Jumanne, 16 Agosti 2016

Vijana wazuia gari la Jeshi kubeba jeneza la Rais Mstaafu wa Zanzibar Mzee Aboud Jumbe Mwinyi

Maziko ya Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi (96) aliyefariki dunia juzi jijini Dar es Salaam yalifanyika jana nyumbani kwake Migombani, Zanzibar huku vijana wakikataa gari la Jeshi kubeba jeneza lenye mwili wake. 

Mwili wa hayati Jumbe uliswaliwa katika Msikiti wa Mushawwar, Mwembeshauri mjini Zanzibar  na wakati wanatoka msikitini vijana walimuomba mtoto wa marehemu Mustafa Jumbe kwamba jeneza lisiingizwe kwenye gari badala yake wao watalibeba hadi nyumbani, umbali wa wastani wa kilomita tatu. 
Hata hivyo, walipofika eneo la Kilimani walikuta gari la Jeshi aina ya Land Rover likiwa limeegeshwa kwa ajili ya kubeba jeneza lakini vijana walikataa kulipandisha badala yake waliendelea kubeba kwa kupokezana hadi nyumbani kwa marehemu Migombani ambako alizikwa. 
Haikuweza kufahamika mara moja kwanini vijana hao walikataa gari la Jeshi kubeba jeneza lakini huenda ilikuwa kutekeleza wosia alioutoa Mzee Jumbe wakati wa uhai wake kwamba akifariki dunia jeneza lake lisifunikwe bendera yoyote kama ishara ya maziko ya kiserikali. 
“Sitaki katika maziko yangu kutumbuizwa chochote kiendacho hata kidogo kinyume na mafundisho ya Uislamu,” aliandika katika wasia. 
“Sitaki beni (bendi), sitaki mizinga, sitaki maombolezo wala lolote jingine lenye hata chembe ya kufuru. Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika dunia. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi wangu, duniani na akhera.” 
Aidha, wakati wa kuweka mwili kaburini yalitajwa majina ya watoto wanne wa marehemu; Ismail, Amari, Rashid na Mustafa pamoja na Sheikh Zubeir ambao ndiyo marehemu aliwaandika kwenye wasia wake kwamba watakuwa na haki ya kuuhifadhi mwili wake kaburini. 
Kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu Jumbe katika makaburi ya nyumbani kwake Migombani kwa ajili ya mazishi, Mufti Mkuu pamoja na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi na Sheikh Khamis Haji Khamis waliongoza dua na swala maalumu iliyofanyika saa 6:45 mchana katika Msikiti wa Mushawwar. 
Viongozi mbalimbali wa Serikali, wastaafu, vyama vya siasa na mabalozi walikuwapo kwenye mazishi hayo. Miongoni mwao ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu Othman Mohamed Chande, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, marais wastaafu wa Jamhuri, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi, makamu wa Rais mstaafu Dk Mohamed Ghalib Bilali, Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. 
Jumbe, aliyechaguliwa kuongoza Zanzibar kuchukua nafasi ya Rais wa kwanza, Abeid Amani Karume aliyeuawa mwaka 1972, aliongoza kwa miaka 12 hadi mwaka 1984 alipovuliwa nyadhifa zote serikalini na ndani ya chama tawala, CCM kutokana na kutofautiana kuhusu muundo wa Muungano. 
Tangu alipovuliwa nyadhifa zake amekuwa akiishi nyumbani kwake Mjimwema, Kigamboni na hakuwa anaonekana kwenye shughuli za kiserikali tofauti na viongozi wengine wastaafu. Mara nyingi wakati akiwa bado ana nguvu alijishughulisha na masuala ya kumcha Mungu.
 Walivyomkumbuka 
Katika mazishi hayo, viongozi mbalimbali wa serikali, wanasiasa na wananchi waliohudhuria walimuelezea kuwa alikuwa jasiri, mnyenyekevu na aliyeishi maisha ya kumcha Mungu. 
“Aliishi maisha ya ucha Mungu, ucha Mungu hauna siasa, hauna chama na hata baada ya kustaafu alichagua kukaa kimya, alishauri kuhusu maendeleo ya nchi bila kuita waandishi wa habari. Ni jambo tunalopaswa kujifunza viongozi tunapostaafu,” alisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, January Makamba.
Makamba alisema Jumbe ni kiongozi aliyeweka historia ya Zanzibar kwa kuanzisha Katiba ya Zanzibar na Baraza la Wawakilishi na kwamba kuna haja ya kuenzi mchango wake. 
Lowassa alimzungumzia Jumbe kama mtu jasiri aliyesimamia kile alichokiamini na kwamba alikuwa mwaminifu na mwenye kufuata utaratibu. 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alimzungumzia Jumbe kama mtu mwenye msimamo, hasa alipotaka Muungano wa Serikali tatu msimamo aliosema hata yeye anauunga mkono. 
Pia, alisisitiza kwamba Jumbe alikusudia kulinda kikamilifu heshima ya watu wa Unguja na Pemba.
“Nadhani wananchi watakumbuka Jumbe alivyoweza kusimama na kujenga hoja juu ya haja ya kuwa na muundo wa Muungano usiokinzana, yaani wa Shirikisho au kama alivyotaja mwenyewe ‘The partnership’ katika azma ya kuheshimu nchi mbili huru zilizoungana, Tanganyika na Zanzibar”, alisema Maalim Seif. 
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Ramadhani Dau alisema, “Marehemu namtamka kwa neno moja tu: Unyenyekevu.” 
Dk Dau alisema maisha ya marehemu Jumbe yalikuwa ya ucha Mungu, alipenda watu na hakuwa mtu wa kujitutumua kutokana na wadhifa wa urais aliokuwa nao. 
Alisema Jumbe aliishi maisha ya kawaida toka nyumba yake ya Mjimwema, Dar es Salaam na Unguja kwenye nyumba yake ya Migombani. 
“Angekuwa kiongozi mwingine hapa ungeona mbwembwe nyingi, lakini huyu mambo yamekwenda kawaida, alijitolea kwenye misikiti na shughuli zote za kidini,” alisema Dk Dau. 
Watoto wa marehemu Jumbe, Suleiman na Ismail walisema kuwa bila shaka baba yao alithamini hatma ya maisha yake ya baadaye, duniani na akhera na hapakuwa na budi wao pamoja na Serikali zote mbili kuheshimu kile alichokiamini yeye kama wasia. 
Maombolezo siku saba 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza siku saba za maombelezo zitakazohusisha kupandishwa bendera nusu mlingoti, lakini shughuli zingine zitaendelea kama kawaida.
Familia ya Mzee Jumbe ilitangaza kuwa viongozi mbalimbali wa dini na Serikali watajumuika pamoja kesho katika Msikiti wa Mushawwar kwa ajili ya dua ya ziada na khitma ya marehemu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni