Alhamisi, 9 Februari 2017

WATUHUMIWA 17 WA DAWA ZA KULEVYA WAKAMATWA SHINYANGA…MAJINA MENGINE ZAIDI YA 20 YAPO KWA DC SHINYANGA

Na mwandishi wetu 
Vita dhidi ya dawa za kulevya imetua mkoani Shinyanga ambapo jumla ya watu 17 wanaotuhumiwa kuwa ni watumiaji wa dawa hizo ikiwemo unga na mirungi wanashikiliwa na jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga. 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro,ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya hiyo amesema mbali na watu 17 kushikiliwa na polisi pia ofisi yake imepokea majina zaidi ya 20 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya. 

“Mheshimiwa rais ametangaza kuwa hii ni vita ya nchi nzima,baada ya wananchi kusikia vita ya dawa za kulevya ikiendelea mkoani Dar es salaam,wametuletea majina zaidi ya 20 ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya,wanasema wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali kupiga vita dawa hizi”,amesema Matiro. 

“Wananchi wenyewe kwa moyo mweupe kabisa ndiyo wametuletea majina ya watu wanaotumia na kuuza dawa za kulevya ikiwemo unga na mirungi,kamati ya ulinzi na usalama tumeunda kikosi kazi cha kushughulikia majina yanayoletwa ili kubaini kama ni kweli wanajihusisha na dawa za kulevya”,alisema Matiro. 

Ametumia fursa hiyo kulipongeza jeshi la polisi kwa jitihada zake dhidi ya dawa za kulevya na kufanikisha kukamata watuhumiwa 17 huku akikisisitiza kuwa vita hiyo siyo ya Dar es salaam pekee bali inatakiwa kufanyika nchi nzima kwani watumiaji na wauzaji wa dawa hizo wapo kila mahali nchini. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni