Jumanne, 30 Agosti 2016

Wakili Apinga Tundu Lissu Kusomewa Mashitaka Mapya........ Hakimu aahirisha kesi hadi mwezi ujao

Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wahariri wa Gazeti la Mawio iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu umeshindwa kuwasomea washtakiwa hao mashtaka mapya baada ya wakili anayewatetea, Peter Kibatala kudai kuwa yaliyofutwa yamerudishwa kwa ‘staili’ tofauti. 
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kibatala kuwasilisha hoja mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba za kupinga washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo mapya. 
Wakili wa Serikali Mkuu, Kishenyi Mutalemwa aliwasilisha maombi mahakamani hapo akiomba kuwasomea hati mpya ya mashtaka washtakiwa hao na Mahakama iliipokea na kuruhusu isomwe, lakini Wakili Kibatala alipinga kwa madai kuwa hayatofautiani na yale yaliyofutwa Juni 28, 2016.
Kibatala alidai katika hati mpya shtaka la kwanza na la tano ni sawa na yale yaliyokuwamo kwenye hati iliyofutwa mahakamani hapo baada ya kupingwa na kuonekana hayakustahili kwa mujibu wa sheria. 
Baada ya Kibatala kuwasilisha hoja hizo, Wakili Kishenyi aliiomba Mahakama hiyo kuiahirisha kesi hiyo kwa muda ili aweze kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi na hakimu aliridhia na kuiahirisha hadi saa sita mchana. 
Ilipofika mchana, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la tano ni kama hayakuwapo mahakamani na kwamba kufutwa kwake haikatazwi kuyarudisha tena na mashtaka hayo ya awali yalifunguliwa bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini hivi sasa yamerudishwa yakiwa na kibali hicho. 
Kuhusu kukata rufaa, Kishenyi alidai wanakata rufaa kwenye kesi ambayo ilisikilizwa na kumalizika. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo na kuwa atatoa uamuzi wa hoja hizo mwezi ujao. 
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob na Lissu ambao kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano yakiwamo ya kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002

Tamko La Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za Binadamu Dhidi Ya Mauaji Ya Askari Wa Jeshi La Polisi

Mtandao wa Watetezi wa Waki za Binadamu (THRDC) kwa niaba ya wanachama wake tunalani vikali maujai ya askari wa jeshi la polisi huku tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi wanaofanya kazi katika misingi na sheria ni watetezi wa haki za binadamu kama walivyo watetezi wengine. 

Kutokana na taarifa rasmi ya jeshi la polisi ni kwamba mnamo tarehe 23/08/2016 saa moja usiku maeneo ya Mbagala Mbande kata ya Mbande Temeke, majambazi ambao idadi yao haikuweza kufahamika wakiwa na silaha za moto walivamia benki ya CRDB tawi la Mbande ambapo waliwashambulia na kuwaua askari wanne wa Jeshi la Polisi waliokuwa kazini na kuwajeruhi raia wawili waliokuwa jirani na eneo hilo. 
 
Askari waliofariki katika tukio hilo ni E,5761 CPL Yahaya, F,4660 CPL Hatibu, G9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone na raia waliojeruhiwa ni Ally Chiponda na Azizi Yahaya wote wakazi wa Mbande. 
Katika tukio hilo, majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbili za SMG na risasi sitini (60) na hakuna pesa au mali za benki iliyoibiwa, ni dhahiri kwamba walikuwa na kusudio la kujipatia silaha kwa ajili ya kufanya uhalifu na si vinginevyo kama baadhi walivyotaka kupotosha. 
Ikumbukwe kuwa majambazi mara kadhaa mwaka jana katika maeneo mbalimbali chini, mfano Kituo cha Stakishari Dar es Salaam na Kituo cha Polisi Ikwiriri , vilivyamiwa na majambazi kwa lengo la kuchukua silaha kwa ajili ya uhalifu.
 
Aidha, Tunalipongoza Jeshi la Polisi kwa kuweza kuwafikia majambazi hao huko Mkuranga bila kuumiza raia. Pia tunatoa pole kwa familia za askari wote watano waliopoteza maisha wakiwa kazini. 
Askari anaekamilsha idadi ya askari waliouwawa kufika watano ni Askari Thomas Njiku,Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi alieuwa Vikindu wilayani Mkuranga wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu waliosadikiwa kuwa ni majambazi waliotekeleza tukio la kihalifu la Mbade,Mbagala.
 
Tunawasihi Watanzania kutoipokea dhana inayotaka kujengwa na wanasiasa kuwa hatukemei matukio haya dhidi ya polisi. 
Kumbukeni kuwa Mtandao wa Watetezi umekuwa ukitoa matamko mbali mbali kukemea mauaji ya askari wa jeshi la polisi, na tumekuwa mara kwa mara tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi ni watetezi wa haki za binadamu, kwa kuwa jukumu lao la kwanza ni kulinda mali za watu na usalama wa binadamu. 
Mtandao unatambua kuwa askari wa jeshi la polisi pia ni ndugu zetu, kaka zetu na baba zetu hivyo madhila wanayokumbana nayo ni yetu sote.
 
Mfano, katika repoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu kwa mwaka jana(2015) , Mtandao uliweza kuwa na kipengele maalumu kilichozungumzia haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa haki za binadamu.
 Katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo Mtandao uliweza kurekodi matukio ya uvamizi na mauaji ya jeshi la polisi zaidi ya kumi (10) na wengine watano (5) wakiachwa wamejeruhiwa. Kwa maana hii tukio lilitokea Mbagala ni muendelezo wa matukio ya kiuhalifu yanayoendelea nchini. 
 
Kumekuwa na changamoto kutoka kwa Jamii kuwatambua askari wa jeshi la polisi kama watetezi wa haki za binadamu, na hii ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao kukandamiza haki za wananchi. 
Hali ilivyo sasa inaweza kuharibu dhana nzima ya polisi kuwa ni walinzi wa raia na mali zao, kwani vitendo wanavyofanya polisi dhidi ya raia hasa wafuasi wa vyama vya siasa na viongozi wao ni sababu kubwa ya kuharibu uhusiano mzuri kati ya polisi na raia.
 
Mtandao unatambua kwamba jeshi la polisi ni mamlaka muhimu sana katika kustawisha amani na ulinzi wa nchi kama litakuwa huru, bila kuingiliwa na wanasiasa na kuegemea upande wowote. 
Mtandao unapenda kuona kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi na kwa mujibu wa sharia na katiba ya nchi. Aidha, Mtandao unaona pamoja na migongano mbali mbali ya kazi za polisi na za wanasiasa ( hasa nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya), ni vyema polisi wakaangalia misingi ya kimataifa ya haki za binadamu ili kuhakikisha usawa mbele ya jamii ili kurudisha mahusiano mazuri baina ya polisi na jamii wanayoitumikia.
 
Sambamba na hayo, Mtandao pia umesikikitishwa na kauli ya Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Mhe Paul Makonda aliyotoa tarehe 25 agosti 2016 wakati wa kuaga miili ya askari wanne waliouwawa huko Mbande Mkoani Dar es Salaam. Mtandao unakemea matamshi ya aina hiyo kutoka kwa kiongozi yoyote Yule, kwakuwa matamshi kama haya yanakwenda kinyume na misingi ya utawala bora na haki za binadamu na yanaweza kuwa sehemu ya kupoteza amani ya Taifa. Kitendo cha kukejeli haki za binadamu na kuamuru askari polisi wapige tu bila kujali taratibu za kisheria kinakwenda kinyume na misingi ya utawala bora.
 
Tunapenda viongozi wa serikali watambue kwamba kazi ya kulinda na kutetea haki za binadamu ni ya kikatiba na ndiyo maana kupitia Katiba yetu tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha viongozi wanaheshimu misingi ya utawala bora na haki za binadamu. Watetezi wa haki za binadamu wanatambulika kote duniani na wanalindwa kisheria mfano, kimataifa tuna Tamko la watetezi wa haki za binadamu la mwaka 1998. 
 
Madhara ya Uhusiano Mbaya kati ya Polisi na Raia
Ili Jeshi la Polisi liweze kufanya kazi yake vizuri ya kupambana na uhalifu hawana budi kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi. Madhara ya kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na raia ni makubwa. 
 
• Mojawapo ya madhara ni pamoja na kukua kwa makosa ya jinai na polisi kukosa taarifa za waalifu toka maoneo mbalimbali.
• Hali ya makosa ya jinai Tanzania imezidi kukua katika kiwango kikubwa. Kukua kwa makosa ya jinai ni zao la kutokuwa na mahisiano mazuri kati ya raia na polisi.
Wito wetu;
• Mtandao unatoa pole kwa Jeshi la Polisi pamoja na familia za askari hao na tunatoa wito kwa askari wengine wa jeshi la polisi kuendelea na kazi zao kwa weledi huku wakiboresha mahusiano mazuri na wananchi.
• Tunaishauri serikali kuliongezea nguvu Jeshi la polisi na kuboresh utalaamu katika kufanya kazi zao
• Tunawasihi askari wa Jeshi la wananchi kuheshimu mipaka ya kazi zao na kuheshimu haki za binadamu na katiba ya nchi katika kutekeleza kazi zao za kila siku
• Tunaishauri serkali kuwe na mabadiliko katika mfumo wa jeshi la polisi kuanzia kwenye mfumo wa kisheria ambao utatoa wajibu na uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu
• Tunaomba umma kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na vyombo vya usalama hasa pale wanapohisi kuna tukio linalo ashiria uvunjaji wa amani na usalama.
• Tunaiomba serikali yetu kuipa kipaumbele jeshi la polisi katika kuboresha vitendea kazi vyao,nyumba za kuishi na mishahara bora ili kukidhi hali ya maisha ya sasa.
• Tunawaomba wadau wengine wa Haki za Binadamu pamoja na mashirika mengine ya maendeleo kukemea vikali tukio hilo. Tunashauri viongozi wa siasa waache kuingilia kazi za polisi ili kuepuka migogoro
 
PICHANI  JUU :Wakili wa THRDC akiwaonyesha waandishi wa habari(hawapo pichani) repoti ambayo ilitolewa na THRDC juu ya hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu kwa mwaka jana(2015) ,ambayo ina kipengele maalumu kilichozungumzia haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa haki za binadamu katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo, 
 
Imetolewa na Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
 
Imewasilishwa na Bennedict Ishabakaki
Wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
 
30/08/2016

Jumapili, 21 Agosti 2016

Wananchi wa Mkoa wa Mara wana asilimia 53% tu ya maji safi na salama




Mkoa wa Mara umegundulika kuwa chini ya viwango vizuri vya kitaifa vya upatikanaji  vya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi jambo ambalo linatajwa kuwa moja ya sababu inayopelekea magonjwa ya mripuko kutokea katika  mkoa huo.

Hayo yalisemwa na mkuu wa Mkoa wa Mara dk.Charles Mulingwa wakati akizungumza na watumishi wa serikali pamoja na madiwani wa halmashauri zote mbili ya mji wa Bunda na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda katika ukumbi wa mikutano mjini Bunda.

Mulingwa alisema kuwa bila kujali mijini au vijijini katika suala la maji safi na salama  kwa wastani ni asilimia 53 licha ya kuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo vingesaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

“Ni sema bila kujali kuwa mjini au kijijini hali hii ya kutopatikana kwa maji safi na salama ipo asilimia 53% tu” alisema Mulingwa

Naye mkuu wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili alitumia fulsa hiyo kumuomba mkuu wa Mkoa kusaidia kusukuma suala la kuhamishwa kwa makao makuu ya hifadhi ya mbunga ya wanyama  Serengeti Nation park kuhamishiwa mjini Bunda ili kusaidia huduma zingine kusonga mbele.

Halmashauri ya wilaya ya Bunda ya omba gari la wagonjwa



Serikali imeombwa kuangalia uwezekano wa kuipatia halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara gari la wagonjwa haraka iwezekanavyo hali itakayosaidia kuboresha kwa huduma ya afya wilayani humo.

Mganga mkuu wa halmashauri hiyo,Dk.Jonathan Budemu aliwasilisha ombi katika taarifa yake aliyoitoa kwa mkuu wa wilaya hiyo,Lydia Bupilipili akisema kukosekana kwa gari hilo kumezorotesha kwa kiwango kikubwa huduma ya afya.

Dk.Budemu aliyemwomba mkuu huyo wa wilaya kusaidia kusukuma kufanikiwa kwa ombi hilo, amesema kutokana na hali hiyo wamekuwa wakishindwa kuwasafirisha kwa wakati wagonjwa mahututi kuwapeleka kwenye matibabu zaidi.

Kwa upande wake Bupilipili licha ya kukubali kusukuma utekelezwaji wa ombi hilo lakini pia aliwataka watumishi wa idara ya afya kufanya kazi zao kwa uadilifu wakizingatia kwamba wanashughulika na maisha ya watu huku akionya kutosita kumwadhibu kisheria mzembe.

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bunda wamemtaka mkurugenzi kumwajibisha Ofisa kilimo na mifungo



Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara wamemtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kumchukulie hatua za kisheria ofisa kilimo na mifugo wa halmashauri hiyo,Serapaion Rujuguru kwa madai kuwa ametoa taarifa za uongo.

Rujuguru anadaiwa kutoa majibu ya uongo kwenye moja ya azimio la kikao cha baraza hilo cha mwezi Mei mwaka huu lililomtaka aeleze kile alichokifanya kuhakikisha kwamba fedha za pembejeo zilizogawiwa kwa wakulima wa kata ya Namhura wilayani humo kiasi cha sh.46mil kimerejeshwa.

Wakiongea katika kikao cha kawaida cha baraza hilo kilichofanyika mwishoni mwa wiki madiwani hao akiwemo Renatus Karoli wa kata ya Kibara na Jogoro Amoni wa kata ya Namhura walisema kitendo cha ofisa huyo kuongopa hakivumiliki hivyo sharti mwajiri wake amchukulie hatua.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mwibara,Kangi Lugora alitilia shaka kama azma ya serikali ya kuboresha sekta ya kilimo kwa lengo la kuinua uchumi wa taifa itafikiwa katika wilaya hiyo ikiwa wahusika wenyewe wanatengeneza taarifa za uongo.

Hata hivyo majibu yake,ofisa kilimo huyo aliahidi kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Isack mahela Kabugu akiwatahadharisha watendaji kuachana na tabia ya kunakili jambo bila kujua uhalisia wake.