Alhamisi, 15 Septemba 2016

Kompyuta zenye majibu ya waliopima ukimwi zaibwa

Kompyuta mpakato zenye majibu ya watu waliopima ukimwi pamoja na majina yao zimeibwa mkoani Tabora.

Kompyuta hizo zipatazo 30 zenye thamani ya Sh70 milioni, zimeibwa kwenye ofisi ya shirika lisilo la kiserikali la Jhpiego linaloshughulika na masuala ya Ukimwi na tohara.

Kompyuta hizo zimeibwa mwishoni mwa wiki kwenye ofisi hiyo iliyo jirani na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa amesema tayari taarifa za tukio hilo zimewafikia  na wanaendelea na uchunguzi wa kina kufahamu kilichotokea.

Inadaiwa kuwa kompyuta hizo, zina majina ya watu waliopima VVU na majibu yao.

“Kinachotatiza ni kwamba kama majina ya watu wenye virusi yakijulikana itakuwa ni utata mkubwa kwani ofisi hiyo itakuwa imewaweka katika wakati mgumu pasipo wao kupenda,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Mkurugenzi wa Jhipego, Dk Albert Komba amethibitisha kutokea kwa wizi huo.

JK azungumza Kuhusu Rais Magufuli Kutokwenda Zambia

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete ameunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli kuahirisha safari kwenda nje ya nchi ili kushiriki katika maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Kikwete amesema uamuzi huo ni wa busara kwa kuwa Serikali inatakiwa kufanya juhudi za makusudi kushughulikia tatizo hilo.

Kikwete aliyemtumia salamu za pole Dk Magufuli na waathirika wa tukio hilo, amesema misaada ya haraka na dharura inahitajika ili waathirika waendelee kupata huduma zote muhimu hasa za kibinadamu.

Kiongozi huyo mstaafu ameyasema hayo  katika hafla ya makabidhiano ya nyumba 22 za watumishi wa afya, 10 zikiwa Chalinze, mbili Bagamoyo na nyingine 10 Mafia zilizojengwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa mkoani Pwani.

“Ndugu zangu pamoja na leo hii tunakabidhiana nyumba 22 za watumishi wa afya mkoani kwetu, naomba tusimame tuwakumbuke wenzetu waliopoteza maisha katika tetemeko la ardhi huko Bukoba na pia natumia fursa hii kutoa pole kwa waathirika wote na Rais Dk Magufuli,” amesema.

Ameongeza kuwa: “kiukweli amefanya uamuzi wa busara kuahirisha safari yake ili kushiriki katika maafa haya.”

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Kituo cha Afya Msoga, Chalinze.

Jumatano, 14 Septemba 2016

Hatuhusiki kumtafutia mtu ajira - Bodi ya Mikopo

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imesema kuwa haihusiki kumtafutia mnufaika wa mkopo ajira badala yake inahusika kumpatia mwanafunzi mkopo na akishamaliza muda wa masomo atatakiwa kurejesha mkopo wake.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Cosmas Mwaisobwa wakati akijibu maswali ya wananchi kupitia kipengele cha Kikaango cha EATV.

“Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inatoa mikopo suala la kutafuta ajira halituhusu hivyo mnufaika yoyote asiwe na kigezo kwamba hajapata kazi , hiyo siyo kazi yetu, kazi yetu ni kuwawezesha kupata elimu basi” Alisema Mwaisobwa.

Aidha Mwaisobwa alisema wanufaika wote ambao walipata mikopo wanatakiwa kukatwa asilimia 8% ya pato la mwezi, na kama mtu anafanya kazi binafsi na hakatwi popote atatakiwa kutoa kiwango cha 120,000/= na kwa ambao wamenufaika na hawataki kuanza kulipa mkopo watapigwa penati ya 10% ya mkopo kwa mwaka.

Pamoja na hayo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imewataka walioomba mikopo kuvuta subira kwani Bodi inasubiri majina kutoka Tume ya Vyuo Vikuu ili Bodi ya Mikopo iweze kufahamu vyuo walivyopangiwa na kiwango cha ada ili haki iweze kutendeka kwa waombaji.

