Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani
Mara wamemtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kumchukulie hatua za
kisheria ofisa kilimo na mifugo wa halmashauri hiyo,Serapaion Rujuguru kwa madai
kuwa ametoa taarifa za uongo.
Rujuguru anadaiwa kutoa majibu ya uongo kwenye moja ya
azimio la kikao cha baraza hilo cha mwezi Mei mwaka huu lililomtaka aeleze kile
alichokifanya kuhakikisha kwamba fedha za pembejeo zilizogawiwa kwa wakulima wa
kata ya Namhura wilayani humo kiasi cha sh.46mil kimerejeshwa.
Wakiongea katika kikao cha kawaida cha baraza hilo
kilichofanyika mwishoni mwa wiki madiwani hao akiwemo Renatus Karoli wa kata ya
Kibara na Jogoro Amoni wa kata ya Namhura walisema kitendo cha ofisa huyo
kuongopa hakivumiliki hivyo sharti mwajiri wake amchukulie hatua.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mwibara,Kangi Lugora alitilia
shaka kama azma ya serikali ya kuboresha sekta ya kilimo kwa lengo la kuinua
uchumi wa taifa itafikiwa katika wilaya hiyo ikiwa wahusika wenyewe wanatengeneza
taarifa za uongo.
Hata hivyo majibu yake,ofisa kilimo huyo aliahidi
kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Isack
mahela Kabugu akiwatahadharisha watendaji kuachana na tabia ya kunakili jambo
bila kujua uhalisia wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni