Jumamosi, 1 Aprili 2017

Hali ya elimu bado ni tatizo mkoani geita



Harakati za marafiki wa Elimu,ni muunganiko wa wananchi mmoja mmoja ,makundi na asasi ,taasisi zenye mapenzi na nia ya kuona kunakuwepo maendeleo chanya katika michakato ya utoaji na usimamizi wa elimu  nchini.
Harakati hizo zilianza mwaka 2003 kwa utaratibu wa karibu wa asasi ya hakielimu hadi sasa harakati hizi zina wanachama takribani 40,000 walioenea pande zote za nchi wakiwakirisha makundi mbali mbali ndani  ya jamii ,walimu ,wanafunzi,wanasiasa,wafanyakazi wa umma ,wazazi  na kina mama.

Tangu kuanzishwa kwa harakati hizo marafiki wamekuwa chachu katika uhamsishaji jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo ya elimu popote pale walipo.Aidha wamekuwa nyenzo kuu katika kuchangia uwajibikaji wa watendaji na wadau mbali mbali ili kuongeza na kuboresha utoaji wa huduma kwa watu wao.

Ili kuboresha utendaji kazi na ushiriki wa Marafiki katika shughuli za elimu na utawala bora ,Asasi ya HakiElimu kwa kushirikiana na wadau wengine wa Elimu imekuwa ikiwajengea uwezo Marafiki kupitia Mafunzo mbali mbali  na upatikanaji wa taarifa mbali mbali ambazo ni za muhimu katika sekta ya Elimu.

Kutokana na hali hiyo Wadau wa mtandao wa marafiki wa elimu Mkoani Geita,wamekutana na kutoa taarifa ya majumuisho ya ufuatiliaji wa uwajibikaji wa Jamii huku  wakibainisha changamoto kubwa  ambazo wamekutana nazo ni  upungufu wa walimu  kwa baadhi ya shule zina walimu wengi ilihali nyingine zina upungufu mkubwa .Sera ya elimu na Mafunzo imetoa mwongozo  kuwa mwalimu mmoja anatakiwa kuhudumia wanafunzi arobaini na tano.

Akielezea hali ya elimu mratibu wa Marafiki wa Elimu Mkoa wa Geita,Ayubu Bwanamadi alisema tatizo la walimu kuwa wachache ni tatizo kubwa ambalo linaendelea kudidimiza elimu kwani katika darasa nunakuta mwalimu mmoja anafundisha zaidi ya wanafunzi 150 hadi 200 ambapo ni kinyume na sera ya Elimu.

Meneja wa idara ya ushiriki na uwajibikaji jamii Pius Makomelelo ,ametoa mapendekezo ambayo yataboresha elimu ni pamoja viongo kupatiwa elimu ,lakini pia halmashauri  zilizopo Mkoani Hapa kuwekeza kwenye  mafunzo ya Tehama.

Aidha kwa Upande wake Lusenga Robart  Manjale Kutoka Taasisi Ya  CODERT ameelezea masikitiko yake kutokana na hali ilivyo ya mlundikano wa wanafunzi   ambapo alitoa ushauri kwa wazazi na walezi kuchangia swala la elimu na kuacha kusubilia serikali ifanye shughuli hiyo.

Akimwakilisha katibu tawala wa Mkoa wa Geita,Elysalver Nkanga amesema kuwa wataakikisha wanashirikiana na  wadau wa Elimu kuboresha zaidi elimu Mkoani Humo.


kampuni ya sola ya Sunking latua Mkoa wa Mara



Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa  bunda  janeth mayanga , aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya bi lydia bupilipili katika uzinduzi wa  kampuni ya sola ya  sunking  amesema kuwa ujio wa kampuni hiyo itasaidia  ongezeko la   fursa za  ajira  kwa jamii katika mji wa bunda na mkoa wa mara kwa ujumla .

Kufuatia uzinduzi huo Mayanja  amewaomba  wananchi kujitokeza kwa wingi kununua  mitambo ya sola kutoka katika kampuni hiyo kwa kuwa ina sola nzuri na inayokidhi mahitaji ya watumiaji wake.
Aidha Mayanja amewakumbusha mawakala wa kampuni hiyo kufuata sheria ya vibali na kulipa kodi ili serikali iweze kujipatia mapato.

Kwa upande wake afisa biashara wa kampuni hiyo bi Jodie Wu  amesema kuwa  bidhaa hiyo  imesambazwa katika wilaya  tano za mkoa wa mara ikiwemo Rorya, Tarime, Butiama, Bunda  na Serengeti ambapo kwa sasa ina jumla ya mawakala 50.

Hata hivyo bi wu  amesema kuwa  Nia ya Sunking ni kuhakikisha wananchi wa maisha ya chini wanaishi kama matajiri, kwani wameamua kuwaletea mwanga mzuri kwa bei ya chini kabisa.

Kauli ya niyonzima dhidi ya azam fc leo


  Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, anaamini kabisa kama timu yake inataka kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ni lazima leo Jumamosi iifunge Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga na Azam tangu mwaka 2008, zimekutana mara 17 katika ligi kuu na zote zimeshinda mechi tano kila moja na zimetoka sare mara saba. Yanga imefunga mabao 23 na Azam imefunga mabao 22.

Katika msimamo wa ligi kuu, Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 53 nyuma ya Simba iliyo kileleni na pointi 55, Azam ni ya tatu na pointi 44.

Niyonzima raia wa Rwanda, amesema mchezo huo utakuwa mgumu kulingana na historia yao kila wanapo-kutana lakini kwao ni muhimu kwani wakishinda watakuwa na mwanga mzuri wa kutwaa ubingwa.

“Mechi yetu na Azam ni mchezo mkubwa na utakuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na kila upande kuhitaji ushindi, lakini tumejipanga kushinda kwani ndiyo mechi ambayo itatoa mwelekeo wa kutetea ubingwa wetu.

“Ni lazima tushinde mechi hii ili tujiweke katika nafasi ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, tuna majeruhi wengi lakini tutapambana ili tushinde,” alisema Niyonzima.
SOURCE: CHAMPIONI

Wananchi wa Mji wa Bunda Mkoa Mara leo siku ya tatu hawana maji safi na salama




Redio Mazingira Fm sauti ya jamii iliyopo katika Mji Wwa Bunda Mkoani Mara Kupitia kipindi cha Duru za Habari(DZH) kinachoendeshwa na Thomas J Masalu na Andrew Mbwiga kuanzia saa kumi kamili jioni hadi saa kumi na mbili jioni katika cha kipengele cha Kubwa la leo siku ya jana walikusogezea habari kuhusu Shirika la umeme Tanzania Tanesco wilaya ya Bunda Mkoa Mara, kuwa wametekeleza agizo lililoagizwa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli la kusitisha huduma ya umeme kwa wale wote wanaodaiwa.

Kaimu meneja wa tanesco wilayani hapo bwana Yusuph Mbaa alisema wametekeleza agizo hilo kwa kuanza kuwakatia umeme mamlaka ya maji wilaya ya bunda kwa kushindwa kulipa deni wanalodaiwa  zaidi ya shilingi milioni 200.

Aliiambia Mazingira fm kwamba kufikia hatua ya kukata umeme kwa mamlaka ya maji inatokana na deni la muda mrefu na tayari walikwishapewa notisi ya kutakiwa kulipa deni hilo lakini hawakutekeleza, na kuongeza kuwa wadaiwa wengine pia wameshapatiwa taarifa ya kutakiwa kulipa madeni yao kwani Tanesco bado wako katika hatua ya kutekeleza agizo la Rais ili shirika lijiendeshe.

Hata hivyo bwana mbaa aliwataka wateja wengine wanaodaiwa na hawajalipa kulipa madeni hayo ili kuepukana na usumbufu wanaoweza kuupata pindi watakapokatiwa umeme.

VIONGOZI WA DINI MKOANI SHINYANGA WASHUSHA UPAKO KWENYE SHULE ILIYOKUBWA NA MAPEPO



Machi 30,2017 redio Mazingira fm iliyopo Mjini Bunda Mkoani Mara kupitia kipindi pendwa cha Duru za habari (DZH) kinachoendeshwa na #Thomas J Masalu na Andrew Mbwiga kuanzia saa kumi kamili jioni hadi saa kumi na mbili jioni katika kipengele cha kubwa la leo walikusogezea habari kuhusu Shule ya sekondari Imesela kuvamiwa na mapepo na kuwafanya wanafunzi kuanguka na kutamka maneno yasiyoeleweka!!.

Hali hiyo ilimlazimisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama kufika shuleni hapo na kujionea hali halisi na kutangaza ufanyike mkutano siku ya Ijumaa Machi 31 kwa ajili kutafutaufumbuzi wa tatizo hilo.

Sasa jana Machi 31,2017,Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Shinyanga wamefanya maombi maalum kuwaombea wanafunzi waliopatwa na mapepo na kusababisha kuanguka na kupiga kelele wakitamka maneno yasiyoeleweka katika shule ya sekondari Imesela iliyopo wilaya ya Shinyanga.
Viongozi hao wa dini walifika shuleni hapo wakiongozana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Josephine Matiro.

Viongozi hao wa dini mara baada ya kufika katika shule hiyo walishuhudia wanafunzi wakianguka,kugaragara huku wakitamka maneno ya ajabu ajabu ambapo chanzo chetu cha habari kimeshuhudia viongozi hao wakiwafanyia maombi wanafunzi hao na kurudi katika hali zao za kawaida.

Viongozi hao wa dini pia walifanya maombi madarasani,vyoo vya wanafunzi na kwenye baadhi ya miti iliyopo katika shule hiyo ambapo baadhi inadaiwa kuwa pale inapoguswa watu hupigwa shoti kama ya umeme.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa maombi hayo mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Shinyanga Elias Madoshi alisema wamefika hapo kuvunja nguvu za shetani ambazo zinawafanya wanafunzi wakose masomo yao na kwamba jambo hilo ni la aibu na fedheha kubwa katika nchi.

“Sisi viongozi watumishi wa mungu tuliopewa mamlaka na mungu kabla hatujaja hapa tumeoneshwa na mungu tumeshamjua mhusika wa mchezo huu wa kijinga,tunamuonya na tunamtaka aache kuanzia sasa,kama hataacha mtamzika hapa kijijini,tunamtaka asirudie mungu hachezewi”,alisema mchungaji Madoshi.
Naye Askofu Josephat Mussa wa kanisa la Tanzania Mision Revival Church (TMRC) alisema viongozi wa dini kamwe hawawezi kukaa kimya na kufurahia vitendo hivyo vya kishirikina na kwamba viongozi wa dini watafanya kambi katika kata ya Imesela ili watu wamjue mungu.

Naye Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu Wahmadyiya mkoa wa Shinyanga sheikh Shaban Luseza alisema asilimia kubwa na wananchi mkoani Shinyanga hawamjui mungu hivyo kuwataka kumwamini mungu.
Sheikh Luseza alishauri wananchi kumwamini mungu kwani kama huna ulinzi wa mwenyezi huna lazima vitendo vya mashetani,mizimu lazima vikupate.

“Lazima mmrudie mungu,asilimia 60 mpaka 70 ya watu Shinyanga hawafuati dini ndiyo maana matatizo haya yanajitokeza,ukiamua kumwelekea mungu naye atakuelekea na kukupa ulinzi”,aliongeza sheikh Luseza.
Kwa upande wake Sheikh Masoud Ramadhan alieleza kukerwa na vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa wanafunzi hao na kuongeza kuwa kviongozi wa dini wamekubaliana kushirikiana ili kumaliza tatizo linalowakumba wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela.

Awali kabla ya kufanya maombi hayo maalumu mkuu wa wilaya alifanya mkutano na wananchi wa kata ya Imesela na kata jirani kujadili namna ya kumaliza tatizo hilo ambapo kwa pamoja walikubaliana viongozi wa dini wafanye maombi badala ya kutumia njia za kienyeji (waganga) kumaliza tatizo hilo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema tatizo la wanafunzi kufanyiwa vitendo vya kishirikina linawaathiri wanafunzi na kusababisha kutohudhuria vipindi darasani kwa kukumbwa na mapepo hayo.

Aidha Matiro aliwataka wananchi kumwamini mungu kwa kila jambo badala ya kuamini katika matambiko kwani hakuna nguvu inayoweza kumshinda mwenyezi mungu.

Kufuatia maombi hayo wanafunzi wa shule hiyo walieleza kufarijika na hatua ya uongozi wa wilaya kufika na viongozi wa dini kufanya maombi hali ambayo inawapa matumaini ya kuendelea na masomo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Imesela yenye jumla ya wanafunzi 252 iliyoanzishwa mwaka 2006 wamekumbwa na mapepo yanayowaangusha na kujikuta wakitamka maneno yasiyoeleweka huku wakitaja majina ya wahusika wanaowafanyia ushirikina.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la shule hilo tatizo hilo limeanza mwezi Novemba mwaka 2016 na hali ilianza kuwashtua mwezi Januari mwaka 2017 na hali ilikuwa mbaya zaidi mwezi Machi mwaka huu ambapo wanafunzi 16 walipatwa na ugonjwa huo usiofahamika na hali imeendelea hivyo kila wanapofika tu shuleni saa moja na nusu asubuhi.