Gavana BOT afichua siri ya kilio cha fedha kupotea mtaani

 
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu jana alitolea ufafanuzi hali ya kiuchumi nchini huku akieleza siri ya kilio kinachovuma cha fedha kupotea mtaani na nyingine zikidaiwa kufichwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa Ndulu alisema kuwa kwakuwa taasisi hiyo ndiyo inayofahamu fedha zote zilizopo benki na zilizopo mtaani, inafahamu kuwa hakuna fedha iliyopotea bali fedha zimepotea kwa watu waliokuwa wanazipata kwa njia ya udanganyifu kwakuwa sasa Serikali imebana mianya hiyo.

“Hakuna fedha iliyopotea, Serikali imebana shughuli za watu na ‘mission town’ sasa shughuli zote zinafanywa na Serikali. Hivyo, kwao fedha zimepotea, lakini kwetu hazijapotea,” alisema Profesa Ndulu.

Hata hivyo, Profesa Ndulu alikiri kupungua kwa fedha katika mabenki nchini hali iliyopelekea kupunguza kasi ya utoaji mikopo kwa wananchi. Alisema hali hiyo ilitokana na kuhamishwa fedha za mashirika ya umma na taasisi kutoka benki za biashara kwenda BoT.

“Fedha hizo zitarudi katika benki hizo wakati zitakapopelekwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali,” Profesa Ndulu aliahidi.

Katika hatua nyingine, Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa uchumi unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.2 mwaka huu, huku akibainisha kuwa moja kati ya sababu zinazopelekea ukuaji huo ni  ongezeko la uzalishaji wa umeme na saraju.

Akizungumzia hali ya deni la taifa, alisema kuwa deni la taifa la ndani limeongezeka kutoka shilingi  trilioni 8.6 Mwezi Desemba mwaka jana hadi shilingi trilioni 10 mwezi Juni mwaka huu.

Profesa Ndulu alibainisha kuwa wakati deni linalotokana na kukopa ndani likipaa, deni linatokana na ukopaji wa limepungua baada ya Serikali kupunguza ukopaji nje ya nchi.


Watano kortini kwa kumdhalilisha Rais Magufuli

VIJANA watano wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha Rais Dk. John Magufuli na Jeshi la Polisi kutokana na mauaji ya askari polisi wanne waliouawa na majambazi katika eneo la Mbande na Vikindu, Dar es Salaam hivi karibuni.

Washtakiwa hao walifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya mahakimu watano tofauti na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Salum Mohammed.

Walisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru, Huruma Shahidi, Margareth Bankika, Dk. Yohana Yongolo na Respicius Mwijage.

Akisomewa mashtaka, mshtakiwa Dennis Mtegwa anadaiwa Agosti 24, mwaka huu eneo la Ubungo External kupitia mtandao wa WhatsApp, aliweka maoni katika group linaloitwa Dsm 11 4u Movement, akisema ‘JPM sijui anawaza nini kichwani… hata samahani hajui au nilikosea hajui’, ‘nchi imefika hapa kwa sababu ya mtu mmoja aliyeamua kujilipua ufahamu wake’, ‘sijaona tatizo kwa hilo, ila kwa huyu bwana misimamo ambaye amesema msinijaribu na ilhali kajaribiwa na ubwabwa wa jubilee kusema yote’.

‘Siasa si chuki wala upinzani si uadui, ajifunze kushindana kwa hoja sio mitutu ya bunduki na mazoezi yasiyo na kichwa wala miguu ya polisi’.

Mshtakiwa Suleiman Saidi anadaiwa Agosti 25, mwaka huu maeneo ya Kigogo, kwa kutumia mtandao wa Facebook, aliandika ‘Safi sana aisee, mi naona wangekufa kama 20 hivi halafu Simon Sirro tumuulize mazoezi wanafanyia wake zao au’.

Katika kesi nyingine, mshtakiwa Juma Mtatuu akiwa eneo la Ocean Road, Agosti 24, mwaka huu anadaiwa kuwa alituma ujumbe katika Facebook akisema ‘Huyu hata akifa ataenda peponi, na kufanya mazoezi kote kule wamekufa Mbagala, mimi nitakuwa wa kwanza kuandamana  kule Kahama, tarehe moja naelekea Kahama kwa Ukuta, mimi nitakuwa namba moja kushika bendera ya Ukuta, kifo kipo tuu, usiogope kwani mawe na mapanga yameisha’