Jumatano, 14 Septemba 2016

Gavana BOT afichua siri ya kilio cha fedha kupotea mtaani

 
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu jana alitolea ufafanuzi hali ya kiuchumi nchini huku akieleza siri ya kilio kinachovuma cha fedha kupotea mtaani na nyingine zikidaiwa kufichwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa Ndulu alisema kuwa kwakuwa taasisi hiyo ndiyo inayofahamu fedha zote zilizopo benki na zilizopo mtaani, inafahamu kuwa hakuna fedha iliyopotea bali fedha zimepotea kwa watu waliokuwa wanazipata kwa njia ya udanganyifu kwakuwa sasa Serikali imebana mianya hiyo.

“Hakuna fedha iliyopotea, Serikali imebana shughuli za watu na ‘mission town’ sasa shughuli zote zinafanywa na Serikali. Hivyo, kwao fedha zimepotea, lakini kwetu hazijapotea,” alisema Profesa Ndulu.

Hata hivyo, Profesa Ndulu alikiri kupungua kwa fedha katika mabenki nchini hali iliyopelekea kupunguza kasi ya utoaji mikopo kwa wananchi. Alisema hali hiyo ilitokana na kuhamishwa fedha za mashirika ya umma na taasisi kutoka benki za biashara kwenda BoT.

“Fedha hizo zitarudi katika benki hizo wakati zitakapopelekwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali,” Profesa Ndulu aliahidi.

Katika hatua nyingine, Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa uchumi unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.2 mwaka huu, huku akibainisha kuwa moja kati ya sababu zinazopelekea ukuaji huo ni  ongezeko la uzalishaji wa umeme na saraju.

Akizungumzia hali ya deni la taifa, alisema kuwa deni la taifa la ndani limeongezeka kutoka shilingi  trilioni 8.6 Mwezi Desemba mwaka jana hadi shilingi trilioni 10 mwezi Juni mwaka huu.

Profesa Ndulu alibainisha kuwa wakati deni linalotokana na kukopa ndani likipaa, deni linatokana na ukopaji wa limepungua baada ya Serikali kupunguza ukopaji nje ya nchi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni