Upande
wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio iliyopo katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeshindwa kuwasomea washtakiwa hao
mashtaka mapya baada ya wakili anayewatetea, Peter Kibatala kudai kuwa
yaliyofutwa yamerudishwa kwa ‘staili’ tofauti.
Hatua
hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo
mapya.
Wakili
wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa aliwasilisha maombi mahakamani
hapo akiomba kuwasomea hati mpya ya mashtaka washtakiwa hao na Mahakama
iliipokea na kuruhusu isomwe, lakini Wakili Kibatala alipinga kwa madai
kuwa hayatofautiani na yale yaliyofutwa Juni 28, 2016.
Kibatala
alidai katika hati mpya shtaka la kwanza na la tano ni sawa na yale
yaliyokuwamo kwenye hati iliyofutwa mahakamani hapo baada ya kupingwa na
kuonekana hayakustahili kwa mujibu wa sheria.
Baada
ya Kibatala kuwasilisha hoja hizo, Wakili Kishenyi aliiomba Mahakama
hiyo kuiahirisha kesi hiyo kwa muda ili aweze kujibu hoja zilizotolewa
na upande wa utetezi na hakimu aliridhia na kuiahirisha hadi saa sita
mchana.
Ilipofika
mchana, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwapo
mahakamani na kwamba kufutwa kwake haikatazwi kuyarudisha tena na
mashtaka hayo ya awali yalifunguliwa bila ya kuwa na kibali cha
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini hivi sasa yamerudishwa yakiwa na
kibali hicho.
Kuhusu
kukata rufaa, Kishenyi alidai wanakata rufaa kwenye kesi ambayo
ilisikilizwa na kumalizika. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote,
Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo na kuwa atatoa uamuzi wa hoja hizo
mwezi ujao.
Washtakiwa
wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina,
Jabir Idrisa, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob na Lissu
ambao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya
kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni