Alhamisi, 15 Septemba 2016

JK azungumza Kuhusu Rais Magufuli Kutokwenda Zambia

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ameunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli kuahirisha safari kwenda nje ya nchi ili kushiriki katika maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Kikwete amesema uamuzi huo ni wa busara kwa kuwa Serikali inatakiwa kufanya juhudi za makusudi kushughulikia tatizo hilo.

Kikwete aliyemtumia salamu za pole Dk Magufuli na waathirika wa tukio hilo, amesema misaada ya haraka na dharura inahitajika ili waathirika waendelee kupata huduma zote muhimu hasa za kibinadamu.

Kiongozi huyo mstaafu ameyasema hayo  katika hafla ya makabidhiano ya nyumba 22 za watumishi wa afya, 10 zikiwa Chalinze, mbili Bagamoyo na nyingine 10 Mafia zilizojengwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa mkoani Pwani.

“Ndugu zangu pamoja na leo hii tunakabidhiana nyumba 22 za watumishi wa afya mkoani kwetu, naomba tusimame tuwakumbuke wenzetu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi huko Bukoba na pia natumia fursa hii kutoa pole kwa waathirika wote na Rais Dk Magufuli,” amesema.

Ameongeza kuwa: “kiukweli amefanya uamuzi wa busara kuahirisha safari yake ili kushiriki katika maafa haya.”

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Kituo cha Afya Msoga, Chalinze.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni