku waliyouza kupitia Bodi ya Tumbaku tangu Septemba, 2015 na kuwa wanashawishiwa kutoa rushwa ili wapewe haki yao. 
Alimwambia Rais kuwa wameambiwa watoe dola 10,983 ili waweze kulipwa fedha zao kupitia tawi la Benki ya CRDB Urambo na kuwa kati ya kiwango wanachodai cha mauzo ya tumbaku wakubali kulipwa dola 87,017 tu. 
Mkulima huyo alisema wamefikisha suala hilo kwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo na kukosa ufumbuzi na kuwa walilipeleka pia kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, Mwigulu Nchemba ambaye alionyesha kuwa tayari kulishughulikia lakini kabla ya kufanya hivyo, alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
Baada ya kumsikiliza takribani kwa dakika nne, Rais Magufuli alimkabidhi mkulima huyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama na kuagiza apewe taarifa baada ya siku tano jinsi walivyoshughulikia suala hilo.

Mtoto Amuua Baba Yake Na Kutaka Kumfukia

Jeshi  la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Patrick Malindisa (29) mkazi wa Mtaa wa Namanyigu Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi Athanasi Malindisa (70) kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali kichwani na kidevuni na kisha kutaka kuufukia kwenye shimo alilochimba ndani ya nyumba yao.

Mmoja wa wanafamilia ambaye ni mdogo wa marehemu Pius Malindisa jana  alisema walipata taarifa ya kifo cha ndugu yao Januari Mosi mwaka huu saa 1:30 jioni  kutoka kwa mtoto wa marehemu Patrick Malindisa.

Alisema marehemu alikuwa akiishi na mtoto wake huyo ambapo baada ya kufanya mauji hayo alianza kuwaarifu ndugu kuwa amefariki kwa ugonjwa wa tumbo.

Kutokana na taarifa hizo ndugu walikusanyika nyumbani kwa marehemu ambapo baada ya kuingia ndani walikuta akiwa amelala ndipo walipowaita viongozi wa mtaa na baada ya kufunua walibaini marehemu ameuawa kwa kupinga na kitu chenye ncha kali kichwani na kidevuni.

“Baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa awali tulitoa taarifa polisi ambapo walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi. Na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma huku mtoto wake akishikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.

“Tulipofika hapa tulikuta shimo limechimbwa ndani ya nyumba na inaelekea lilimshinda na kuamua kuanza kutoa taarifa kwetu ambapo alidai alikuwa anaumwa ugonjwa wa tumbo,” alisema Pius

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo kwa sasa wanamshikilia mtoto wa marehemu, Patrick Malindisa kwa uchunguzi zaidi.