Alhamisi, 6 Oktoba 2016

Waziri Mkuu angumza haya alipotembelea wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba mkoani Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameahidi kukutana na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba mkoani Dodoma ili kuzungumzia namna ya kulikarabati na kulifanya liwe la kisasa.

Amesema miongoni mwa mambo watakayoyajadili katika kikao hicho ambacho hakutaja siku ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara hasa kwa wanaouza bidhaa nje ya maduka.
 
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatano, Oktoba 5, 2016wakati alipotembelea maduka hayo yaliyoko katika barabara ya One Way inayopita katikati ya barabara ya sita hadi ya 11 pamoja na soko la Sabasaba akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
 
Alisema Serikali tayari imeshahamia Dodoma hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kutumia fursa hiyo kwa kuboresha biashara zao ili waweze kumudu ushindani wa soko.
 
“Wafanyabiashara lazima mboreshe biashara zenu, muongeze usafi zaidi na ikiwezekana muimarishe majengo yenu yawe ya kisasa zaidi kwani haiwezekani maduka ya Makao Makuu ya Nchi yawe katika hali hii,” alisema.
 
Pia Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara hao wasiogope kwenda kukopa katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa lengo la kujiongeza mitaji na kupanua biashara.
 
Alisema tayari alishatoa maagizo kwa wamiliki wa benki kuhakikisha wanawawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapa mikopo, hivyo aliwataka wasiogope na badala yake wachangamkie fursa hiyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma matatani, majaliwa aagiza achunguzwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana kuchunguza ni kwa nini Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino Kilumbi amekwenda kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000. Uongozi wa gereza hilo ulitengeneza madawati hayo kwa watu binafsi ambapo dawa moja limegharimu sh. 70,000.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano, Oktoba 5, 2016 wakati alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii mjini hapa.

Alisema kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo amemtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati inatoka wapi na inakwenda kwa nani.

“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali,” alisisitiza.

Serikali imeandaa utaratibu wa kuwezesha taasisi zake zikiwemo za kijeshi kwa kuzipa kazi ya kutengeneza bidhaa na miundombinu mbalimbali ikiwemo madawati ili kuyaongezea tija aliongeza

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi alisema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.

Aidha, Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Kuhusu changamoto ya makazi kwa askari Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na imeweka mkakati wa wa ujenzi na kwa upande wa askari Magereza wataanzia kwa mkoa wa Dodoma.

Wakati huo huo Waziri Mkuu alitembelea maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo katika maeneo ya soko la Sabasaba na Majengo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Jumatano, 5 Oktoba 2016

Fifa kuongeza timu zitakazoshiriki kombe la dunia kufikia 48

Rais wa Fifa Gianni Infantino ameshauri kuongezwa wa timu zinazoshiriki kombe la dunia na kufikia 48 zaidi ya ahadi yake aliyoitoa wakati akiwania nafasi hiyo kuwa atafikisha timu 40.

Anashauri kuwa timu 16 kati ya zote zitatolewa katika hatua ya awali kabisa.

Kisha kubaki 32 zitakazoendelea katika makundi baada ya hatua ya mtoano kukamilika.

Infantino anasema kuwa mapendekezo hayo yatapelekwa katika bodi ya Fifa Januari.

''Haya ni mawazo ya kupata suluhisho la uhahika, tutayajadili mwezi huu na kufahamu nini cha kufanya mwaka 2017,'' alisema Infantino mwenye miaka 46.

Infantino aliingia madarakani kuliongoza shirikisho hilo la Fifa mwezi Februari baada ya kujiuzulu kwa Sepp Blatter.

ITF yatoa onyo kwa wachezaji baada ya kupunguza adhabu ya Sharapova


Chama cha Tennis duniani ITF kimempunguzia mchezaji nyota wa tennis Maria Sharapova adhabu ya kufungo cha miaka miwili na sasa itakuwa miezi 15.

Lakini kimesema kuwa wachezaji wa mchezo huo hawataruhusiwa kukata rufaa kama watahisiwa kuhusika kwa maksudi na matumizi ya dawa zilizokataliwa michezoni.

Katika taarifa yake chama hicho kimesema kuwa hakitakuwa tayari kupokea maelezo yoyote ambayo yanaonyesha kuwa mchezaji alitumia dawa hizo kwa maksudi baada ya taarifa zote kutolewa.

Sharapova ni mshindi mara tano wa Grand slam na kwa mujibu wa jarida la Forbes ni mwanadada anayelipwa zaidi katika mchezo huo kwa miaka 11 mfululizo mpaka alipopitwa na Serena Williams mwaka huu.

Sharapova aligundulika kutumia dawa hizo karibia mwezi mmoja tokea zilipofungiwa januari 2016.

Shearer alikuwa sahihi kusema Uingereza inatapatapa?

Mlinzi wa kushoto wa timu ya taifa ya Uingereza Danny Rose amesema Alan Shearer alikuwa sahihi kuita timu hiyo ya taifa kuwa inatapatapa baada ya kujiuzulu kwa meneja Sam Allardyce.

Anasema kuwa sio jambo zuri kwa meneja kuondoka muda mfupi akiwa bado hajatimiza mikakati aliyojiwekea na hilo linaathiri pia wachezaji.





''Nilimtumia ujumbe nikimshukuru kwa kunijumuisha katika kikosi chake, na kunifanya kuwa na heshima ningine katika ulingo wa soka la kimataifa, nikamwambia pole sana kwa kupoteza nafasi yake na kumtakia kila la kheri mbeleni'' alisema Rose.


Allardyce ameingia katika historia ya kukaa kwa muda mfupi katika timu hiyo kwa siku 67 tu, aliingia baada ya Roy Hodgson kubwaga manyanga alipotolewa mapema katika michuano ya Euro 2016.

Vijana wakwamisha Uchaguzi DRC

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila ametupilia mbali shutuma kwamba amesogeza mbele tarehe ya uchaguzi ili aendelee kung'ang'ania madarakani.

Rais Kabilla amewaambia waandishi wa habari jijini,Dar es salaam kuwa lengo kuu la Serikali yake kubadili ratiba ya uchaguzi ni kutokuwa na maandalizi ya kutosha.

Amesema serikali yake isingependa kuacha idadi kubwa ya wananchi wake na wengi wao wakiwa ni vijana ambao hawakujiandikisha kupiga kura na wakose haki yao ya kupiga kura .

Mwishoni mwa wiki iliyopita,kiongozi wa tume ya uchaguzi nchini Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo alitangaza uwezekano wa kusogezwa tarehe ya kupiga kura hadi hapo desemba 2018.

Duterte asema Obama anaweza 'kwenda jehanamu'

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amerejelea tena shutuma zake dhidi ya Rais Obama na viongozi wengine wa nchi za Magharibi wanaopinga mpango wake wa kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya.
Kiongozi huyo amesema Bw Obama anaweza "kwenda jehanamu".
Umoja wa Ulaya, ambao pia umemkosoa Bw Duterte, unaweza "kuchagua kwenda eneo la kutakasia dhambi ndogo, kwa sababu jehanamu kumejaa", amesema.
Watu karibu 3,000 wameuawa tangu kiongozi huyo alipoingia madarakani mwezi Juni.
Watu wanaoshukiwa kulangua mihadarati au kuwa waraibu wa dawa hizo wamekuwa wakiuawa na maafisa wa polisi na magenge yanayoungwa mkono na serikali.

Bw Duterte amesema Urusi na China wako tayari kuwa washirika wake.