Harakati za marafiki wa Elimu,ni muunganiko wa wananchi mmoja mmoja
,makundi na asasi ,taasisi zenye mapenzi na nia ya kuona kunakuwepo maendeleo
chanya katika michakato ya utoaji na usimamizi wa elimu nchini.
Harakati hizo zilianza mwaka 2003 kwa utaratibu wa karibu wa asasi ya
hakielimu hadi sasa harakati hizi zina wanachama takribani 40,000 walioenea
pande zote za nchi wakiwakirisha makundi mbali mbali ndani ya jamii
,walimu ,wanafunzi,wanasiasa,wafanyakazi wa umma ,wazazi na kina mama.
Tangu kuanzishwa kwa harakati hizo marafiki wamekuwa chachu katika
uhamsishaji jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo ya elimu popote pale
walipo.Aidha wamekuwa nyenzo kuu katika kuchangia uwajibikaji wa watendaji na
wadau mbali mbali ili kuongeza na kuboresha utoaji wa huduma kwa watu wao.
Ili kuboresha utendaji kazi na ushiriki wa Marafiki katika shughuli za
elimu na utawala bora ,Asasi ya HakiElimu kwa kushirikiana na wadau wengine wa
Elimu imekuwa ikiwajengea uwezo Marafiki kupitia Mafunzo mbali mbali na
upatikanaji wa taarifa mbali mbali ambazo ni za muhimu katika sekta ya Elimu.
Kutokana na hali hiyo Wadau wa mtandao wa marafiki wa elimu Mkoani
Geita,wamekutana na kutoa taarifa ya majumuisho ya ufuatiliaji wa uwajibikaji
wa Jamii huku wakibainisha changamoto kubwa ambazo wamekutana nazo
ni upungufu wa walimu kwa baadhi ya shule zina walimu wengi ilihali
nyingine zina upungufu mkubwa .Sera ya elimu na Mafunzo imetoa mwongozo
kuwa mwalimu mmoja anatakiwa kuhudumia wanafunzi arobaini na tano.
Akielezea hali ya elimu mratibu wa Marafiki wa Elimu Mkoa wa Geita,Ayubu
Bwanamadi alisema tatizo la walimu kuwa wachache ni tatizo kubwa ambalo
linaendelea kudidimiza elimu kwani katika darasa nunakuta mwalimu mmoja
anafundisha zaidi ya wanafunzi 150 hadi 200 ambapo ni kinyume na sera ya Elimu.
Meneja wa idara ya ushiriki na uwajibikaji jamii Pius Makomelelo ,ametoa
mapendekezo ambayo yataboresha elimu ni pamoja viongo kupatiwa elimu ,lakini
pia halmashauri zilizopo Mkoani Hapa kuwekeza kwenye mafunzo ya
Tehama.
Aidha kwa Upande wake Lusenga Robart Manjale Kutoka Taasisi Ya
CODERT ameelezea masikitiko yake kutokana na hali ilivyo ya mlundikano wa
wanafunzi ambapo alitoa ushauri kwa wazazi na walezi kuchangia swala la
elimu na kuacha kusubilia serikali ifanye shughuli hiyo.
Akimwakilisha katibu tawala wa Mkoa wa Geita,Elysalver Nkanga amesema
kuwa wataakikisha wanashirikiana na wadau wa Elimu kuboresha zaidi elimu
Mkoani Humo.